Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chunya Mhe; BOSCO MWANGIDE amesema Serikali haitavumilia kuona uharibifu wa mazingira kwa sababu yoyote ile unaendelea kufanyika wilayani Chunya, Hivyo kila atakaye bainika kuharibu mazingira sheria, kanuni na taratibu zitazingatiwa ili kumuwajibisha mtu huyo
Mwanginde alitoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kitongoji cha Idendeluka kilichopo kijiji cha Sangambi kata ya Sangambi na kueleza msimamo wa serikali kuhusu uharibifu wa mazingira unaofanywa kupitia Uchomaji wa Mkaa katika kitongoji hicho.
“Wako watu ambao si waaminifu na wanaona miti hii kama ni zawadi yao peke yao, wanaanza kuifanyia fujo, wanaikata na kuwanufaisha wao peke yao kitu ambacho mimi kama mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Sitakubali kabisa kwani Mimi nipewa dhamana ya kusimamia shughuli za maendeleo Chunya hivyo katika kipindi change Mimi nitapambana nao sana hawa wanaoharibu Mazingira kwa manufaa yao”
Awali akitoa salamu kwa wananchi Diwani wa kata ya Chalangwa Mhe Haji Chapa amesema Mazingira hayana mipaka hivyo yeye kufika katika kata ya Sangambi ni kutambua umuhimu wa mazingira na hatimaye kushirikiana pamoja kuhakikisha mazingira yanatunzwa
“Uharibifu wa mazingira hauna mipaka kwani ukame hautasema miti imekatwa sana Idendeluka basi ukame utakuwa idendeluka, ukame utakuwa kote wilaya ya Chunya kwa ujumla, hivyo tumefika hapa ili tuweze kupambana kwa pamoja kuhakikisha tunalinda mazingira pamoja na uharibifu unaofanywa katika maeneo haya ni mkubwa sana”
Diwani mwenyeji wa Kata ya Sangambi Mhe JUNJULU NDETE amesema haiwezekani viongozi wetu wa kitaifa wanahangaika kupambana kuhakikisha mazingira yanalindwa lakini sisi tunaharibu mazingira bila utaratibu hilo halitavumiliwa kabisa
“Vyomba vya habari vinaeleza namna ambavyo makamu wa Rais Mhe Dkt Philip Mpango ameonekana maeneo mbalimbali akizindua program za kupanda miti maeneo mbalimbali je sisi ni akina nani tukate miti bila kupanda miti? Hili mimi sitavumila kabisa”
Innocent Lupembe afisa misitu Mkuu (TFS) wilaya ya Chunya amesema wilaya ya Chunya hasa katika kitongoji cha Idendeluka ina uharibifu mkubwa wa mazingira na ndio sababu kubwa iliyopelekea uwepo wa mkutano huo ili kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira ukizingatia eneo hilo mbali ya kuwa moja ya Chanzo cha Maji kuelekea bonde la usangu na hata maji kwaajili ya matumizi ya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo
Mabadiliko ya tabia nchi yanasababishwa na uharibifu wa Mazingira hasa ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa na kilimo jambo ambalo linahitaji nguvu za pamoja kuhakikisha uharibifu huo unakomeshwa ili kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza hapo Mbeleni ikiwepo ukame, njaa na hata mafuriko.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya ataendelea na ziara hiyo ya kutoa elimu kuhusu Utunzaji wa mazingira na kueleza msimamo wa serikali juu ya utunzaji wa mazingira tena leo 5/4/2023 katika kijiji cha Shoga ambapo mkutano wa hadhara utafanyika katika Kitongoji cha Tukuyu, Lengo likiwa ni kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kwa ustawi wa viumbe hai na jamii kwa ujumla.
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.