FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA UTALII
Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ina vivutio vya asili vya utalii na yapo maeneo ya kutosha yenye vivutio kwa ajili ya shughuli za utalii.
1.0 Mlima Mwene.
Halmashauri imebarikiwa kuwa na mlima mkubwa sana wa kihistoria ambao chifu wa Bungu alitaka kuuhamisha kutoka Kipembawe kwenda Wilaya Songwe Kwimba ili autumie kuhutubia wananchi wake, watu wengi walikufa kwa ajili ya zoezi hilo la kuubeba mlima na kuuhamisha kwa kuangukiwa na mawe. Mlima huu upo katika Kata ya Mamba takribani km 80 kutoka makao makuu ya Wilaya. Inaonesha kwamba katika mlima huu kuna nguvu ya asili zinazoambatana na machifu waliozikwa katika mlima huo, kumekuwa na maajabu mengi yakitokea katika mlima huo mfano kuku kuonekana akiwa na mguu mmoja n.k. unapoupanda utakutana na vivutio lukuki kama wanyamapori kama digi digi, Nyani, na aina mbalimbali za ndege kama Kanga, Kware na Njiwa wazuri. Mlima una sifa ya kuwa na kilele ambacho hutumika kuangalia maeneo ya mbali
2.0 Bwawa la Viboko Nzingwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imejaliwa kuwa na Bwawa kubwa la wanyama aina ya Viboko, wanyama hawa imekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutokana na muonekano wao, Inashauriwa kuwa eneo hili linatakiwa kuhifadhiwa kwani ni kivutio kikubwa cha utalii kutokana na aina hiyo ya wanyama kuwepo humo.
3.0 Pango la Kipembawe lililomeza watoto.
Wilaya ya Chunya ina pango la ajabu lililomeza watoto, pango hili linalopatikana katika kata Mafyeko Tarafa ya Kipembawe. Pango la Kipembawe limetokana jina la Tarafa hiyo. Pango hilo lina mwonekano mzuri wa kiutalii na unapolichungulia unaweza kuona giza nene ndani yake. Pango hili lina maajabu mengi sana ambapo ukifika katika eneo hili utajulishwa mambo mengi sana kuhusu historia ya pango hili.
4.0 Uwindaji wa kitalii.
Wilaya ya Chunya ina vitalu vizuri vya uwindaji wa kitalii ambapo Shughuli za uwindaji wakitalii hufanyika kila mwaka kuanzia mwezi julai hadi disemba. Uwindaji wa kitalii imekuwa kivutio kikubwa sana cha wageni. Shughuli za uwindaji wa kitalii zinafanikiwa kutokana na idadi kubwa ya wanyama wanaopatikana katika maeneo ya uwindaji. Wanyama wanaowindwa zaidi ni samba, nyati, chui palahara na kongoni wanyama hawa wanapatikana kwa urahisi hivyo kuvutia idadi kubwa ya wageni.
5.0 Soko la Dhahabu. (Utalii wa Madini)
Wilaya ya Chunya imekuwa ni eneo moja wapo lililobarikiwa kuwa na madini ya Dhahabu. Shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanyika wilaya ya Chunya imekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii, hadi sasa kuna soko kubwa la dhahabu linalopatika wilayani hapa ambapo shughuli za uuzaji na ununuzi wa dhahabu hufanyika.
Wilaya ya Chunya ina idadi kubwa ya mashine za uchakataji wa dhahabu kuna idadi kubwa ya makarasha yanayotumiwa na wachimbaji kwaajili ya uchakataji wa dhahabu. Wilaya bado inamaeneo makubwa ambayo yanahitaji uwekezaji kama vile mashine za kisasa kwaajili ya uchakataji wa dhahabu , n.k.
6.0 Ngoma za asili (Utalii wa utamaduni)
Wilaya ya Chunya imebarikiwa kuwa na ngoma maarufu za makabila makubwa yanayopatikana wilaya ya chunya ni pamoja na Waguruka na Wakimbu pamoja na makabila mengine yaliyohamia kama wangoni ngoma hizi zina mvuto sana kutokana na mazingira yake, Ngoma ya wakimbu zinapatikana zaidi katika tarafa ya Kipembawe, ngoma nyingine maarufu zinapatikana Chunya Mjini, ngoma hizi huchezwa na kabila la wangoni ambao kwa umoja wao hutumia vifaa kama filimbi zinazotokana na vibuyu ambavyohufungwa na naironi kwa lengo la kutoa sauti yenye mvuto, nyimbo nzuri huimbwa kulingana na matukio kama ni matukio ya sherehe za harusi basi nyimbo zenye mafunzo ya ndoa huimbwa na kama matukio ni ya huzuni hakika nyimbo za huzuni huimbwa zikiambatana na uwiano wa stepu unaofanana .
7.0 JENGO LA MAKUMBUSHO.
Wilaya ya Chunya imebarikiwa kuwa na jumba la makumbusho ambapo vitu vya kale, kazi za sanaa, na taarifa mbali mbali kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii zinapatikana. Aidha jumba la makumbusho lina mkusanyiko wa taarifa za kiutamaduni na mazingira asilia na wenyeji wa Chunya kabla na baada ya uhuru. Jumba la Makumbusho lina vitu asilia vilivyo tumika enzi za babu zetu wa kale mfano kuna nguo ya magome ya miti iliyovaliwa miaka ya 1800 iliyo ambatana na historia yake ambayo hadi sasa ina miaka takribani 200.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.