Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mbarak Alhaji Batenga amewataka wakina baba wote wilayani Chunya kuhakikisha wanawasaidia wake zao na wakina mama wengine waliopo katika maeneo yao kupata lishe bora kabla ya kubeba ujauzito, wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua kwani suala la lishe kwa mtoto huanzia Tumboni kwa mama yake
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Afya na lishe kwa ngazi ya kijiji yaliyofanyika tarehe 18/6/2024 katika kijiji cha Ifumbo kilicho katika kata ya Ifumbo, ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho hayo ambapo wilaya ya Chunya hufanya kila robo ya mwaka lengo ikiwa ni kuhimiza Afya bora na Lishe bora kwa mtoto na jamii kwa jamii kwa ujumla Mhe Batenga amesema wakina baba (wanaume) watambue kuwa hilo nalo ni jukumu lao
“Tukaboreshe lishe, hivi vitu (Vyakula katika Makundi mbalimbali ya Lishe) havitoki Mbinguni na vingine tukapande wenyewe ili tuwapatie lishe bora familia zetu. Wakinababa tuwasaidie wakinama ili wapate lishe bora maana suala la lishe linaanza tumboni na kwakufanya hivyo tutakuwa tumetekeleza vyema suala la kujali familia zetu” alisema Mhe Batenga
Akitoa taarifa ya hali ya Lishe wilaya ya Chunya, Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya Dkt Darison Andrew amesema wanaume wengi hawawajibiki ipasavyo katika kuhakikisha mama wajawazito wanapata lishe bora na sababu ni kukosekana kwa Elimu, ni tamaa yao kuona wanaume wakiambatana na wenza wao wanapokuja kliniki ili waweze kupata Elimu hiyo muhimu
“Ni tamaa yetu kuona wanaume wengi wanapata elimu hii sababu mtoto aliyedumaa hana mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Taifa na hata akisoma uelewa wake utakuwa mgumu sana, hivyo ni tamaa yetu mama mjamzito apate vyakula vyote kama vilivyowekwa kwenye meza ile na mtoto atakapotimiza miezi saba baada ya kuzaliwa akipata lishe bora itamjenga katika maisha yake yote”
Aidha, Dkt Darison Andrew ameongeza kuwa katika wajawazito 100, wajawazito 2 mpaka 9 wanakuwa na upungufu wa damu mwilini hivyo anakuwa na upungufu wa kinga mwili jambo ambalo linamuweka hatarini kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Amewaomba wananchi wa Ifumbo na Chunya kwa ujumla kuwapatia lishe bora wajawazito na kwakufanya hivyo itasaidia kupata Taifa lenye watu wenye afya bora
Kwa niaba ya wananchi wa kata ya Ifumbo waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo ya Afya na Lishe, Diwani wa kata ya Ifumbo Mhe. Weston Mpyila amesema suala la Lishe katika kata ya Ifumbo ni la lazima na wananchi wa Ifumbo wanazingatia hilo kwani mpaka sasa watoto wanapata Lishe wawapo nyumbani na hata wakiwa shuleni kwani vyakula vipo.
“Tunafanya jitihada kuhakikisha watoto wetu wanazingatia suala la lishe, sisi suala la lishe ni lazima sio ombi tena na wananchi wameitikia hivyo chakula kinatolewa katika Taasisi zote za shule za binafsi na Serikali, lakini pia kwenye kilimo tunafanya vizuri kwani vyakula vyote ulivyoona hapa mbele tunalima wenyewe hivyo sisi lishe sio tatizo”
Muhudumu wa Afya ngazi ya kata bwana Charles Jailos Ngazi amesema Elimu hii ya lishe huwa inatolewa mara kwa mara kwenye zahanati na vituo vyao vya afya huku akisema elimu hiyo imepokelewa vizuri na wananchi kwani mwitio wao ni mkubwa huku akirejerea idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza katika siku ya Afya na lishe.
Siku ya Afya na Lishe huadhimishwa na kila kijiji kwa kila Robo ya mwaka huku uongozi wa Halmashauri kwa maongozi wa maafisa lishe wa wilaya ya Chunya huchagua kuhudhuria katika maadhimisho ya kijiji kimojawapo ili kuongeza chachu ya kuthamini lishe pamoja pamoja na kutoa elimu Zaidi kuhusu lishe, kwa Robo hii ya nne uongozi ulitembelea siku ya afya na lishe katika kijiji cha Ifumbo ndani ya kata ya Ifumbo.
Baadhi ya vyakula vilivyletwa kwenye darasa la lishe wakati wa maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ngazi ya kijiji ambapo Mkuu wa wilaya ya Chunya alikwa Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo
Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mbarak Alhaji Batenga akifafanua faida za ubuyu kwenye Afya ya Binadamu wakati akizungumza na wananchi kwenye Maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ilifanyika kwenye kijiji cha Ifumbo
Mganga Mkuu wa wilaya ya Chunya Dkt Darison Andrew akifafanua jambo wakati wa maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe yaliyofanyika kijiji cha Ifumbo kilichopo kata ya Ifumbo
Diwani wa kata ya Ifumbo Mhe. Weston Mpyila akitoa salamu za wananchi wa kata ya Ifumbo kwa Mkuu wa wilaya ya Chunya wakati wa maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe yaliyofanyika ndani ya kata anayoiongoza ambayo ni kata ya Ifumbo
Wananchi wa Ifumbo wakiendelea kuburudika wakati wa maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe iliyofanyika kata ya Ifumbo katika kijiji cha Ifumbo
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.