Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ndugu Tamim Kambona amesema katika Uchaguzi huu hakuna mgombea atakayepita bila kupingwa bali kila mgombea atapaswa kupigiwa kura kwa mujibu wa Sheria, kanuni na miongozo, hivyo amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa wavumilivu na kutoa ushirikiano pindi watakapotakiwa kufanya hivyo ili kuhakikisha zoezi la Uchaguzi linaisha kwa Amani
Akizungumza kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya leo tarehe 26/09/2024 Msimamizi wa Uchaguzi amesema wapiga kura, wagombea na wadau mbalimbali wa Uchaguzi wanapaswa kupata maelekezo kuhusu utaratibu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakavyofanyika kuanzia hatua ya kujiandikisha mpaka hatua ya kupiga kura.
“Maelekezo yote muhimu yatawekwa ili wagombea na wapiga kura wayajue na kufuata ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na uwazi na kwa kuzingatia sheria zilizowekwa za uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema Kambona.
Aidha Kambona ametoa wito kwa wagombea wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyikaNovemba 27, 2024 ambazo ni wenyeviti wa vijiji, vitongoji na wajumbe Halmashauri ya vijiji kuchukua fomu katika Ofisi za msimamizi msaidizi wa Uchaguzi huku akiwataka wakazi wote wenye umri kuanzia miaka 18 au zaidi kushiriki kwenye uchaguzi huo wa serikali za mitaa.
Akitoa salamu za Serikali Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe Mbaraka Alhaji Batenga amesema katika uchaguzi wa Serikali za mitaa Wilaya ya Chunya inapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya siasa safi na kudumisha Amani wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi, lakini pia amewataka wanasiasa kuziishi na kuzitekeleza kwa vitendo sera ya 4R za Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuwaelimisha wafuasi wao ili kuendelea kudumisha Amani
“Sera ya 4R aliyokuja nayo Mhe Rais Samia ilikuwa ni kutibu matatizo ya kisiasa yaliyotokea kwenye uchaguzi uliopita, sera hii kwetu ni lazima kuitekeleza sio chaguo”amesema Mhe Batenga.
Viongozi wa dini akiwemo Sheikh wa Wilaya, Mwenyekiti wa Wachungaji Kanisa la Moravian Wilaya na mwakilishi wa wazee wa mila wameahidi kutoa ushirikiano kwa msimamizi wa Uchaguzi na Serikali kwa ujumla kuhimiza waumini wao kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kuanzia hatua ya kujiandikisha mpaka kupiga kura.
Mkutano huu wa maelekezo kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 umefanyika leo tarehe 26 Septemba, 2024 na umehudhuliwa na Viongozi wa Vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakilishi kutoka makundi mbalimbali kama vile wasafirishaji, vijana, wasanii, walemavu na makundi mengine mengi.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndugu Tamim Kambona akitoa maelezo kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe Novemba 27, 2024 mapema leo kwenye kikao kilichoketi kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Mwenyekiti wa Makanisa ya Moraviani wilaya ya Chunya Mchungaji Kayange akitoa nasaha zake kwa niaba ya Wachungaji baada ya Msimamizi wa Uchaguzi wa wilaya ya Chunya kuhitimisha kutoa maelezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024
Sheikh mkuu wa wilaya ya Chunya akitoa neno wakati wa Mkutano wa kutoa maelezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotaraji kufanyika Novemba 27, 2024, mapema leo kwenye ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Wananchi na wadau wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa waliojitokeza kwenye kikao cha Maelezo ya Uchaguzi kilichoketi mapema leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.