WANUFAIKA wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya wametakiwa kutumia mikopo hiyo kwa makini ili iwaletee manufaa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mh. Bosco Mwanginde wakati wa ziara ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ilipotembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri.
Mwanginde amewasisitiza wanufaika kuhakikisha mikopo wanayoipata wanaitumia kwa manufaa yao wenyewe na kujikwamua kiuchumi huku akiwataka wale wote ambao wamepatiwa mikopo kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili watu wengine waweze kukopa.
Vile vile Mwanginde amesema kuwa kuna dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa mikopo hiyo ni hisani kwamba haitakiwi kujereshwa, hivyo kuwataka wanufaika hao kuondokana na dhana hiyo na kuhakikisha wanarejesha tena kwa wakati ili kila mtu mwenye sifa anayehitaji mkopo huo aweze kupatiwa.
“Lengo la mikopo hii ni kuhakikisha wananchi wote wenye sifa ya kupata mikopo wanapata kwa lengo la kuwainua kiuchumi, ndio maana nasisitiza kuirejesha tena kwa wakati kwani hii mikopo sio hisani kama baadhi ya watu wanavyodhani” Alisisitiza Mh Mwanginde.
“Sisi tunajua tayari tumewapa pa kuanzia kinachotakiwa ni kuendelea kutafuta faida ili sasa msiendelee tena kuitegemea Serikali.” Aliongeza Mwanginde.
Pia Mwanginde alitumia fursa hiyo kukipongeza kikundi cha HAPA KAZI TU kwa mwenendo mzuri wanaokwenda nao na kurejesha mkopo waliopatiwa kwa muda muafaka.
“Maeneo mengi tunakopesha fedha na hazirudi lakini kwa taarifa ya Afisa Maendeleo ya Jamii, ninyi mnakwenda vizuri hongereni sana,” alisema Mh Mwanginde.
Kwa upande wa miradi mingine iliyotembelewa na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango Wajumbe wa Kamati wametoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ubora na ufanisi mkubwa
Aidha wajumbe wameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Miradi iliyotembelewa na kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ni pamoja na Vituo vya Afya Mafyeko, Kambikatoto na Sangambi, ujenzi wa nyumba ya watumishi 3/1 katika kituo cha afya Kambikatito, ujenzi wa majengo mbalimbali katika hospitali ya Wilaya
Kwa upande wa elimu kamati imetembelea mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Lualaje sambamba na Shule ya Sekondari Mayeka.
Aidha kamati imetembelea ukamilishaji wa ujenzi wa soko la madini pamoja na jengo la utawala
Wajumbe wa kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya halmashauri ya wilaya ya Chunya walipotembelea vikundi vya vijana wa Bodaboda waliopatiwa mkopo wa asilimia 10 na Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Afisa Maendeleo ya Jamii Ndg Vincent Msolla akitoa maelezo kwa Waheshimiwa madiwani wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipanga ya Halmashauri walipotembelea na Kukagua kikundi cha Bodaboda kilichopatiwa mkopo wa Asilimia 10 toka Halmashauri
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.