MKUU wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chunya na viongozi wake kwa ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya Sangambi.
Homera ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa alipokuwa wakikagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Chunya.
“Maeneo mengine nimepita, hii ni Halmashauri yangu ya sita, kote nilipopita waje wajifunze Chunya, kule nimepita hawajajenga majengo yote, wamejenga OPD tu, lakini Chunya mmejenga majengo ya kutosha kuanzisha kituo cha Afya." Alisema Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera.
Pia Mkuu wa Mkoa amewapongeza wananchi wa kata ya Sangambi kwa kujitolea nguvu kazi zao na kuhakikisha ujenzi wa kituo cha afya Sangambi unakwenda vizuri na kukamilika kwa wakati.
Miradi iliyotembelewa na kamati hiyo ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya Sangambi na ujenzi wa soko la madini ikiwa miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani.
Ujenzi wa kituo cha afya unakadiriwa kutumia kiasi cha shilingi milioni mia sita, ambapo kati ya hizo shilingi milioni 500 kutoka Halmashauri ya wilaya ya Chunya kama mapato ya ndani na milioni 100 kutoka kwa wananchi wa kata ya Sangambi.
"Mkurugenzi usione shida kuendelea kuleta miradi kwa wananchi wanaojitoa, kwa wananchi wanaojitolea sana wewe shusha miradi tu kwa sababu hawatuangushi.” Amesema Homera.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kuhakikisha ifikapo Mei mosi, kituo cha afya kianze kufanya kazi na kutoa huduma kwa wananchi wa Sangambi.
Kwa sasa wananchi wa kata ya Sangambi wanapata huduma kwenye kituo cha afya cha Charangwa ambacho kipo umbali wa kilomita 19 au kwenda kwenye hospitali ya Wilaya ya Chunya ambayo ipo umbali wa kilomita 32 kutoka Sangambi.
Kwa upande wa ujenzi wa soko la madini, Homera ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kuhakikisha ifikapo mwezi wa tano soko hilo liwe limekamilika na kuanza kutumika.
Pia, Homera amezita benki zote ambazo zimeonesha nia ya kuwekeza katika jengo hilo kuhakikisha wanaweka matawi yao ambayo yatakuwa msaada kwa wafanyabiashara wa dhahabu.
“Sisi tunawapa muda mpaka ifikapo mwezi wa tano hizo benki zote zilizoonesha dhamira ya kuwekeza katika soko hili wawe wameshafanya utaratibu wa kufungua matawi hapo vinginevyo tutaalika benki nyingine zije zifanye biashsara hapa.
“Hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atakuwa anatorosha dhahabu Wilayani Chunya tutachukua hatua kama ambavyo tumechukua hivi karibuni kutaifisha zaidi ya gram 900, dhamira yetu sisi kuuza kwenye soko letu hili ili Chunya iendelee kukusanya mapato, hatuwezi kujenga hapa watu wakauzie dhahabu vichochoroni tutachukua hatua kali.” Alisema Homera.
Jengo la Mama na Mtoto pamoja na Wodi katika Ujenzi wa Kituo cha Afya Sangambi
Jengo la OPD Ujenzi wa Kituo cha Afya Sangambi
Muonekano wa majengo Mengine katika Ujenzi wa Kituo cha Afya Sangambi
Soko la Dhahabu Linalojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kwa Mapato ya Ndani
Muonekano wa ndani katika Ujenzi wa Soko la Dhahabu
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.