Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Zuberi Homera ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi wa maji Matundasi ambapo unahudumia zaidi ya wakazi 9,000 katika vitongoji vya Matundasi A, B pamoja na kitongoji cha Kisimani.
Akizungumza leo, Februari 2, 2025 kwenye ziara ya kikazi alipokuwa akikagua mradi wa maji Matundasi uliopo katika kitongoji cha Kisimani wilayani Chunya , Mhe. Homera amesema suala la maji ni muhimu sana kwa wananchi ndio maana miradi ya maji inatekelezwa katika maeneo mbalimbali kwenye mkoa wa Mbeya huku dhamira ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani ni kumtua mama ndoo kichwani.
“Naupongeza uongozi wote wa Wilaya ya Chunya kwa kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji Matundasi na kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ilikuwa miongoni mwa waathirika wa ugonjwa huu, na ukweli ugonjwa umepungua na hatuoni magonjwa hata mmoja katika hospitali zetu” amesema Mhe. Homera.
Katika hatua nyingine, Mhe. Homera ametoa wiki mbili kwa meneja wa RUWASA Wilaya ya Chunya kuunganisha mtandao wa maji kutoka kwenye mradi kwenda kwenye makazi ya wananchi wa kitongoji cha Kisimani kwakuwa mradi wa maji upo kwenye eneo lao na ndipo ulipojengwa.
Dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani ni kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama kwenye kaya zao na sio kubeba maji kichwani, amesisitiza Mhe. Homera.
“Haiwezekani mtandao wa maji uende kwenye vitongoji vingine vya mbali halafu kitongoji hiki cha kisimani ambapo mradi umetekelezwa wakose maji, wananchi wa Kisimani ndio walinzi wa miundombinu hii ya mradi wa maji, natoa siku 14 Kitongoji cha Kisimani kuunganishiwe maji kama vijiji vingine” amesema Homera.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji Matundasi uliopo katika kijiji cha Kisimani, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Chunya, ndugu Shabibu Ayubu amesema mradi wa maji Matundasi umetekelezwa kwa Shilingi Milioni 350 kwa ufadhili wa P4R, mradi ulianza April 14, 2024 na kukamilika tangu Agosti 15, 2024.
Pump iliyofungwa kwenye mradi wa maji Matundasi ina uwezo wa kuvuna maji lita 17,500 kwa saa. Mradi wa maji Matundasi umekamilika kwa asilimia mia moja na unahudumia wakazi zaidi ya 9,000 wa vitongoji vya Matndasi A, B na kitongoji cha Kisimani. Amesema Ayubu.
Mkuu wa Mkoa Mbeya, Mhe. Juma Himera akisikiliza taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji Matundasi iliyosomwa na Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Chunya, ndugu Shabibu Ayubu.
Muonekano wa Tanki la maji katika mradi wa maji Matundasi ambao unahudumia zaidi ya wakazi 9,000 katika vitongoji vya Matundasi A, B pamoja na Kitongoji cha Kisimani.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.