Mbunge wa Jimbo la Lupa Mhe Masache Njelu Kasaka amesema serikali itatoa ruzuku kwenye Mbolea itakayotumika kwenye zao la Tumbaku jambo ambalo ni tofauti na msimu uliopita ambapo ruzuku ya Mbolea haikulenga zao la Tumbaku jambo ambalo lilichangia wakulima kuwa na gharama kubwa katika uzalishaji wa zao hilo hivyo kuathiri vipato kwa mwananchi mmoja mmoja.
Amesema kauli hiyo mapema leo tarehe 08/10/2023 wakati akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Malangamilo na Mkola kwa nyakati tofauti ambapo amefika katika vitongoji hivyo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya Kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Lupa ili kuwapa mrejesho wa Bunge la Bajeti pamoja na namna ambavyo serikali inayoongozwa na Mhe Samia Suluhu Hassan inavyotatua kero za wananchi katika Nyanja mbalimbali.
“Tumefanikiwa kufufua kilimo cha Tumbaku kwenye kata ya Mkola na tayari chama chetu cha Ushirika kinafanya kazi vizuri lakini Changamoto ilikuwa Mbolea ambapo serikali haikuweka Ruzuku kwenye mbole inayohusiana na zao la Tumbaku lakini kwakusikia kilio cha wananchunya serikali imekubali kutoa Ruzuku ya Mbolea kwenye zao hilo la Tumbaku na Tayari Mbolea imeshafika kwenye ghara kuu la Mkoa wa Mbeya hivyo niwahakikishie kwamba mtaipata mapema na kwa wakati”.
Katika kujibu kero ya Maji inayowakumba wanachunya wakiwepo wananchi wa Kata ya Mkola na vitongoji vyake Mhe Masache amewataka wananchi wawe na subira kwani mradi unaotekelezwa na serikali ili kuwahudumia wananchi wa kata ya Mkola utakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa hivyo mwezi Desemba wananchi wa Mkola watapata maji safi na salama kwani fedha zimeshatolewa kwaajili ya utekelezaji wa mradi huo.
“Miezi mitatu ndugu zangu sio mingi mniamini mtoto wenu nipo kazini kutekeleza kile mlichonituma, tumesubiri muda mrefu sana hatuwezi kushindwa kusubiri miezi mitatu kwani mradi unaotekelezwa katika kata ya Mkola ili kutatua kero ya maji pesa zake zimeshaletwa (Milioni mia moja) nawahakikishia kufikia Desemba mwaka huu wananchi wa mkola mtapata maji safi na salama, na mwezi Desemba nitakuwepo hapa ili tuzindue pamoja kutumia maji safi na salama” amesema Mhe Masache.
Akijibu kero za wananchi Mhe Masache amewataka wananchi kununua dhahabu kwenye eneo la machimbo katika kata hiyo kama miongozo ya serikali ilivyoelekeza huku akiwataka wataalamu wa madini kusimamia utaratibu wananchi wanunue dhahabu kama miongozo, taratibu na kanuni zinavyoelekeza huku akiwakumbusha kwamba serikali inasisitiza biashara huria hivyo wasimamie taratibu.
“Nimepata taarifa kwamba kwenye kata yenu kuna eneo kuna machimbo ya dhahabu lakini watu wa madini wametoa maelekezo kwamba mnunuzi wa dhahabu awe mmoja jambo ambalo limepelekea mnunuzi huyo kuelemewa na matokeo yake wananchi kuanza kuhangaika, sasa mimi nasema Ruksa kununua dhahabu katika machimbo hayo, watu wa Madini kazi yao ni kusimamia utaratibu na sio kuteua mnunuzi mmoja, hayo sio maelekezo ya serikali, serikali imesema soko huria, hivyo wananchi kanunueni dhahabu kwa uataratibu uliowekwa na serikali”.
Awali akimkaribisha Mbunge wa jimbo hilo, Diwani wa kata ya Mkola Mhe. Mbwiga M. Mwasongole amewataka wananchi kuuliza maswali yenye kujenga kata hiyo na yenye tija huku akiwakumbusha wananchi kwamba jimbo la Lupa lina kata ishirini (20) hivyo nafasi ya kuonana na Mbunge inaweza kuwa finyu kulingana na ukubwa wa jimbo hilo hivyo amewashauri kuuliza maswali yenye tija na yenye kuleta maendeleo ya kata ya Mkola na vitongoji vyake.
Steven Michael na Mchungaji Elisha Luvanda wamewawakilisha wananchi wengine kupeleka kero kwa Mhe. Mbunge na kero zao zilikuwa kutounganisha umeme kwa wakati, kukosa wahudumu kwenye zahanaiti na vituo vya afya pamoja na ukosefu wa Soko katika kata hiyo ya Mkola. Kero zote zimepatiwa majibu wakati wa mkutano huo.
Ziara ya Mhe Mbunge leo imehusisha kitongoji cha Malangamilo na kitongoji cha Mkola na awali kikao cha viongozi wa Chama na Serikali ngazi ya kata kimeketi kujadili mambo mbalimbali na ziara hiyo inataraji kuendelea tarehe 10/10/2023 katika kata ya Chalangwa na baadaye tarehe 11/10/2023 ziara itahitimishwa kata ya Ifumbo.
Baadhi ya wananchi katika Picha waliojitokeza kumsikiliza Mbunge wa Jimbo la Lupa Mhe Masache Njelu Kasaka wakati alipotembelea Kitongoji cha Mkola Kilichopo kata ya Mkola
Mbunge wa jimbo la Lupa Mhe Masache Njelu Kasaka akisalimiana na wananchi waliojitokeza baada ya kumaliza kuzungmza na wananchi wa kitongoji cha Mkola
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.