Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Zuberi Homera ampa heko Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chunya kwa kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo jengo la baba, mama na mtoto lilojengwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa kuzingatia thamani ya fedha na usawa wa jinsia kwenye utoaji huduma.
Mhe. Homera ameyasema hayo leo Februari 11, 2025 wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili kwenye ukaguzi wa jengo la baba, mama na mtoto lililopo Hospitali ya Wilaya ya Chunya, ambapo pamoja na mambo mengine Mhe. Homera amekagua maendeleo ya ujenzi wa stendi mpya ya kisasa, ujenzi wa uwanja wa michezo, na ujenzi wa karavati uliopo jirani na jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
“Natoa pongezi Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya, Mwenyeti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, tumefanya ziara nzuri tangu jana tulipoanza na leo ni siku ya pili tunahitimisha ziara hii, miradi imejengwa kwa kiwango cha juu sana, mafanikio ni makubwa na thamani ya fedha inaonekana, naamini kwa namna tunavyotekeleza miradi tunaenda vizuri kwa mkoa wa Mbeya” amesema Homera.
“Tunachohitaji sisi ni kuona thamani ya fedha tunapokuja kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi ya maedneleo, nimeambiwa hapa jengo la baba, mama na Watoto limegharimu milioni 258 na ukiangalia hapa unaona kabisa jengo limekidhi viwango lakini pia jengo hili limezingatia usawa wa kijinsia ambapo wakinababa, wakinamama na Watoto wanapata huduma za afya” amesema Mhe. Homera.
Katika hatua nyingine Mhe. Homera amesisitiza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na shule katika ngazi ya msingi na sekondari kuripoti shuleni kabla ya Machi 15, 2025 vinginevyo hatua kali za sheria zitachuliwa dhidi ya wazazi na walezi walioshindwa kuwapeleka wanafunzi shuleni.
“ Mpaka ikifika Machi 15, 2025, wakuu wa Wilaya wote, Wakurugenzi wote, maafisa elimua na Maafisa elimu kata wahakikishe wanafunzi wote waliopaswa kuanza masomo wawe shuleni haswa wa kidato cha kwanza” amesema Mhe. Homera.
Akiwa kwenye ukaguzi wa ujenzi wa karavati, Mhe. Homera amefurahishwa na utekelezaji wa agizo lake la ujenzi wa karavati alilolitoa Februari, 2023 wakati wa ziara ya kikazi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
“Febrauri, 2023 nilitoa agizo kwa Ofisi ya TARURA wilaya ya Chunya kujenga karavati kwaajili ya watumishi, wananchi kupita kwenye eneo hili la mto ili wakapate huduma mbalimbali kwenye jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, nimefurahi ujenzi wa karavati umeisha na umerahisisha mawasiliano kwa wananchi kupata huduma za kiserikali kwa kufika kwa urahisi ofisi ya Mkurugenzi” amesema Mhe. Homera.
Naye Hanifa Rajabu mtumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya amemshukuru Rais watanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha ya ujenzi wa karavati ambapo imeondoa adha ya kuvuka barabara hiyo wakati wa mvua lakini pia imesaidia kurahisisha kufika kituo cha kazi kwa wakati.
Vilevile, Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera amekagua ujenzi wa standi mpya ya kisasa ya mabasi ya Wilaya ya Chunya huku akimtaka mkandarasi kufanya kazi muda wa ziada ili kukamilisha ujenzi wa standi mwezi Juni, 2025.
“Sisi lengo letu ni kuja kuizindua standi ya mabasi ya kisasa mwezi Juni, 2025 ili wananchi waendelee kupata huduma za usafiri lakini pia mkandarasi unatakiwa kuchangia jamii(CSR) inayokuzunguka kwa kuwa serikali imekupa zabuni ya ujenzi wa standi unaogharimu Tsh. Bilioni 2.8, na tayari umeshalipwa Milioni 400 kama kianzio” amesema Mhe. Homera.
Awali akikagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Homera amempongeza mwenyekiti wa kamati ya ujenzi kwa kazi kubwa ya ujenzi wa uwanja
“ Kazi kubwa kwenye uwanja ni uzio pamoja na sehemu ya uwanja (Pitch) na nimeambiwa mumeshagiza nyasi, ila sasa nyasi mulizoagiza muweke maboresho kuwe na jina la uwanja pamoja na kuendelea kujiunga mkono timu ya mpira wa miguu ya Ken Gold ambayo ni timu ya wanachunya” amesema Mhe. Homera.
Naye mhandisi wa Wilaya ya Chunya, Charles Kway amesema, uwanja wa mpira upo kwenye hatua nzuri ambapo nyasi tayari zimeshaagizwa na zinatarajia kufika nchini baada ya miezi mawili.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliambatana na viongozi wa chama cha Mapinduzi, viongozi wa serikali, wataalamu kutoka Mkoa na Halmashauri pamoja na kamati ya ulinzi na usalama kutoka mkoa wa Mbeya na Wilaya ya Chunya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera akikagua ujenzi wa mradi wa standi mpya ya kisasa ya Mabasi Wilaya ya Chunya. Standi mpya ya Mabasi inajengwa katika Kata ya Itewe jirani na Sheli ya LY.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera akitoa maelekezo kwa mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi wa standi mpya ya kisasa ya Mabasi Wilaya ya Chunya. Standi mpya ya Mabasi inajengwa katika Kata ya Itewe jirani na Sheli ya LY.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera akitoa maelekezo kwa mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa mradi wa Uwanja mpya wa michezo wa Wilaya ya Chunya. Uwanja wa michezo unajengwa katika Kata ya Mbugani katika Wilaya ya Chunya.
Muonekano wa uwanja wa michezo wa Wilaya ya Chunya unaendelea kujengwa katika Kata ya Mbugani Wilaya ya Chunya.
Baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Chunya wakimsiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mara baada ya kuwasili kukagua mradi wa ujenzi wa Karavati.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera akifurahia jambo mara baada ya kukagua ujenzi wa Karavati liliwarahishia wananchi kupita njia kuelekea jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kupata huduma mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Hospitali ya Wilaya ya Chunya kukagua ujenzi jengo la huduma ya baba, mama na mtoto.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.