MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Mh. Bosco Mwanginde, amewataka Madiwani na wataalam wa Halmashauri kushirkiana katika ukusanyaji wa mapato.
Mwanginde ameyasema hayo akifungua Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, robo ya pili kwa mwaka 2021/2022, uliofanyika Machi 11, 2022 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali toka vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo.
Katika Mkutano huo, Mwanginde amesema, makusanyo ya Halmashauri yameongezeka kwa asilimia 23 kutoka asilimia 37 kwa kipindi kilichopita cha robo mwaka ukilinganisha na kipindi cha sasa cha robo mwaka.
“Makusanyo ya jumla ya Halmashauri kuanzia Julai hadi Desemba 2021 yameongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na kipindi kilichopita cha robo ya pili kama hii tulikuwa na asilimia 37 lakini leo tuna zungumzia asilimia 60.” Alisema Mwanginde.
Aidha, Mwanginde alisema, hadi kufikia Desemba 2021, mapato ya Halmashauri yaliongezeka kwa asilimia 31 baada ya kukusanya bilioni 3.2 ambayo ni sawa na asilimia 68.
“Mapato yetu ya ndani hadi kufikia Desemba 2021 yamefikia shilingi bilioni 3.2 sawa na asilimia 68% ambapo ni takriban mara mbili ya makusanyo ya mwaka uliopita kwa kipindi kama hiki tulikuwa na asilimia 37%.”
Mh. Mwanginde alisisitiza kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Halmashauri inafikia malengo ya asilimia 100 ya ukusanyaji wa mapato.
“Pamoja na hayo tunahitaji sana kuongeza juhudi kwa maana kwamba tusibweteke kwa sababu tayari tupo katika nafasi nzuri, kikubwa tutambue bado hatujafikia asilimia 100, hivyo ni jukumu letu sasa kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji.” Alisema Mh. Mwanginde
Kadhalika, aliwataka Madiwani kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa watendaji na viongozi mbalimbali wa Halmashauri pindi wanapopita katika maeneo yao kwa ajili ya kukusanya mapato.
“Sisi kama madiwani tuendelee kutoa ushirikiano kwa wataalam na watendaji mbalimbali wanapokuja kwenye maeneo yetu.”
Aidha, Baraza la Madiwani, limewataka wakala wa barabara za vijijini (TARURA) kuhakikisha barabara zote ambazo zipo kwenye matengenezo ziwe zimekamilika hadi kufikia mwisho wa mwezi huu.
“Tunawaagiza ndani ya mwezi huu, barabara tayari zina wakandarasi na wakandarasi wanasuasua, ziwe zimekamilika ili kuwaondolea kero wananchi hasa ikiwemo barabara ya Lualaje.” Alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bosco Mwanginde.
Kadhalika, Baraza limewataka TARURA kuhakikisha wanabadilika na kufanya kazi kwa wakati ili kuweza kutatua changamoto ambazo zinawakumba wananchi pindi barabara zinapoharibika.
“Fedha hizi ni za Serikali, zinatakiwa zihudumie wananchi wa Chunya kwa wakati kama ambavyo zimekwenda kutengeneza madarasa ya UVIKO-19, kama ambavyo zimekwenda kutengeneza vituo vya afya na zahanati kwa wakati hata fedha za TARURA zinatakiwa ziende kwa wakati.
Hili ni onyo la mwisho kama mpaka mwezi mmoja hamjakamilisha barabara zote ambazo muda wake umeisha basi tutachukua hatua kama baraza la madiwani”. Alisisitiza Mh. Mwanginde
Waheshimiwa Madiwani pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria, wakifuatilia Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Chunya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndg Tamim Kambona akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani
Waheshimiwa Madiwani wakiwa kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.