MDAU wa Maendeleo Wilaya ya Chunya Bi. Veronica Masache amechangia mifuko 20 ya saruji katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya cha Lupa.
Bi. Veronica ambaye ni mke wa mbunge wa Jimbo la Lupa ametoa mchango huo Machi 5, 2022 kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyofanyika kiwilaya kwenye Kata ya Lupa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
“Mimi kama mama katika zoezi zima mlilolianzisha la ujenzi wa wodi ya mama na mtoto kwenye kituo chetu cha afya cha Lupa niliwaahidi tutakuwa pamoja kwenye hili,” alisema Bi Veronica.
“Na kwa kuanza, leo naomba nikabidhi mifuko ishirini ya saruji, kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo chetu cha afya hapa Lupa, huu ni mwanzo, tutaendelea kujitoa na tuendelee kuonesha jitihada kwa sababu hili linafanyika kwa ajili yetu sote.” Alisisitiza Bi Veronica.
Wanawake wa jamii ya Lupa kufuatia changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakati wanakwenda kupata huduma za afya kwenye kituo cha afya, zimewapelekea kuanzisha mchakato wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto ili kutatua kero wanazokumbana nazo.
Kwa upande mwingine Bi. Veronica amewasisitiza wanawake na wote walioshiriki katika maadhimisho hayo kujitokeza kuhesabiwa wakati wa zoezi la sensa litakapowadia.
“Mwaka huu ni mwaka wa sensa, itakapofika kipindi cha sensa tujitokeze tuhesabiwe, maendeleo yana nyanja nyingi sana, ikijulikana idadi ya kaya zetu na watu ni moja ya kuleta maendeleo katika jamii zetu hivyo tulizingatie hilo.” Alisema Bi Veronica.
Aidha amewataka wanawake wahakikishe wanaitumia fursa iliyotolewa na Mh. Rais Samia Suluhu Hassan ya wanafunzi wa kike waliopoteza nafasi ya kusoma kuwarejesha mashuleni ili wakapate elimu.
Akisoma risala ya wanawake Kata ya Lupa, Bi. Dorice Paul Boma, alitaja baadhi ya changamoto ambazo wanakabiliana nazo kuwa ni uhaba wa watoa huduma za afya katika kituo cha afya pamoja na ukosefu wa nyumba za watumishi.
“Sisi wanawake wa Lupatingatinga kwa pamoja tumetambua na kuona changamoto kubwa tunazokumbana nazo katika kituo chetu cha afya zinatuathiri moja kwa moja, hivyo tukaazimia kuanzisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto, eneo hili sio muhimu tu kwa jamii ya wanalupa bali pia litasaidia jamii za jirani hasa katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua.” Alisema Bi Dorice.
Aidha, kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inasema, "Kizazi cha Haki na usawa kwa Maendeleo Endelevu, Tujitokeze Kuhesabiwa", ambapo maadhimisho hayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8.
Bi Veronica Masache Akikabidhi Risiti ya Manunuzi ya Saruji kwa Mwenyekiti wa Kamati katika Maadhimisho wa Siku ya Wanawake wilaya ya Chunya yaliyofanyika Katika kata ya Lupa
Afisa Maendeleo ya Jamii halmashauri ya wilaya ya Chunya Bw. James Sunge akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri katika Maadhimisho ya siku ya wanawake ambapo kiwilaya yalifanyika kata ya Lupa
Umati wa Wananchi waliojitokeza katika Maadhiisho ya siku wa Wanawake Kiwilaya kata ya Lupa halmashauri ya wilaya ya Chunya
Katibu wa Maandalizi ya Serehe ya kilele cha Siku ya Mwanamke Bi Dorice Boma Akiwasilisha risala ya Wanawake wa Jamii ya Lupa kwa Mgeni rasmi maadhimisho hayo kiwilaya yamefanyika Kata ya Lupa Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Vijana wakike wakionyesha Umahiri wao wakuruka sarakasi kwenye madhimisho ya siku ya wanawake wilaya ya Chunya katika kata ya Lupa
Wanawake wakiwa kwenye Maadhimisho ya Siku yao Kiwilaya imefanyika kata ya Lupa Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.