Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Alhaji Batenga amewataka watumishi wa umma kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kushughulika na shida za wananchi kwa kuzingatia haki, usawa na utawala bora ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na stahiki.
Mhe. Batenga ameyasema hayo leo Machi 4, 2025 wakati akizindua mafunzo ya siku ya moja ya elimu ya uraia na utawala bora yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwanginde Hall uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, jengo jipya na yaliyoendeshwa na Wizara ya Katiba na Sheria ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha utendaji kazi na utawala bora kwa watumishi wa umma nchini.
“Wananchi wana kero zao na ndio shida zao, twendeni tukahangaike na shida za wananchi kwasababu utendaji kazi wa serikali upo katika ngazi ya Wilaya kuanzia kwenye Tarafa, Kata, Kijiji, Kitongoji na mitaa na ndipo wananchi walipo” amesema Mhe. Batenga.
Aidha, Mhe. Batenga amesema, wenyeviti wa vijiji, vitongoji anaweza wakafanya wananchi wakaipenda au wakaichukia serikali kwasababu viongozi hao wanakutana na wananchi mara kwa mara hivyo ni muhimu viongozi hao kufahamu majukumu na nafasi walizonazo kiutendaji.
“Wiki moja baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa, mimi niliwaita watendaji wa kata, vijiji, wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa vitongoji pamoja na wajumbe wote wa serikali za vijiji kuwapa semina elekezi ya mafunzo ya uongozi ili kujua namna ya kwenda kuwahudumia wananchi na kujenga uhalali wa serikali kukubalika kuanzia ngazi za chini” amesema Mhe. Batenga.
Mhe. Batenga amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kutoa haki kwa wakati kwakuwa uelewa wa wananchi umeongezeka katika kutambua haki zao. Ameongeza kuwa, wananchi wanazijua na kuzidai haki zao, hivyo, viongozi wasisubiri wananchi wadai haki zao, wananchi wakidai haki zao hiyo haki inakuwa imecheleweshwa na haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa.
“Naomba niwaahidi kuwa, watumishi wangu ni waaminifu na wataenda kutekeleza majukumu yao kulingana na mafunzo waliyoyapata kupitia Wizara ya Katiba na Sheria” amesema Mhe. Batenga.
Naye, Wakili wa serikali na mratibu wa mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili Prosper Alexander Kisinini amesema lengo la mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora ni kuwajengea uwezo viongozi na watendaji ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Huu ni mwanzo wa kujenga nchi salama kupitia kuongeza uzingatiaji wa masuala ya haki, ulinzi na usalama Wizara ya Katiba na Sheria ina matumaini makubwa na mafanikio ya mafunzo haya” amesema Wakili Kisinini.
Winnie Michael, Mtendaji wa Kata ya Bwawani, Wilaya ya Chunya amewashukuru wawezesehshaji wa mafunzo ya uraia na utawala bora huku akiahidi kwenda kutekeleza kwa vitendo ili kuwahudumia wananchi wa Kata ya Bwawani.
Mafunzo ya siku moja ya elimu ya uraia na utawala bora yametolewa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya wakiwemo watendaji wa kata, maafisa ardhi, maafisa ustawi wa jamii, maafisa maendeleo ya jamii na kuhudhuriwa na viongozi wa ulinzi na usalama Wilaya ya Chunya.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga akiwa kwenye picha ya pamoja na wakufunzi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na washiriki wa mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora kutoka Wilaya ya Chunya katika Ukumbi wa Mwanginde uliopo jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, leo Machi 4, 2025.
Afisa Uchaguzi, Tume ya Haki za binadamu na utawala bora, ndugu Paul Sulle akiwasilisha mada ya demokrasia na Utawala Bora kwa washiriki wa mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora katika ukumbi wa Mwanginde uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
Washiriki wakisikiliza kwa makini mada mbalimbali zilizowasilishwa kwenye mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora katika ukumbi wa Mwanginde uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, jengo jipya.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.