Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mayeka S Mayeka amewataka wananchi wa wilaya ya Chunya kuanza kuchukua tahadhari mbalimbali ili kukabiliana na majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua zinazoweza kunyesha msimu huu kama wataalam wa Mamlaka ya Hali ya hewa Nchi walivyotahadharisha uwepo wa Mvua kubwa katika Msimu wa Mvua unaotarajiwa kuanza hivi karibu.
Ametoa rai hiyo leo tarehe 30/10/2023 maeneo ya kijiji cha Lola na kijiji cha Upendo vilivyo kata ya Upendo wakati alipofanya mikutano na wananchi ikiwa ni sehemu ya ziara ya kawaida ya kusikiliza kero za wananchi, kuzitatua na zile zitakazoshindikana kwa wakati huo kuzitafutia suluhu yake kupitia viongozi mbalimbali wanaohusika.
“Kutokana na maelekezo ya wataalam wa Hali ya hewa nchini inawezekana tukapata Mvua nyingi kuliko kiwango tulichozoea hivyo naomba tujiandae kwanza kutunza chakula cha kutosha ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, pili tujiandae kuwa na Mbegu zinazoweza kustahimili maji mengi lakini pia tuandae maeneo yanayoweza kutumika yatakapotokea mafuriko katika maeneo yetu”.
Aidha Mkuu wa wilaya ya Chunya ametaka serikali za vijiji kuanza kutenga maeneo ya kutosha kujenga miundombinu mbalimbali ya kijamii kama vile shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na miundombinu mingine tofauti na ilivyo sasa ambapo serikali za vijiji hawana ardhi matokeo yake kila mradi unapokuja serikali inaanza kuomba maeneo kwa wananchi jambo hili halikubariki kabisa.
“Anzeni sasa kutenga maeneo au kuomba ardhi karibu na zahanati hii maana Lola inakuwa, watu wanaongezeka mtahitaji kujenga kituo cha afya hivyo eneo zaidi litatakiwa. Hii tabia ya kuwaomba wananchi aridhi kila wakati serikali inapotaka kujenga miundombinu ni jambo ambalo haliwezekani ni lazima serikali za vijiji muanze kuwa na benki za aridhi” aliongeza Mhe Mayeka.
Akitoa salamu za wananchi wa kata ya Upendo Diwani wa kata hiyo Mhe Richard N. Itelekelo amemshukuru Mhe Rais kwa kuendelea kumwamini Mkuu wa wilaya ya Chunya na kuendelea kumuacha aendelee kuwepo wilaya ya Chunya lakini pia ameshukuru kuwapa fedha Milioni 50 katika kijiji cha Lola ili wajenge zahanati ambayo itawapunguzia wananchi umbali wa kutembea kufuata huduma za afya.
Ziara hiyo ya Mkuu wa wilaya na kamati ya usalama imedumu kwa siku moja, Pamoja na kero mbalimbali za wananchi katika kata ya Upendo kupatiwa majibu Mkuu wa wilaya ametembelea Zahanati ya kijiji cha Lola ambayo imepelekewa fedha shilingi milioni Hamsini na serikali kwaajili ya kuikamilisha, lakini pia ametembelea shule ya sekondari ya kata ya Upendo inayojengwa katika kata hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wa upendo wanapata huduma bora wakiwa kwenye mweneo yao.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mayeka (anaye andika) akinukuu kero zinazowasilishwa na wananchi katika kijiji cha Lola mapema leo
Mkuu wa wilaya ya Chunya (aliyesimama na amenyoosha mkono) akijibu kero za wananchi katika kijiji cha Lola wakati alipofanya zaiara ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia majibu
Mkuu wa wilaya ya Chunya akizungumza na wananchi waliojitokeza baada ya kukagua ujenzi wa Zahanati inayojengwa Lola
Mkuu wa wilaya (aliyenyoosha mkono wake wa kulia) akioneshwa mipaka ya Shule ya sekondari Upendo(aliyenyoosha mkono wake wa kushoto Diwani wa kata ya Upendo)
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.