MGENI RASMI KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA MH. MKUU WA WILAYA YA CHUNYA BI.REHEMA MADUSA MWENYE KOTI LA BLUU (katikati), HAKIMU MFAWIDHI WA MAHAKAMA YA WILAYA NDG. OSMUND NGATUNGA (kushoto kwake), AKIWA KWENYE PICHA YA PAMOJA NA WANASHERIA, MAWAKILI NA WADAU MBALIMBALI WA SHERIA.
Chunya.
Siku ya Sheria Nchini Tanzania iliadhimishwa kiwilaya tar. 1/2/2018 ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya wiki ya sheria
Nchini..
Shughuli mbalimbali zilifanyika katika wiki hiyo ikiwa ni Pamoja na kutoa Elimu ya sheria kwa Wananchi walioko maeneo
(kata) mbalimbali ya wilaya ya Chunya.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mh. Rehema Madusa aliyeambatana na kamati ya
Uilnzi na Usalama, Pamoja na Viongozi wa Dini.
Kauli Mbiu katika Maadhisho hayo ilikua ni "Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa wakati na kwa kuzingatia Maadili"
Mada mbalimbali ziliwasilishwa na Wataalam mbalimbali wa Sheria ambapo kwa kuanzia Mwendesha Mashtaka katika Wilaya ya
Chunya Ndg.Raymond Lukomwa, alitoa salamu zake kwa kusisitiza kuwa Mahakama ni Chombo kinachosimamia Haki. Hivyo
aliwasisitizia Wananchi kupeleka Malalamiko yao Polisi na Uchunguzi unapokua umekamilika Malalamiko hayo hupelekwa
Mahakamani kwa ajili ya uendeshaji wa Kesi.
Mwanasheria katika H/W Chunya Ndg.Egito Bilali aliwasilisha Mada juu ya Ndoa. na kueleza kuwa ndoa ni Taasisi ya mwanzo na
ya zamani zaidi kwa mujibu wa Vitabu vya Dini, na ni Muungano wa hiari kati ya mwanaume na Mwanamke kwa muda wote watakao
kuwa Duniani.
katika kuelezea aina za ndoa zilizopo kisheria alisema ni pamoja na Ndoa ya Mme mmoja na Mke mmoja(kwa wakristo), Mme na wake
wengi(kwa waislamu), Ndoa ya kiserikali(ni Jukumu la Wahusika kuamua.) na Pamoja ile ya kimila ambayo ni ya Wake Wengi.
Pia aliendelea kutanabaisha kuwa Uchumba wenye masharti pindi utakapovunjika basi huambatana na fidia, na Mahali hutoka kwa Mwanaume
kwenda kwa Mwanamke na ndoa ambayo haijalipiwa mahali ni batili na zaidi mahali si kigezo cha kuhalalisha ndoa.
Alisema kuwa Ndoa batili ni ile ambayo imefungwa lakini Sheria Haiitambui. alisema kuwa mwanamke mwenye umri Mdogo kama miaka 15
anaweza kuolewa ila kwa ridhaa ya wazazi/walezi.
aliendelea kueleza kuwa ndoa batili ni ile iliyofungwa kati ya watu wenye Undugu wa damu, kama mmoja wa wenye ndoa hakuwa
hiari, Wahusika hawakuwepo wakati wa ufungishaji wa ndoa, kwa Mkristo kwenda kufunga ndoa ya pili, Mtu asiye sahihi
kufungisha ndoa(Mfungishaji lazima awe na leseni), Ndoa ikifungwa katika kipindi cha Eda, na pia lazima ndoa iwe na
mashahidi.
Aidha Mwanasheria aliendelea kuweka wazi juu ya wakati gani ndoa inakuwa batilifu(halali ila inakasoro). Wakati mmoja wa
Wanandoa kukosa uwezo wa kutimiza tendo la ndoa, katika kipindi cha Uchumba hukugundua kuwa mwenza wako ni mgonjwa wa
akili, ukigundua kuwa mwenza wako anaugonjwa wa zinaa, kama mmoja wa wanandoa hajafikisha miaka 18 hasa mwanamke,
mmoja wa wanandoa anagoma kutimiza tendo la ndoa.
Aidha alimaliza kwa kusistiza kuwa mwanamke anayohaki ya kumiliki mali binafsi, na Talaka ni halali kama ndoa
hairekebishiki na Jukumu la kutunza familia ni la Baba.
Mbali na wataalam mbalimbali kuwasilisha Mada zao pia Mh.Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Chunya Ndg. Osmund Ngatunga
alipata fursa ya kuhutubia na kugusia mambo mbalimbali ikiwemo Tehama na umuhimu wake, Jukumu la utoaji Haki, Faida ya matumizi
ya TEHAMA kama njia ya kuimarisha ubora wa utoaji haki, Changamoto, Mikakati na Mipango ya baadaye ya mahakama.
Mh. Hakimu mfawidhi alianza kwa kuitambulisha kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ambayo ni:-
“Matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki kwa wakati na kwa kuzingatia Maadili”
Alizidi kueleza kuwa, Kwa maneno mengine kauli mbiu ina lengo la kutuonyesha matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma za jamii, hasa utoaji haki
na kuimarisha uwazi na maadili.
TEHAMA ni nini? Ni Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kihistoria, dhana hii imegawanyika katika makundi mawili ambayo
ni analogia na digitali.
Analogia ni upashanaji habari isiyotumia vifaa vya kielekitroniki kama typewriter, posta, mkono kwa mkono, matumizi ya
karatasi, mafaili ya kawaida n. k.
Digitali ni upashanaji wa habari kwa kutumia vifaa vya mawasiliano, na mifumo mtandao au program, (kielekitroniki) ili
kugawana habari kupitia tovuti (www.judiciary.go.tz), barua pepe (info@judiciary.go.tz), faksi, video confencing, simu
(smart phones), scanner, mitandao ya kijamii kama facebook, whatsapp, twiter, instagram, blogs, you tube n.k.
Mahakama Maboresho kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mkataba wa Huduma kwa Mteja 2002 na Mpango Mkakati wa Mahakama
2015-2020 inakusudia pamoja na mambo mengine kutumia TEHAMA katika kuboresha misingi ya utawala bora, amani na utulivu,
uthabiti na umoja wa kitaifa ili kuchochea maendeleo ili kufikia lengo lake la kuwa na Mahakama iliyokaribu na inayofikiwa
na wananchi katika kutoa huduma za utoaji haki Nchini.
2.Jukumu la Utoaji Haki.
Kama vilivyo vyombo vingine vya dola ambavyo vimekasimiwa mamlaka ya Kikatiba ya utendaji (Utawala), uwakilishi, kutunga
sheria na kuisimamia Serikali (Bunge) Mahakama imepewa jukumu la Kikatiba na kisheria la utoaji haki. Ina mamlaka yenye
“kauli ya mwisho” ya utoaji haki kwa wananchi kwa mujibu wa Ibara ya 4, 107A, 107B ya Katiba yetu.
Kwa mujibu wa Ibara ya 107B ya Katiba ya Nchi, Mahakama inapaswa ilinde uhuru, haki, hadhi na mamlaka ya Kikatiba dhidi ya
mihimili mingine ya dola na wananchi. Dhana ya uhuru wa Mahakama imejikita hasa katika mambo ya ki-utawala, fedha na
utendaji wake hasa wakati shauri linaposikilizwa na kuamuliwa bila kuathili ibara ya 8 na 146 ya Katiba ya Nchi.
TEHAMA ina lengo, pamoja na mambo mengine, kuharakisha upatikanaji wa huduma mbalimbali zitolewazo na Mahakama ili
kukidhi Dira yake isemayo “Haki sawa kwa wote na kwa wakati”. Mbali na kutumia TEHAMA pia tumekusudia kutumia Mahakama
itakayotembea yaani kuna gari maalum litakalotumika kufika sehemu mbalimbali ndani ya Wilaya yetu ili kwenda kusikiliza
mashauri na kutoa elimu. Mahakimu, watunza kumbukumbu na Katibu Muhtasi watakao tekeleza jukumu hili katika eneo letu
wameshateuliwa.
TEHAMA itafanikisha kurekodi ushahidi, umalizikaji mashauri haraka, mazingira mazuri ya utendaji kazi, kupata huduma za
mahakama bila urasimu, kupata nakala za mwenendo na uamuzi wa Mahakama kwa wakati.
Ni imani ya Mahakama kwamba endapo TEHAMA itatumika kama ilivyokusudiwa itasaidia kuondoa misemo ya wanazuoni isemayo
“haki siyo tu itendeke bali ionekane imetendeka”, pia “haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa” lakini vilevile “haki
iliyoburuzwa ni haki iliyozikwa”.
kwa hotuba kamili ya Mh. Hakimu Mfawidhi bonyeza hapa. HOTUBA YA HAKIMU MKAZI MFAWIDHI -2018.pdf
Akiongea na hadhira ya wananchi walihudhuria maadhimisho ya siku hiyo ya sheria Mkurugenzi Mtendaji wa H/W Chunya Bi.
Sophia kumbuli alianza kwa kuwapongeza wananchi walijitokeza kwa wingi kuhudhuria Hafla hiyo na kusistiza kuwa ule
utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi kila siku za Alhamisi utaendelea na kuwasihi wananchi kuja kupewa ushauri wa
kisheria hasa kuhusu ardhi.
Pia Katibu tawala wa wilaya Bi. Mahija Nyembo aliwashukuru wananchi kwa kufika kwa wingi na kwamba kero zao zote
wanazoziwasilisha na watakazo ziwasilisha zitafanyiwa kazi, pia hakusita kuwasisitiza wapite kwanza kwenye ngazi za chini
za maamuzi kama kata, tarafa kabla ya kufika kwenye ngazi ya wilaya na kwamba kero zao ziwe za kweli.
Naye Mgeni rasmi katika Hafla hiyo ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Chunya Bi. Rehema Madusa alianza kwa kuwapongeza
wananchi wote kwa kuuona Mwaka Mpya, na kumshukuru Mungu kuweza kuwalinda wote. na kueleza kuwa wananchi wengi
wanachangamoto ya kisheria na kwamba Mabaraza ya Kata bado hayajaweza kuwafikia wananchi Wengi kwa sababu mbalimbali,
aliipongeza serikali kwa kusimamia uendeshaji wa kesi kwa haraka na wakati, akiwasihi wananchi kutowaogopa mahakimu na
wanasheria, na aliwaeleza wananchi waende ili kupewa msaada wa kisheria. Mh.Mkuu wa wilaya alisisitiza kuwa masuala ya
Mimba kwa wanafunzi si ya kujadili nje ya mahakama na kwamba mashauri hayo yapelekwe mahakamani na sheria ichukue mkondo
wake kwa wahusika, na kurudia kusisitiza tamko la Raisi kuwa binti atakayepewa ujauzito hastahili kurudi shuleni hivyo anapaswa kulindwa.
Alitumia Fursa hiyo kuwakaribisha Mawakili wa kujitegema, Maafisa Takukuru na vyombo vinginevyo kuja kuungana naye kila siku ya
Alhamisi ili kusikiliza kero za Wananchi.
aliendelea kuwasihi viongozi wa Dini juu ya kuwakumbusha Wananchi masuala mbalimbali ya kiusalama, na kusema mambo mengi
yanaanzia chini kwa Wananchi, hivyo Elimu jamii itolewe kwa Wananchi, na kusisitiza ni lazima kurekebisha vyombo
vinavyosimamia haki za Wananchi,
akiongelea suala la maadili aliwasisitiza wananchi kutotekwa na tabia za umagharibi na kwamba watanzania tunapaswa
kuheshimu maadili yetu.
Pia hakusita kuwasisitiza Wananchi juu ya kujenga nyumba bora ikiwemo na zile za wageni yaani Guest Houses kwani Wilaya ya
Chunya inatarajia kuja kuwa na wageni wengi hapo baadaye ikiwemo wawekezaji. Kwa kumalizia aliwaasa wananchi kuzingatia
masuala ya ulinzi na Usalama, na uhifadhi wa mazingira. Pia hakusita kumshukuru Hakimu mfawidhi wa Wilaya na kumsihi
wajipange katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la mahakama.
katika Hafla hiyo wananchi wengi walipata fursa ya kuuliza maswali mengi yanayohusiana na sheria na kupatiwa majibu kutoka kwa
Wataalam Mbalimbali wa Sheria waliokuwepo.
MGENI RASMI MKUU WA WILAYA YA CHUNYA AKIWA NA VIONGOZI WA DINI, HAKIMU MFAWIDHI, KATIBU TAWALA NA MWANASHERIA WA H/W.
HAKIMU MFAWIDHI AKIWA NA WADAU MBALIMBALI WA SHERIA
HAKIMU MFAWIDHI AKIWA NA WAWAKILISHI WA CHAMA TAWALA
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.