Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika kata ya Lualaje iliyopo wilayani Chunya baada ya kutoa fedha shilingi Milioni Mia moja kujenga Nyumba ya walimu (2 in 1) kwaajili ya walimu wanaofundisha Shule ya Sekondari Lualaje ambayo imefunguliwa Rasmi mwaka huu ambapo mpaka sasa ina wanafunzi 86 wa kidato cha kwanza na walimu 13 na imegharimu zaidi ya shilingi milioni 480 kukamilika kwake.
Shule hiyo iliyojengwa kwa zaidi ya Shilingi Milioni mia nne na themanini (Milioni mia nne na sabini zimetoka serikali kuu na milioni kumi na moja kutoka Halmashauri ya wilaya ya Chunya) imehusisha ujenzi wa vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, maabara za Kemia, Baolojia, na Fizikia pamoja na matundu ishirini ya vyoo, mpaka sasa kuna vyumba sita vya madarasa vinasubiri wanafunzi wa kidato cha kwanza 2024 watakaopangwa katika Shule hiyo.
Diwani wa kata ya Lualaje Mhe. Tusalimu Mwaijande kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowajali wananchi wa kata ya Lualaje kwa kukubali kutoa milioni mia nne na sabini (470) ili kukamilisha miundombinu ya shule hiyo na ameshukuru baraza la Madiwani kukubali shule hiyo ijengwa Lualaje na hata Ofisi ya Mkurugenzi kuongezea fedha eneo ambalo mradi ulikwama lakini kuhakikisha shule inapata walimu wa kutosha.
“Kwanza wananchi wa kata ya Lualaje wanaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita maana ndani ya uongozi wake Barabara ya Lualaje sasa inapitika mwaka mzima tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzo, tumepata shule bora kabisa ya Sekondari kupata kutokea wilayani Chunya na tuna vyumba vinavyosubiri wanafunzi, lakini bado ametupatia milioni mia moja kujenga Nyumba (2 in 1) kwaajili ya walimu, wananchi wa Lualaje Hatuna cha kumlipa zaidi ya kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kwa kufanya kazi kwa bidii na kusimamia fedha zote zinazoletwa kwenye kata yetu”.
Aidha Mhe Mwaijande amesema tayari wameanza kuzungumza na wadau wengine ili kuanza kujenga Nyumba nyingine ya walimu (2 in 1) ili kuondokana na kero ya makazi kwa watumishi wanaoishi na kufanya kazi kwenye kata hiyo kwani wameshapata zaidi ya milioni sita kutoka kwa wadau tayari kuanza ujenzi wa nyumba hiyo.
“Mwaka huu tumekusudia kujenga nyumba mbili zenye uwezo wa kuhifadhi familia nne tayari hii ya kwanza inakamilika Oktoba 30, lengo letu kila mwaka kujenga nyumba moja yenye uwezo wa kuhifadhi watumishi wawili mpaka tutakapoimaliza kabisa kero ya makazi kwa watumishi walipo katika kata yetu, lakini tunaendelea kuishukuru serikali maana mpaka sasa Lualaje ni ya Kijana, barabara zinapitika, huduma za afya zipo na sasa Sekondari imejengwa watumishi wameanza kuomba kuhamia Lualaje” alisema Mhe Mwaijande.
Kata ya Lualaje ni moja ya kata zilizoko pembezoni mwa wilaya ya Chunya ambapo ni zaidi ya Kilometa 40 kutoka Lupa Tingatinga na kilometa 128 kutoka Mkao makuu ya wilaya hivyo uwepo wa Shule hiyo ya sekondari umesaidia kupunguza umbali kwa wanfunzi kwenda kupata elimu lakini pia uhakika wa kupata elimu umeongezeka maana wanafunzi watapata usimamizi mzuri kutoka kwa wazazi wao na walimu kwa kushirikiana tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzo.
Shule ya sekondari Lualaje imekusudiwa kupokea wanafunzi kutoka shule ya Msingi Mwiji. Lualaje na Shule ya Msingi Mpembe ambapo kwa mwaka 2024 inataraji kupokea wanafunzi mia moja na ishirini (120).
Nyumba ya walimu (2 in 1) inayojengwa kata ya Lualaje kwaajili ya walimu wa shule ya sekondari Lualaje
Upande wa nyuma wa Nyumba ya walimu (2 in 1) inayojengwa kwaajili ya walimu wa shule ya sekondari Lualaje iliyopoa kata ya Lualaje
Shule ya Sekondari Lualaje ikionesha miundombinu yote ya shule isipokuwa Nyumba ya Mwali inayojengwa kwaajili ya walimu wanaofundisha katika shule hiyo
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.