Mwenyekiti wa wadau wa Tumbaku ambaye pia ni Afisa kilimo wa Wilaya ya Chunya ndugu Cuthberth Mwinuka amewataka wakulima wa zao la Tumbaku kulima zao hilo kwa kufuata taratibu, miongozo na kanuni za zao hilo ili kupata zao bora kwani kwa kuto kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa ni kinyume cha Sheria .
Ameyasema hayo mapema tarehe 10/03/2025 wakati wa kikao cha mrejesho wa tathimini ya zao la tumbaku kwa msimu wa kilimo wa 2024/2025 kilichoketi katika ukumbi wa mikutano wa kampuni ya Mkwawa kwa lengo la kuhitimisha zoezi la tathimini ya zao lililodumu Zaidi ya siku 18.
“Nimeshawaelekea kwamba kilimo cha Tumbaku kipo kwa mujibu wa sheria za bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kina miongozo pamoja na adhabu kwa mtu anaye kiuka miongozo hiyo ikiwa ni pamoja na faini, au kifungo au vyote kwa pamoja, hivyo kwa wale wote wanaoacha mabua wakayatoe, maotea nayo wakayatoe kwasababu yanaathiri uzito wa tumbaku na wale wanaoacha mbegu ni kinyume cha sheria kwasababu kila mwaka mkulima anatakiwa kupanda mbegu mpya zinazotolewa na makampuni ili kupata zao bora”amesema Mwinuka
Aidha Mwinuka amesisitiza kwa viongozi wa vyama vya ushirika waliohudhuria kikao hicho kuhakikisha wanakwenda kuwaeleza wakulima yale yote yaliyoelezwa katika kikao hicho lakini pia kwenda kuyafanyia kazi ili yaweze kuleta tija katika kupunguza changamoto mbalimbali zilizojitokeza lakini pia kuleta tija katika zao hilo la kibiashara.
Naye Mkurugenzi wa zao la Tumbaku bodi ya Tumbaku Tanzania ndugu Nicholaus Mauya ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya ushirika kuwasimamia wakulima kuhakikisha wanalinda na kulithamini kila jani katika mmea ili kuongeza tija ya zao la tumbaku na kumwezesha mkulima kupata kipato ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza wakulima kuvuna kuanzia jani la chini hadi jani la juu kwasababu kila jani la zao hilo ni pesa.
“Sisi kama viongozi lazima tuoneshe mfano wa kuvuna majani ya chini lakini pia viongozi na maafisa ugani mkawasaidie wakulima kuhakikisha wanazingatia kanuni bora za kilimo cha tumbaku ili kuhakikisha tunaboresha kilimo cha tumbaku na kuongeza tija ili kuendana na hali halisi.”amesema Mauya
Meneja mkuu CHUTCU ndugu Juma Nshinshi amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia vyama vyao kama ambavyo wameaminiwa na wanachama ikiwa ni pamoja na umakini katika kusimamia mali ya chama lakini pia viongozi wahakikishe mnawasisitiza wakulima kufunga tumbaku mapema ili masoko yaweze kufanyika mapema.
Boniface Richard kutoka Global Leaf Tanzania Limited, Godfrey Gobbo kutoka kampuni ya Mkwawa wakiwakilisha kampuni zingine za Tumbaku wametoa msisitizo mkubwa kwa viongozi wa vyama vya ushirika kuwa na makadirio yanayoendana na uhalisia lakini pia kuendelea kuwaelimisha wakulima wao juu ya changamoto zilizojitokeza wakati wa tathimini ili kuondkana na kasi ya upotevu wa jani na kuongeza pato la mkulima kwani kila jani katika mche lina thamani yake.
Kikao cha mrejesho wa tathimini ya zao kimetokana na tathimini iliyofanyika kwa majuma mawili kwa wilaya ya Chunya na Wilaya ya Songwe na kuhusisha wadau mbalimbali wa tumbaku ikiwa ni pamoja na Makampuni ya tumbaku, Bodi ya Tumbaku Tanzania, wataalamu kutoka Halmashauri , chama kikuu cha ushirika na wadau wa taasisi za fedha na kujadili mambo mbalimbali yalioonekana wakati wa tathimini ya zao ili kuboresha uzalishaji wa zao hilo na kuongeza tija ya zao hilo
Mwenyekiti wa wadadu wa Tumbaku ndugu Cuthberth Mwinuka akizungumza na wadau kujadili mambo mbalimbali yaliyoonekana wakati wa tathimini ya zao wakati wa kikao cha mrejesho wa tahimini ya zao kwa mwaka 2024/2025 ili kuendelea kuboresha na kuongeza tija ya zao.
Mkurugenzi wa zao la tumbaku ndugu Nicholaus Mauya akitoa rai kwa viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima wa tumbaku juu ya uchumaji wa kila jani katika mche ili kuongeza kipato cha mkulima.
Viongozi wa vyama vya ushirika na wadau wa Tumbaku wakifuatilia na kutoa mikakati yao katika kikao cha mrejesho wa tathimini ya zao kwa mwaka 2024/2025 kilicichoketi katika ukumbi wa Mikutano wa kampuni ya Mkwawa
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.