WAJUMBE wa Kamati ya Chama Cha Mapinduzi {CCM} Mkoani Mbeya na Wilaya ya Chunya wamefanya ziara ya siku mbili kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilayani Chunya.
Kamati imetembelea miradi ya Idara ya Afya, Idara ya Elimu sekondari, Mradi wa Barabara chini ya TARURA na Mradi wa Maji unaotekelezwa na RUWASA.
Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani hapa, Mhe. Mohamed Mashango ameonesha kuridhika na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
Akizungumza katika ziara hiyo Mhe. Mashango amesema, ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hasa miradi ya Afya ambapo Halmashauri inatekeleza ujenzi wa kituo cha Afya Kambikatoto, Mafyeko pamoja na ujenzi wa wodi ya wanawake na wanaume, ujenzi wa Bohari ya Dawa na Jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya.
“Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya niwape hongera na kuwapongeza kwa muda mliopewa na hatua nzuri iliyofikia, na kama mlivyotoa ahadi ndani ya mwezi mtakuwa mmekamilisha basi hakikisheni mnakamilisha kama mlivyoahidi." Alisema Mashango.
“Tumeona kule kwenye ujenzi wa kituo cha afya majengo yamefika kwenye asilimia kubwa zaidi na kwa kasi ya ujenzi huu wa nyumba ya madaktari tumeridhika nayo." Aliongeza Mhe. Mashango.
Aidha, Mhe. Mashango alieleza matarajio yake katika ujenzi wa miradi hiyo,na kuwahimiza wajenzi kukamilisha kazi haraka iwezekanavyo ili wananchi waanze kupata huduma.
"Kwa hiyo matarajio yetu ni kwamba katika kipindi hicho ambacho mmeahidi, tukija kwa mara nyingine tutakuta matarajio makubwa zaidi, kwamba tutakuta angalau watu wameshaanza kupata huduma na huku tukute Madaktari wamekaa itakuwa nzuri zaidi ili kuwapunguzia watu adha wanayoipata." Alisema Mhe. Mashango.
Kwenye kituo cha Afya Kambikatoto kamati imeushauri uongozi wa Halmashauri kuchukua hatua za haraka za kuchimba kisima ili kuhaikisha kituo kinakuwa na maji pindi mchakato wa kupata maji ukiendelea.
“Ni vizuri pakawa na mpango wa kuchimba kisima kama ambavyo mmesema, maeneo haya maji ukiyatafiti yanapatikana, tumejifunza pale kijijini watu wamechimba visima wamepata maji, vizuri pakawa na kisima hata kimoja ili kusaidia kutoa huduma hapa.” Alisema Ndg Charles J Seleman Katibu wa CCM Wilaya ya Chunya.
Kwa upande wa mradi wa Eimu Sekondari kamati haikuridhika na kasi ya utekelezwaji wa mradi huo unaojengwa kwa nguvu za wananchi kwani unakwenda taratibu na umechukua miaka mingi bila ya kukamilika.
Kamati imeutaka uongozi wa Kata ya Mafyeko kwa kushirikiana na Halmashauri kuchukua jitihata za haraka kuhakikisha ujenzi wa sekondari ya Mafyeko unakamilika ili mwakani isajiliwe na watoto waanze kusoma, ili kuwapunguzia watoto adha ya kutembea umbali mrefu pindi wanapokwenda shuleni.
Kamati ya Siasa Mkoa kweye ziara hii waliambatana na Wataalamu wa Sekretarieti ya Mkoa, Wataalam wa Wakala wa Serikali TARURA, RUWASA pamoja na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Chunya, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chunya, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Mh. Mayeka Simon Mayeka wakwanza kushoto akiwa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya Mhe. Mohamed Mashango wa Katikati pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Chunya Ndg Charles Seleman wakati wa Ziara ya Kamati ya siasa Mkoa na Wilaya kukagua utekelezaji wa Miradi ya maendeleo wilaya ya Chunya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndg Tamim Kambona wa kwanza kulia akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mbeya Mh. Mohamed Mashango wakati wa ziara ya kamati ya Siasa Mkoa na wilaya walipotembelea wilaya ya chunya kukagua Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa na Wilaya wakikagua Ujenzi wa Sekondari ya Mafyeko wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilayani Chunya.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na Wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wa Vijana UVCCM mkoa wa Mbeya Mh. Mohamed Mashango wakikagua ujenzi wa wodi ya Wanawake na wanaume katika hospitali ya wilaya.
Kamati ya Siasa Mkoa na Wilaya wakikagua Ujenzi wa Kituo cha Afya Mafyeko wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilaya Chunya.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.