Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mayeka S. Mayeka akimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Mbeya amewataka Maafisa maendeleo ya jamii halmashauri zote za mkoa wa Mbeya pamoja na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawalinda watoto kwa kuwazuia kutumia vitu vya kielekitroniki bila usimamizi wa walezi au wazazi jambo ambalo litapelekea kuwalinda watoto hao na ukatili mbalimbali unaojitokeza katika jamii ya sasa.
Mhe. Mayeka amesema hayo leo tarehe 16/6/2023 alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo imeadhimishwa kimkoa wilayani Chunya katika viwanja vya shule ya Msingi Makongolosi iliyopo kata ya Bwawani Mamlaka ya Mji mdogo Makongolosi
“Nawaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri zote kuhakikisha wanatoa Elimu kwa wazazi na walezi ili watambue haki za mtoto ili kumpatia malezi yanayofaa. Na wazazi hakikisheni mnawazuia watoto kutumia vitu vya kielekitroniki kama vile simu, televisheni, intaneti na nyinginezo bila usimamizi wa wazazi au walezi amesema Mhe. Mayeka
Aidha Mhe. Mayeka amesema ukatili wa kijinsia bado ni tatizo katia mkoa wa Mbeya huku ubakaji ukiongoza kuwa na kesi nyingi hivyo amewataka wananchi wote kujitokeza kutoa taarifa mbalimbali za ukatili pamoja na kutoa ushahidi mahakamani pindi watuhumiwa wa unyanayasaji wa kijinsia wanapokuwa wamekamatwa ili kuhakikisha sheria inawatia hatia na kupewa adhabu stahiki
Ushahidi imekuwa changamoto kubwa sana mahakamani kwani sisi wananchi huwa hatujitokezi kutoa ushahidi pale tunapotakiwa kufanya hivyo, Niwaombe mjitokeze kutoa ushahidi pale mtapotakiwa kufanya hivyo kwani nje ya hapo maana yake mahakama inawaacha huru watuhumiwa wa ukatili wa kijinsia kwakukosa ushahidi
Awali akimkaribisha Mkuu wa wilaya ya Chunya, Katibu tawala wa wilaya ya hiyo Ndugu Anakleth Michombero amewataka wananchi waliojitokeza katika madhimisho hayo kuhakikisha wanawalea watoto wao ili watakapofika umri wa utu uzima waoneshe nidhamu na mwenendo mwema kama walivyolelewa
“Mlee mtoto katika njia impasayo, hataiacha hata akiwa mzee, hivyo kujua kama mtoto alilelewa vizuri au vibaya akiwa mtoto ni katika utu uzima wake ndipo itajulikana, Hivyo naomba tuwalee watoto katika maadili mema wawapo wadogo ili watakapokuwa wenye umri wa utu uzima waoneshe maadili mema waliyolelewa walipokuwa wadogo
Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Chunya Ndugu Vincent Msolla kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wilaya ya Chunya amesema kama halmashauri wataendelea kuhakikisha mtoto yuko salama na anapata mahitaji yote muhimu katika maisha yake, Lakini pia amewataka wananchi wilaya ya chunya kuendelea kulipia kodi ili serikali ikusanye mapato ambayo baadaye yanarudi kujenga miradi mbalimbali kama ambavyo shule mpya ya msingi inayojengwa katika kata ya Makongolosi
“Tuna kazi ya kuhakikisha mtoto yuko salama na anapata mahitaji yote muhimu katiia maisha yake ya kawaida na hatimaye kutimiza ndoto za maisha yake. Lakini pia wananchi naomba tuendelee kutoa kodi kwa mujibu wa sheria ili tuendelee kuongoza katika ukusanyaji wa Mapato, kujitoa kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo ili tuendelee kuungana na serikali yetu kutuletea maendeleo kama ambayo serikali imeona vema kutujengea shule mpya ya msingi katika kata ya Makongolosi”
Meneja wa Kanda Mkwawa Leaf Tobacco L.T.D ndugu Chrispine Mchafu amesema kampuni ya Mkwawa inaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita Inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kupambana na ukatili kwa watoto ambapo mwezi wa saba kampuni itaanzisha kampeni maalumu ya kupinga utumishwaji wa wototo kwenye mashamba ya Tumbaku maana kuna ukatili mkubwa katika shughuli hizo
Sisi Kampuni ya Mkwawa Leaf Tobacco tuko bega kwa began a serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanzia mwezi wa saba tunataraji kuanzisha Kampeni Maalumu ya kupinga utumikishwaji wa watoto kwenye mashamba ya Tumbaku tunayoyasimamia kwani katika uzalishaji wa Tumbaku kuna unyanyasaji mkubwa wa watoto hususani katika mchakato wa kukausha zao la Tumbaku amesema Mchafu
Naye Meneja miradi wa Child Support Mbeya Hildergade Megrab ametoa ombi maalumu kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuboresha mazingira ya shule ya msingi Makongolosi ili iwape nafasi watoto wenye mahitaji maalumu kupata huduma kwa urahisi kuliko ilivyo sasa kwani watoto wenye uhitaji maalumu wapo zaidi ya 25 katika shule hiyo lakina miundombinu sio rafiki kwao
Naomba kuleta ombi binafsi kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba irekebishe miundombinu ya Shule ya Msingi Makongolosi ili kuwapa nafasi watoto wenye mahitaji maalumu maana mpaka sasa kuna watoto zaidi ya 25 wenye mahitaji maalumu lakini miundombinu sio rafiki sana kwao
Sauda Mwendo na Angel Juma wanafunzi kutoka shule ya sekondari Makongolosi wamewawakilisha watoto wenzao wa Mkoa wa Mbyea kusoma Risala kwa Mgeni Rasmi ambapo wamesema Ndoa za utotoni, ubakaji,kubakwa, kufichwa kwa watoto wenye ulemavu na mengine mengi bado yanawakabili watoto wa Mbeya huku wakisema wanafamilia kukaa na kumalizana na ndugu wanaobainika kufanya vitendo hivyo kunapelekea watoto kuendelea kutokuwa salama katika maisha yao ya kila siku
Ndoa za utotoni, ubakaji na ulawiti, kufichwa kwa watoto wenye ulemavu pamoja na mambo mengine bado yanaendelea kututesa watoto na ndugu wanapokaa na kumalizana na ndugu waliobainika kufanya vitendo vya kikatili kwa watoto bado vinaendelea kufanya watoto kutokuwa salama, Hivyo tunaomba kila mtu atekeleze jukumu lake ili sisi watoto tuweze kuwa slama.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.