Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mayeka S Mayeka amewataka wananchi wa wilaya ya Chunya kutunza vitambulisho vya Taifa walivyovipata kwani vina umuhimu mkubwa kwao ikiwa ni pamoja na utambulisho wa Utaifa wao
Ametoa Kauli hiyo Mapema leo tarehe 8/12/2023 katika viwanja vya stendi ya Mabasi Chunya wakati akizindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya Taifa ambapo wilaya ya Chunya imepata zaidi ya vitambulisho elfu sabini na saba
“Wanachunya naomba tuvitunze vizuri vitambulisho hivi kwani ni utambulisho wa uraia wako lakini pia hutumika maeneo mbalimbali ili kukutambua na kukupatia huduma, lakini pia vitambulisho hivyo msipovitunza vikaangukia kwenye mikono ya watu wabaya basi vinaweza kutumika kukutia hatiani au kukuhusisha na matukio mabaya”
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa wilaya ya Chunya katika Hafla hiyo, Afisa usajili wilaya ya Chunya Bi Emma Ndunguru ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha wananchi wa Chunya wanapata vitambulisho vya Taifa na kwa awamu hii wilaya hiyo imepata vitambulisho Elfu sabini na saba na mia mbili arobaini na tatu (77,243)
“Tunaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha wananchi wa wilaya ya Chunya wanapata vitambulisho kwani mpaka sasa Chunya tumepokea vitambulisho 92315 ambapo awamu ya kwanza tulipokea vitambulisho 15072 na awamu hii tumepokea vitambulisho 77,243” alisema Bi Emma
Akitoa salamu za wananchi wa kijiji cha Kibaoni mbele ya Mkuu wa wilaya ya Chunya Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana Joshua Mlambalala amemshukuru mkuu wa wilaya ya Chunya kuiteua kata ya Chokaa na hasa kijiji cha Kibaoni ili kuwakilisha vijiji vingine vya wilaya ya Chunya katika uzinduzi wa Zoezi hilo la ugawaji wa vitambulisho vya Taifa
“Nakushukuru sana Mhe Mkuu wa wilaya ya Chunya kwa kutupatia nafasi hii ya kuwakilisha maeneo mengine ya wilaya ya Chunya kuzindua zoezi hili muhimu la ugawaji wa vitambulisho vya Taifa, tunatambua yapo maeneo mengi katika wilaya hii lakini ukasema zoezi hili lifanyike kijiji cha Kibaoni, Sisi wana kibaoni tunakushukuru”
Zoezi la uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho vya Taifa limefanyika kata ya Chokaa kwenye kijiji cha Kibaoni eneo la stendi ya mabasi ambapo Mkuu wa wilaya ya Chunya amezindua zoezi hilo kwa kugawa vitambulisho kumi kwa wananchi, na zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo litaendelea kwenye ofisi za vijiji na kata ambapo wananchi wanapaswa kufika ofisi za kata kuona majina yao na hatimaye kuchukua vitambulisho hivyo, Kumbuka kitambulisho hicho ni haki yako na ni bure kabisaa
Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mayeka S Mayeka akizungumza na wananchi waliojitokeza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho vya Taifa Mapema leo katika viwanja wa Stendi ya Mabasi Chunya
Katibu tawala wilaya ya Chunya Bw Anakleth Michombero akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa wilaya ya Chunya wakati wa Hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho mapema leo
Mkuu wa wilaya ya Chunya (Aliyeavaa suti) akikata utepe ili kuzindua zoezi la ugawaji wa Vitambulisho, mwenye tisheri ya Blue bahari ni mtendaji wa kata ya Chokaa na mwenye tisherti nyekundu ni mwenyekiti wa kijiji cha Kibaoni
Mkuu wa wilaya ya Chunya akikabidhi kitambulisho cha Taifa kuashiria uzinduzi rasmi wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo wilayani Chunya
Afisa msajiliwa NIDA wilaya ya Chunya Bi Emma Ndunguru akisoma taarifa mbela ya Mkuu wa wilaya ya Chunya wakati wa uzinduzi wa zoezi la Ugawaji wa vitambulisho vya Taifa mapema leo
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.