Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe. Mayeka S. Mayeka amewataka walimu wanafunzi na jamii kwa ujumla kulinda miundombinu ya shule iliyoko katika Maeneo yao ikiwa ni pamoja na madawati ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na ameuagiza uongozi wa shule kwa ujumla kuwachukulia hatua wazazi ambao hawatimizi mahitaji ya watoto wao (wanafunzi)
Mhe. Mayeka ametoa kauli hiyo jana katika Shule ya Msingi Mapongolo iliyopo kata ya Chokaa wilayani Chunya wakati akipokea Madawati Hamsini (50) yenye thamani ya Milioni tatu (3,000,000/=) kutoka Bank ya CRDB tawi la Chunya ikiwa ni sehemu ya Banki hiyo kurudisha Faida kwa wataje wake na kuungana na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha Mwananchi wake wanapata huduma bora.
“Nikupongeze meneja wa banki ya CRDB kwa Madawati haya, Sio kidogo kama mwingine anaweza kufikiria, Ni mengi sana kwani yanatusaidia kupunguza uhitaji na hata yangekuwa madawti matano bado ningefika kuyapokea. Mkoa wa Mbeya tumekubaliana hakuna mwanafunzi yeyote anakaa chini hivyo ninyi mnatusaidia Chunya kutekeleza Mpango wetu”
Meneja wa banki ya CRDB tawi la Chunya Bw. Hamis Mbinga amesema wao Kama Banki wataendelea kuungana na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali kama walivyofanya maeneo mbalimbali yakiwepo Elimu, hivyo kutoa madawati hayo hamsini (50) ni mwendelezo wa kile ambacho wamekuwa wakikifanya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Chunya
“Tumekuwa na utaratibu wa kufanya mambo tofauti tofauti kama elimu, afya na mengine ili na sisi tutoe mchango kwa jamii. Tumekuwa tunashirikiana na Mkurugenzi na Ofisi yako Mhe Mkuu wa wilaya, na katika sekta hii ya Elimu tumetoa madawati kiwanja sekondari, tumeshiriki kutengeneza maabara Kiwanja sekondari na pia kata karibu zote za tarafa ya Kiwanja tumezifika kwa kutoa madawati 240 hivi, na hili linaloendelea hapa ni mwendelezo katika kuhakikisha tunailetea maendeleo wilaya yetu” Meneja CRDB
Naye Diwani wa kata ya Chokaa Mhe. Samwel Komba kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo ameishukuru benki ya CRDB kwa namna ambavyo wameweza kutoa msaada huo wa madawati katika Shule ya Msingi Mapongolo huku akiomba kutokuwachoka pale watakapopeleka maombi mengine kwaajili ya miradi mingine ya Maendeleo
“Nikupongeze sana Meneja na endelea kupambana na sisi kama wawakilishi tuko tayari kufanya kazi na CRDB, tutakuja tena ofini kwenu hata kama sio kwa madawati kwa njia nyingine tutawafikia CRDB msituchoke, kwa niaba ya wananchi wa kata ya Mapogolo tunashukuru sana” Mhe. Diwani
Katibu wa Chama cha Mapinduzi tawi la Mapogolo Ndugu Jumanne Rashid Mariatabu akitoa salamu za Chama hicho amesema Ilani ya chama cha Mapinduzi inasimamiwa vizuri na inatekelezwa ipasavyo na viongozi kuanzia ngazi ya Wilaya hadi tawi hivyo naye ametoa shukrani kwa Meneja wa banki ya CRDB kwa namna ambavyo wamekuwa mstari wa Mbeya kuhakikisha wananchi wanapata elimu kwa uzuri kwani Madawati hayo yatasadia wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapongolo kusoma kwenye mazingira rafiki.
Awali akitoa taarifa mbele ya Mkuu wa wilaya, Makamu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Frank Sanga amesema Shule ilikuwa na upungufu wa madawati 257, hivyo ongezeko hilo litasaidi kwa kiwango kikubwa kuondoa tatizo la uhaba wa madawati katika shule hiyo, huku akisema madawti hayo yatasaidia wanafunzi kusoma kwa utulivu, kuwa na mwandiko mzuri na kuleta hamasa katika kusoma.
Pamoja na kupokea Madawati hayo Mkuu wa wilaya ya Chunya amekagua ujenzi wa Madarasa mawili yanayojengwa kupitia mradi wa Boost katika Shule ya msingi Mapogolo, huku Mhandisi wa Halmashauri Eng Charles Kwai anayesimamia ujenzi wa mradi huo amesema mwezi juni, 2023 ujenzi wa madarasa hayo utakuwa umekamilika na kuanza kutumiwa na wanafunzi.
Picha Mbalimbali katika tukio la Makabidhiano
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.