Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe. Mayeka S.Mayeka ameutaka uongozi wa shule ya msingi Nyerere ambao ndio wasimamizi wa ujenzi wa shule mpya Mzalendo kuhakikisha mambo madogo madogo yaliyosalia katika ujenzi wa shule ya awali na Msingi Mzalendo yanakamilika kwa wakati ili shule ianze mapema kama matarajio ya serikali.
Maagizo hayo ameyatoa tarehe 9/10/2023 wakati alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi na awali ya Mzalendo iliyojengwa katika kitongoji cha Ntankini kata ya Makongolosi ambapo ujenzi wa Shule hiyo umekamilika yamesalia mambo madogo madogo ya kukamilisha.
“Hakikisheni mnarekebisha sehemu zote ambozo nimewataka kurekebisha yakiwemo madawati , madirisha ya vyoo pamoja na kusawazisha maeneo yote yanayoizunguka shule kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua tafuteni hata wadau watakaoweza kuwasaidia greda kwaajili ya kusawazisha maeneo mbalimbali yanayozunguka shule “ alisema Mhe. Mayeka.
Aidha Mhe. Mayeka ameutaka Uongozi wa shule kuacha kuwalipa Mafundi pesa yote kabla kazi haijakamilika kwani kwa kufanya hivyo inasabaisha baadhi ya mafundi kuto kufanya kazi zao kwa ubora na ufanisi lakini pia ameagiza Mafundi ambao bado hawajakamilisha kazi zao wahakikishe wanazikamilisha kama ilivyokusudiwa.
Mwalim Mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi Nyerere Ndugu Gwantwa Mwasomola akitoa maelezo juu ya hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa shule ya awali na Msingi Mzalendo amesema ujenzi umekamilika yamesalia mambo madogo madogo ambayo mafundi wanaendelea kuyakamilisha ikiwa ni pamoja na kufunga milango , kupaka rangi baadhi ya sehemu chache zilizosalia pamoja na madawati.
Mwalim Gwantwa pia amekiri kuyapokea maagizo yote yaliyotolewa na mkuu wa Wilaya na kuahidi kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kumuita fundi aliyetengeneza madawati na kuhakikisha anayarekebisha madawati hayo kwa viwango vinavyotakiwa kulingana na muongozo aliopewa.
‘’Maagizo yote na maelekezo tumeyapokea na tutayafanyia kazi kwani Mafundi wetu wote wapo tutahakikisha wanakamilisha kazi zao lakini pia kwa maeneo yanayohitaji marekebisho tutayarekebisha kama ambavyo tumepokea maelekezo” alisema Gwantwa
Shule ya awali na Msingi Mzalendo ni miongoni mwa shule mpya zilizojengwa katika halmashauri ya Wilaya ya Chunya kupitia mradi wa BOOST kwa lengo la kuboresha sekta ya Elimu Nchini , shule hii inatarajiwa kuhudumia watoto wanaotaka maeneo mbalimbali katika kata ya Makongolosi.
Mkuu wa wilaya ya Chunya akiendelea na ukaguzi wa ujenzi wa shule Mpya ya Msingi na awali inayoyojengwa Kata ya Makongolosi Chunya
Mkuu wa Wilaya Mhe Mayeka akikagua madawati yaliyowekwa ndani ya Madarasa ya shule ya Msingi Mpya inayojengwa Kata ya Makongolosi
Mkuu wa wilaya ya Chunya akikagua vyoo vinavyojengwa kwenye shule ya Msingi mPya inayojengwa kata ya Makongolosi
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.