MKUU wa Wilaya ya Chunya Mhe. Mayeka S. Mayeka akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Wataalam toka Halmashauri ya Wilaya ya chunya wamefanya mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Mpembe kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo, Mkuu huyo wa Wilaya alianza kwa kuwataka wananchi wa kitongoji hicho kueleza matatizo yanayowakabili,
“Kikao chetu kipo wazi kabisa uwe huru kueleza kero yoyote na mimi nitaichukua kama nina uwezo wa kuitatua hapa hapa na wenzangu tutafanya hivyo lakini Kama ni lazima niende nikaifanyie kazi nitafanya hivyo pia.” Alisema Mhe. Mayeka.
Pia DC Mayeka aliwataka wananchi hao kuwa wawazi katika kueleza changamoto zao hata kwa mambo ambayo hawayafahamu vizuri waulize ili wapatiwe ufafanuzi mzuri kutoka kwa wataalam alioambatana nao.
Wananchi wa kitongoji cha Mpembe wengi wao walionekana kuwa na changamoto ya uelewa juu ya Shamba la Korosho, Huduma ya Afya, miundombinu ya barabara sambamba na kero ya shule kuwa mbali na maeneo wanapoishi.
Akieleza kero yake kwa Mkuu wa Wilaya, Ndugu Joseph Gamba alisema, matatizo yamekuwa yakiibuka mara kwa mara, kitu kinachowasababisha kushindwa kufanya mandeleo katika kitongoji chao.
“Hapo kipindi cha nyuma tuliambiwa tuhame huku kuna TANAPA, limetoka hilo limekuja suala la korosho, tunaambiwa tuhame humu ni eneo la shamba la korosho tunashindwa hata kufanya maendeleo”
Akijibu kero za wananchi hao kuhusu shamba la korosho, Mayeka amesema, wananchi wamepotoshwa sana kwa jinsi wanavyolizungumzia suala la korosho ambapo inaonekana wamepewa taarifa tofauti na suala lenyewe lilivyo.
“Sasa hivi baada ya kuligusa eneo la shamba la korosho imeonekana miundombinu yote ipo kule, kana kwamba hakuna maeneo mengine huku kwamba ukigusa eneo la korosho hamtajenga shule na kufanya maendeleo, sio kweli taarifa mlizopewa.” Aisema Mayeka.
“Hili shamba ni shamba ambalo Serikali inaligharamia lenyewe, hao wanaotoa visiki ni hatua za mwanzo zitakuja mashine kutengeneza vizuri na kuligawa, hilo litafanyika, hayo hayawezi kufanyika kama hakuna barabara nzuri itakayotufikisha Chunya.” Aliongezea Mayeka.
Aliendelea kusema serikali inatekeleza ujenzi wa daraja eneo la mbanga ili kuweza kutengeneza miundombinu ya barabara kuja katika mradi wa shamba la korosho utakaotekelezwa katika kitongoji cha Mpembe.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Ndg Curthbert Mwinuka amesema, Shamba la Korosho Lualaje limekuja baada ya uongozi wa Kijiji cha Lualaje kupendekeza mradi huo kufanyika katika kijiji chao eneo la Gibiso
“Tuliandika barua kwenye Serikali za Vijiji zote, lakini kijiji cha kwanza kujibu kwamba tuje ni kijiji cha Lualaje, lakini tuliwaandikia barua ile sio kunyang’anya mashamba ya wananchi, tuliwaambia tunataka kulima korosho kwenye misitu ya kijiji ambayo tunayovuna mkaa.” Alisema Mwinuka.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.