Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe. Mbaraka Alhaji Batenga amesema kwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025 Halmashauri ya wilaya ya Chunya ihakikishe inakusanya Bilioni 10 ili kuendana na kasi ya kuleta maendeleo kwenye Wilaya hiyo.
Batenga ametoa kauli hiyo wakati akitoa salamu za Serikali kwenye Baraza la Madiwani liloketi kujadili na kupitisha hesabu za mwisho wa mwaka wa Fedha 2023/2024 za Halmashauri ya wilaya hiyo mapema Agosti, 27 kwenye ukumbi wa Halmashauri uliopo jingo jipya la utawala
“Mwaka wa fedha 2023/2024 tumevuka lengo la kukusanya mapato kwa asilimia 50, tumekusanya Billion 9, mwaka ujao ni Bilioni 10 tujipange vizuri kukusanya mapato hakuna kurudi nyuma” amesema Batenga.
Aidha Mhe Batenga ameipongeza Halmashauri kwa kuandaa taarifa nzuri ya hesabu za fedha huku akiwataka watumishi wa Serikali kuhakikisha hoja zote zilizotolewa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali zote zinajibiwa vizuri ili Halmashauri isivuke mwaka huu wa fedha na viporo vya hoja.
Pia Batenga amewataka viongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanalipa likizo na malimbikizo mengine ya watumishi ili kuongeza Morali ya watumishi kufanya kazi kwa bidii jambo litakalopelekea Halmashauri kuendelea kuwatumikia wananchi wa wilaya hii.
Vilevile, Batenga aliwakumbusha watendaji wa Halmashauri kuhakikisha wanafanya maandalizi kwanza ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotaraji kufanyika Novemba mwaka huu huku akiwamkumbusha jukumu linguine la kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na shule ya awali, msingi na sekondari mwakani 2025.
Tanzania inatarajia kufanya Uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuchagua viongozi wa mitaa na vijiji ambao utafanyika Novemba 27, 2024 na badaye mwaka ujao uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2025 ambapo wananchi watachagua madiwani, wabunge na Rais kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Waheshimiwa Madiwani wakiendelea kupitia kitabu cha hesabu za mwaka wakati wa Mkutano wa baraza la Madiwani la kujadili na kupitisha hesabu za mwaka 2023/2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.