Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mbaraka Alhaji Batenga amewataka wananchi wakitongoji cha Simbalivu na Kijiji cha Itumba kuendelea kujiandikisha kwenye Daftari la Mkazi la Kitongoji ili waweze kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe Novemba 27, 2024 huku akiridhia ombi lao la kitongoji cha Simbalivu la kuendelea kubaki kijiji cha Itumba kilichopo kata ya Chalangwa
Akizungumza wakati wa Mkutano wake na wananchi wa kitongoji cha Simbalivu kilichopo kijiji cha Itumba kata ya Chalangwa mapema leo tarehe 18/10/2024 amesema Lengo la Serikali ni kuwaletea wananchi maendeleo hivyo amesema wananchi hao waendelee kujiandikisha kwenye daftari la mkazi la kitongoji na waendelee kuonekana kwenye kijiji cha Itumba kilichopo Kata ya Chalangwa tofauti na Ilivyokuwa hapo awali.
“Tunafahamu mbele yetu kuna zoezi la upigaji kura lakini kuna hatua za kujiandikisha lakini watu wote hawa hawajajiandikisha Je Mko tayari kujiandikisha leo? Hata sasa hivi uko tayari kujiandikisha? (Ndioooo) Nilikuja hapa tukafanya mkutano, mkaeleza mnahitaji nini (umeme, maji na mengine) na wataalamu wakafafanua kwamba kitongoji hiki kinapata umeme awamu hii na mtaalamu wa Maji alisema hapa tunakuja kuchimba maji bajeti ya 2024/2025, Sasa ili maendeleo hayo yafanyike lazima mjiandikishe ili tushirikiane na viongozi hao kuwaletea maendeleo. Tulichokubaliana ni kwamba mkajiandikishe na mtajiandikisha chini ya viongozi wa kitongoji cha simbalivu wakishirikiana na viongozi wa kijiji cha Itumba pamoja na viongozi wa Kata ya Chalangwa” Amesema Mhe Batenga
Kikao hicho cha Mkuu wa wilaya na wananchi kimekuja ikiwa ni siku moja baada ya wananchi kuzungumza na vyombo vya habari kugomea kitongoji hicho kuwekwa kata ya Sangambi Jambo ambalo limepelea kamati ya usalama kuitisha kikao cha Pande mbili yaani kata ya Sangambi na kata ya Chalangwa hatimaye kufikia maamuzi ya kuruhusu wananchi kujiandikisha na kusomeka kata ya Chalangwa
Ikumbukwe tarehe 16/09/2024 Serikali ilitangaza majina na mipaka ya vijiji na vitongoji, katika Tangazo hilo Kitongoji cha Simbalivu kilionekana kuwa sehemu ya Kijiji cha Sangambi jambo ambalo wananchi wa Kitongoji hawakubaliani nalo. Kamati ya usalama ikiongozwa na Mkuu wa wilaya imeridhia ombi lao na kuruhusu wajiandikishe kwenye kijiji cha Itumba, kata ya Chalangwa na Mpaka mchana wa saa tisa Kitongoji cha Simbalivu kimesajiri wakazi Zaidi ya 40 huku taarifa ya kijiji cha Itumba kwa ujumla itakujia baada ya Majumuisho saa kumi na mbili jioni baada ya vituo kufungwa.
Wananchi wa Kitongoji cha Simbalivu wakiwa kwenye mstari kuelekea kujiandikisha baada ya Kumalizana na Mkuu wa wilaya ya Chunya kuhusu Kitongoji hicho kusomeka Kijiji cha Itumba kilichopo kata ya Chalangwa, Tofauti na ilivyokuwa awali ambapo Kitongoji hicho kilisomeka kijiji cha Sangambi na kata ya Sangambi
Baadhi ya wananchi wakishangilia maamuzi ya Mkuu wa wilaya ya Chunya na wakiwa kwenye Mstari wakisubiria kujiandikisha kwenye Daftari la makazi la kitongoji
Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Batenga akiongoza kikao cha viongozi wa Kata mbili yaani kata ya Sangambi na kata ya Chalangwa ili kufikia suluhu juu ya wapi hasa kitongoji cha Simbalivu kinapaswa kuwepo
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.