Kutokana na elimu, maelekezo na ushauri unaotolewa na wataalamu wa Afya wilayani Chunya, Wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kupoata Chanjo ya polio awamu ya pili na hata ushiriki wao kwenye chanjo nyinginezo pamoja na mambo mengine ya afya yanayotekelezwa wilayani Chunya kupitia Wataalamu wa Afya wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya.
Chanjo ya Polio awamu ya pili inaendelea katika Mikoa ya nyanda za juu kusini kwa watoto walio chini ya miaka 8 ili kuwakinga na athari zinazoweza kujitokeza endapo ugonjwa wa polio utaikumba familia ambapo nje ya ulemavu kwa mtoto, madhara mengine yanweza kuwa ni kifo.
Ili lengo la serikali la kuwahudumia wananchi wake litimie lazima wananchi wa Chunya tuendelee kuhimizana sisi kwa sisi kwa mambo tunayoelekezwa na wataalamu wetu jambo litakalopelekea jamii kuwa salama na hatimaye kuendelea na shughuli za kila siku za uzalishaji mali.
Chanjo ya Polio awamu yapili inayolenga watoto wenye umri chini ya miaka nane (8) limeanza leo tarehe 2-5/11/2023 hivyo mwananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya hakikisha mtoto wako na hata mtoto wa jirani anapata chanjo hii maana ukimkinga mwanao tu na mtoto wa jirani ukamwacha bila kupata kinga bado mwanao yuko kwenye hatari ya kupata Ugonjwa huo kupitia kwa mtoto wa jirani ambaye atakuwa hajapata Chanjo ya Polio.
Kinga ni bora kuliko Tiba, wazazi tuendelee kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaopita kutoa chanjo hizo na pia tukumbushane kwamba Chanjo hizo ni bure na ni kwa usalama wa watoto wetu na jamii kwa ujumla.
Kauli mbiu inayoongoza zoezi la Chanjo ya Polio awamu ya Pili inasisitiza usalama wa watoto wetu “kila tone la Chanjo Humkinga Mtoto dhidi ya Ulemavu na Kifo, Mpeleke mtoto apate Chanjo”.
Tujifunze kidogo kuhusu Ugonjwa wa Polio
Polio ni Ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha Polio, ambacho huenezwa kwa kula chakula na kunywa maji yaliyochafuliwa na kinyesi cha mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huo.
Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu kwa kutozingatia kanuni za usafi na endapo mtoto mmoja atapata maambukizi, watoto wote watakuwa kwenye hatari ya kuambikizwa ugonjwa wa Polio.
Ugonjwa wa Polio hushambulia mishipa ya fahamu, na kusababisha kupooza kwa misuli hasa miguu, mikono au yote kwa pamoja na kwa wakati mwingine misuli ya kifua inayosaidia kupumua na kusababisha kifo.
Dalili za ugonjwa wa Polio ni pamoja na mgonjwa kuwa na homa kali, mafua, maumivu ya mwili, maumivu ya kichwa na shingo, ulemavu wa ghafla wa viungo.
Ifahamike kuwa, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wapo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa Polio, ingawa unaweza kuwapata watu wa rika zote.
Ugonjwa wa Polio unaweza kuzuiwa kwa kupata chanjo ya kukinga ya Polio pamoja na kuzingatia usafi wa mikono, usafi wa mazingira ikiwemo matumizi sahihi ya choo bora.
Nchini Tanzania chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio hutolewa mara 4 kwa mtoto kwa nyakati zifuatazo, mara tuu mtoto anapozaliwa, afikishapo wiki 6, 10 na 14 na wakati wa kampeni maalum zitakapohitajika.
Ni muhimu mtoto kupata chanjo wakati wa Kampeni za chanjo za Kitaifa hata kama amekamilisha ratiba ya chanjo kwa utaratibu wa kliniki.
Hivi ndivo zoezi la Chanjo ya Polio awamu ya Pili likiendela Halmashauri ya wilaya ya Chunya, wazazi wanaendelea kushirkiana na wataalamu wa Afya kuhakikisha watoto chini ya Miaka nane (8) wanapata Chanjo kwa usalama wa watoto wenyewe na jamii kwa ujumla
Mtaalamu wa Afya akiendelea na zoezi la Chanjo katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya lengo ikiwa ni kufikia watoto wote wenye umri tarajiwa (Chini ya miaka nane) bila kujali eneo la kijiografia na hata umbali wa eneo hilo kutoka makao makuu ya wilaya. kata ama kijiji, lazima watoto wote wafikiwe
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.