Halmashauri ya wilaya ya Chunya ikiwakilisha Mkoa wa Mbeya kwenye Mashindano ya Riadha yanayotambulika kwa jina la Twende Olympic yaliyofanyika mkoani Singida imeshika nafasi ya pili kwenye Mbio za Mita 1500, mita 400 na mita 100 ambapo wanafunzi washiriki kutoka ya Sekondari Sangambi waliwakilisha wanafunzi wengine katika Mashindano hayo
Mashindano hayo yamefanyika Mkoani Singida, viwanja vya Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo manispaa ya Singida, na yamedumu kwa siku mbili kuanzia tarehe 4-5/4/2024 ambapo Mwanafunzi Joel Samwel amekuwa Mshindi wa pili kwenye mbio za mita 1500, Peter Joseph ameshika nafasi ya pili kwenye mbio za mita 400 wakati Salum Adam akishika nafasi ya pili kwenye mbio za mita 100 wanafunzi wote ni kutoka Shule ya Sekondari Sangambi iliyopo kata ya Sangambi katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya.
Akitoa taarifa za mashindano hayo Kaimu afisa utamaduni na michezo wa wilaya ya Chunya Bi Hawa Mtonyole amesema vijana kutoka wilaya ya Chunya wamepambana sana kuhakikisha wanafanya kile walichoelekezwa na walimu wao wakati wa maandalizi ili kuhakikisha azma ya uongozi wa wilaya ya Chunya ya kufanya vizuri katika maeneo yote inatimia hata katika uga wa michezo
“Mashindano yalikuwa magumu sana ukizingatia mikoa ya Singida ni maarufu kwa riadha na katika mbio zote tulizoshiriki washindi wa kwanza wametoka mkoa wa Singida lakini kwa mazingira yetu kupata medali tatu na fedha shilingi laki mbili kwa kila mshindi sio haba hivyo lazima tuwapongeze vijana wetu wamefanya vizuri”. Alisema Mtonyole
Aidha kaimu afisa utamaduni na michezo wilaya ya Chunya ameshukuru uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya kwa namna ambavyo wanasimamia mambo mbalimbali jambo linalopelekea wao watumishi kujituma katika kutekeleza kila jambo linalowakabili ili kuhakikisha linakuwa na ufanisi mkubwa.
Naye afisa michezo Mkoa wa Mbeya Mwalimu Robert Mfugale amesema wilaya ya Chunya imechagiza medali tisa ambazo mkoa wa Mbeya umezipata kwani medali tatu kati ya medali tisa ambazo mkoa umepata zimetoka wilayani Chunya huku akisema kama Halmashauri bado kuna jukumu la kufanya kuhakikisha vipaji vya watoto vinalelewa vyema kutoka shule za msingi na Hatimaye shule za sekondari.
“Uwakilishi wa Chunya umechangia kuupaisha mkoa wa Mbeya kwani medali tatu toka Chunya imechangia katika medali tisa za mkoa wa mbeya, Kwenye sekondari lazima tuongeze usimamizi wa michezo kwani Shule za msingi wanafunzi wanafanya vizuri sana kwenye michezo ikiwepo riadha lakini wakifika sekondari wanapotea hivyo bado tuna kazi ya kufanya kuhakikisha tunaendelea kuwalea watoto ili waendelee kufanya vizuri wakifika sekondari. Pia kupitia michezo hii iwe fundisho kwetu ili kuandaa timu zetu kuelekea mashindano ya UMISETA” Amesema Mfugale
Msafara wa watu tisa (9) wanafunzi saba kutoka Shule ya Sekondari Sangambi, Mwalimu wa Michezo na Afisa Michezo wa wilaya wataungana na timu nzima kutoka mkoa wa Mbeya na kuanza safari ya kurudi mkoani Mbeya Kesho Jumamosi, na kwa mujibu wa afisa michezo wilaya Bi MtonyoleTimu hiyo itafikia Shule ya Sekondari Iyunga na Baadaye Jumapili itarejea wilayani Chunya wakiwa vifua Mbele vikipendezeshwa na medali za ushindi pamoja na kitita cha Fedha tasilimu Shilingi Laki mbili (200,000/=) kwa kila mshindi.
Ikumbukwe Chunya inafanya vizuri Maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu yake ya kawaida, Ni lengo la Uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya kuhakikisha inaendelea kufanya vizuri maeneo mbalimbali bila kujali changamoto zinazojotokeza wakati wa utekelezaji wa jukumu lengo ikiwa ni kufikia ufanisi stahiki
Timu ya wanafunzi saba na Walimu wao kutoka Halmashauri ya wilaya ya Chunya wakiwa kwenye viwanja vya Michezo Mkoani Singida. (Kutoka Kushoto waliokaa Bi Hawa Mtonhole Kaimu Afisa Michezo na Utamaduni (Mwenye tisheti nyekundu), Mwalimu wa Michezo kutoka Shule ya Sekondari Sangambi Mwalim Philimon J Lulimo)
Mwanafunzi Joel Samwel (Mwenye Bukta ya Njano) akielekea kuhitimisha safari ya mbio ya Mita 1500 ambapo yeye alikuwa Mshindi wa Pili akiwakilisha Mkoa wa Mbeya
Timu ya Riadha kutoka Chunya ikiwa kwenye picha ya Pamoja baada ya kupokea medali tatu kutoka katika mbio za aina umbali tofauti ikiwepo mita 1500, mita 400 na mita 100
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.