Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Maafisa Habari Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Seriksali za Mitaa kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ya kazi.
Waziri Mchengerwa ametoa wito huo leo, wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Habari wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Ofisi ya Rais-TAMISEMI kinachofanyika katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma uliopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma.
“Mmebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi hivyo msiwaache watanzania walishwe habari potofu” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, Maafisa Habari nchini ni rasilimaliwatu muhimu hivyo wakitambua wajibu wao na kujiimarisha kiutendaji ni wazi kuwa wananchi watapata taarifa sahihi kwa wakati.
“Iwapo kila mmoja wenu akiwa mzalendo na kutambua wajibu wake, habari mtakazozitoa ndio zitaaminiwa na kupokelewa na watanzania kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambayo imeshamiri hivisasa,” Waziri Mchengerwa amehimiza.
Waziri mchengerwa amesema, ana amini kwamba maafisa habari waliopo wana weledi na ujuzi unaowawezesha kutoa taarifa sahihi zenye tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Sanjari na hilo, Waziri Mchengerwa ameelekeza Maafisa Habari wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa washiriki kwenye ziara za viongozi ili wapate uelewa utakaowawezesha kutangaza kwa ufanisi mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Waziri Mchengerwa amewaelekeza waajiri katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha Maafisa Habari wanaokaimu ukuu wa vitengo ambao wana sifa, wapewe vitengo ili waweze kutekeleza kikamilifu jukumu la kuuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi zao ikiwa ni pamoja na kutangaza mafanikio yaliyopatikana kwenye eneo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambalo limepewa kipaumbele na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maafisa Habari wa Nyanda za juu kusini wakiwa na picha ya pamoja na Mhe. Waziri wa Nchi - TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa.
Maafisa Habari wa Mkoa, Halmashauri na Taasisi zilizopo TAMISEMI wakifutilia kwa makini kikao kazi cha siku mbili kilichofanyika Mkoani Dodoma, Mei 23-24, 2025.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.