Afisa ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndugu Nashi Mwalende amewataka wanaume wilayani Chunya kuacha kasumba na kuogopa bali wajitokeze katika ofisi za Ustawi wa Jamii ili kupata msaada pale wanapofanyiwa ukatili wa namna yoyote ile kuliko kujichukulia maamuzi ambayo baadaye yanakuja kuwa ni kinyume na sheria jambo ambalo linagharimu maisha yao na familia kwa ujumla
Akizungumza tarehe 25/7/2025 ndani ya studio za Redio Baraka ambapo Maafisa kutokaofisi za ustawi wa Jamii na Idara ya Maendeleo ya Jamii wilaya ya Chunya waliungana kutoa elimu ya ukatili ambapo Ndugu Mwalende, amesema ofisi za ustawi wa jamii wilaya ya Chunya ziko tayari kupokea wanaume wote na kuwahudumia huku akisema wapo maafisa wanaume ambao wanaweza kuwahudumia watu wanaotaka kuhudumiwa na afisa wa kiume
“Wanaume tunawaomba sana wajitokeze madawati yetu yako huru waondoe ile dhana kwamba wanawake wakienda ustawi wa jamii wanapendelewa kuliko wanaume sisi tutawahudumia wote kwa usawa kabisa, Tumekuwa tunapita maeneo mbalimbali kwenye vijiji wanaume wenyewe wameshuhudia kwamba nao wanafanyiwa ukatili jambo muhimu wajitokeze katika ofisi za ustawi wa jamii na kama wanaona shida kufika wanaweza kutupigia simu na kama bado wanaweza kuona shaka kwetu waende polisi dawati la jinsia”
Naye Afisa Mendeleo ya Jamii Nasra Hassan Mkupete ametaja aina mbalimbali za ukatili ikiwa ni pamoja na ukatili wa kiuchumi ambao unawakumba jinsi zote huku akisema wanaume wamekuwa wagumu sana kujitokeza kueleza na kutafuta msaada pindi wanapofanyiwa ukatili jambo linalopelekea wanaume wengi kuwa na msongo wa mawazo na wakati mwingine kutenda mambo ambayo kama wangejitokeza kutafuta msaada wasingefanya maamuzi ya namna hiyo
“Aina ya kwanza ni ukatili wa kimwili ambao husababisha madhara kwa mwili, ukatili wa kingono ambao mara nyingi hutokea kwa watoto wa kike, ukatili wa kisaikolojia ambao huathiri moyo, hisia na aina nyingine ya ukatili ni ukatili wa kiuchumi ambao hufanyiwa wanaume na wanawake lakini wanaume wengi huwa hawatoi taarifa kamili wanapofanyiwa ukatili”
Naye Groria Amandi Kavishe kutoka ofisi ya Maendeleo ya jamii wilaya ya Chunya amesema jamii inaweza kupata madhara mbalimbali kutokana na ukatili wa kijinsia hivyo jamii haina budi kupambana na ukatili wa aina yoyote ile ili kuhakikisha jamii inakuwa salama kwa manufaa ya jamii yenyewe na Taifa kwa ujumla.
“Pia kuna madhara yanaweza kutokea kutokana na ukatili mfano mtu anaweza kufa , umaskini ambao unaweza kutokea kutokana na mtu kuzuiwa kufanya kazi na mumewe jambo linaloweza kupelekea umaskini, msongo wa mawazo na madhara mengine mengi”
Maafisa hao wamefika Redio Baraka ili kutoa Elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wananchi ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kuhakikisha Jamii inaepukana na ukatili wa namna mbalimbali nakuwa na jamii salama huku shughuli za kujipatia kipato zikiendelea jambo ambalo litapelekea jamii kujikomboa kiuchumi
Nashi Mwalende afisa ustawi wa jamii akifafanua jambo walipokuwa Mubashara Redio Braka kutoa elimu ya Ukatili
Nasra Hassan Mkupete akieleza Jambo pindi Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa ustawi wa Jamii wilaya ya Chunya walipokuwa Mbashara Redio Baraka Kutoa elimu ya ukatili
Groaria Amandi Kavishe akiwa Mubashara Redio Baraka Maafisa toka wilaya ya Chunya walipofika kutoa elimu ya Ukatili
Maafisa kutoka wilaya ya Chunya katika Picha ya Pamoja ndani ya Studio za kurusha Matangazo za Redio Baraka baada ya kutamatisha Zoezi la uelimishaji Jamii kuhusu Ukatili kupitia Redio Baraka. Aliyekaa ni Frank Philip Mwandishi na Mtangazaji wa kipindi, aliyesimama kuanzia Kulia ni Nashi Mwalende kutoka ustawi wa Jamii, katikati ni Groria Kavishe na anayemalizia ni Nasra Hassan kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.