Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Mhe Ramadhan Shumbi amewata wananchi wa kijiji cha Lola kuendelea kuvumilia mpaka pale mifumo ya kifedha itakapokuwa sawa Milioni 50 iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuja kujenga zahanati ya Lola italetwa maana tayari ilishaingia Halmashauri lakini kinachokwamisha kwasasa ni mifumo ya kifedha
Makamu mwenyekiti ametoa kauli hiyo mwishoni mwa juma alipoiongoza kamati ya fedha. Uchumi na Mipango kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Lola ambayo mpaka sasa kupitia michango ya wadau wakishirikiana na wananchi imefikia kiwango cha kuezekwa, kupigwa ripu, kufungwa dari na sasa wanaendelea kupanga mawe tayari kukamilisha sakafu kwa gharama ya Millioni 16
“Ndugu viongozi na wananchi wa Lola fedha yenu kwaajili ya ujenzi wa zahanati hii ilishafika Chunya changamoto ilipo mpaka sasa ni mifumo ya kifedha hivyo ninyi vumilieni tu fedha hizo zitatolewa na zitawafika, epukeni wapotoshaji wanaotoa maneno mbalimbali ili kuwafini na serikali ya Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan
Aidha kamati hiyo kupitia makamu mwenyekiti wake imewataka wananchi na viongozi kutohujumu miundombinu mbalimbali ya serikali inayojengwa katika maeneo yao na amesema kamati haitakubali miradi mbalimbali kuhujumiwa na mtu yeyeto bila kujali nafasi yake ama uwezo wake kifedha kwani lengo la serikali ni kuwarahisishia wananchi wake upatikanaji wa huduma mbalimbali katika maeneo wanayoishi
“Hatutamwacha salama mtu yeyote atakaye hujumu miradi ya maendeleo na nawaomba msijitokeza kuwasaidia watu wa namna hiyo wakibainika kuhujumu miundombinu yetu, achene tu sheria ichukue mkondo wake ili wajifunze na wapate adabu” Alisema Mhe Shumbi
Naye Nebart Gavu kwa niaba ya afisa mipango na uratibu wa wilaya ya Chunya amewahakikishia wananchi wa lola kwamba Changamoto iliyopo sio kwa fedha za zahanati ya Lola tu bali ni Halmashauri zote huku akitaja miradi mbalimbali yenye thamani ya Zaidi ya Bilioni Mbili pia pesa zimekwama kutokana na mifumo ya kifedha hivyo mifumo ikiwa sawa fedha hizo zitafika na kuendelea kumalizia mradi huo kama ilivyokusudiwa
Katibu tawala wa wilaya ya Chunya Ndugu Anakleth Michombero amewataka viongozi na wananchi wa kijiji hicho kuendela kushirkiana katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo kama walivyofanya katika ujenzi wa Zahanati hiyo kwakufanya hivyo hata miradi mingine itakayoletwa katika kijiji itafanikiwa pia
Kamati hiyo pia imeshauri uongozi wa kijiji hicho kuendelea kupanda miti kuzunguka eneo hilo la Zahanati huku wakichukua tahadhari ya umbali kutoka eneo jengo lilipojengwa ili kuepusha miti hiyo kuanguakia jengo hilo hapo mbeleni jambo linaloweza kuleta hasara isiyo ya lazima na kuisababishia hasara serikali na hata wananchi wa kijiji hicho pia
Zahanati ya kijiji cha Lola mpaka hatua ilipofika imegharimu Zaidi milioni 16 ambapo Nguvu za wananchi ni milioni 12,200,000/=, Wadau wa maendeleo wamechangia shilingi milioni mbili (2,000,000/=) huku serikali imetoa milioni Hamsini (50,000,000/=) kwaajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.