Mthibiti ubora wa shule wilaya ya Chunya mwalimu Arton Joseph Kayombo awajengea uwezo walimu wakuu wa shule za sekondari na maafisa elimu kata juu ya utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa ukihusisha mafunzo ya amali na mafunzo jumuishi.
Mafunzo hayo yametolewa leo, Januari 24, 2025 katika ukumbi mdogo wa mikutano wa shule ya sekondari Kiwanja yakiwa na lengo la kuwaandaa walimu wanaofundisha shule za sekondari juu ya utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa.
“Utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa utaleta mabadiliko makubwa sana kwa jamii kwasababu malengo yake ni kuaandaa wanafunzi wenye uwezo wa kujitegemea kwakuwa elimu ya mafunzo ya amali inatolewa kwa vitendo na itapelekea kupunguza tatizo la upatikanaji ajira nchini” amesema Kayombo.
Aidha Mwalimu Kayombo amewahimiza walimu wakuu wa shule za sekondari kuendelea kutoa mafunzo endelevu shuleni(MEWAKA)ili kuwajengea uwezo walimu walio chini yao kuweza kutoa mafunzo yenye tija kwa kufuata mtaala wa mafunzo.
Awali akifungua mafunzo hayo, mwenyekiti wa wakuu wa shule za sekondari Wilaya ya Chunya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Isangawana mwalimu Sikitu Wakson Shurra amesema ni wakati muwafaka sasa kwa walimu wakuu na maafisa elimu kata kuwasimamia walimu wanaofundisha kwenye shule zao za sekondari kuhakikisha maandalio ya somo na ufundishaji unaokidhi viwango na vigezo vilivyopo kwenye mtaala mpya ulioboreshwa unazingatiwa ili uleta tija.
Mwalimu Shurra amesema, walimu wakuu wanapaswa kukagua ufundishaji wa walimu ikiwemo ukaguzi wa andalio la somo, mpango na zana za kufundishia kama vinakidhi mahitaji ya somo husika.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Mayeka, mwalimu Flora Mwanchuli amesema Mabadiliko ya mtaala mpya ulioboreshwa utamfanya mwanafunzi atayehitimu mafunzo kwa ngazi ya sekondari kuwa na ujuzi utakaomsaidia kwenye maisha kwakuwa mafunzo ya amali yatatolewa kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne.
Kwa upande wake Afisa elimu kata ya Chalagwa, Fatuma Mahenge amesema, mtaala mpya ulioboreshwa una stadi nyingi za vitendo zinazompa chaguzi mbalimbali mwanafunzi kujifunza kitu anachokipenda na baada ya kuhitimu mafunzo mwanafunzi ataweza kumudu kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kwakuwa alijifunza akiwa shuleni kupitia mafunzo ya amali na jumuishi.
Mafunzo ya mtaala mpya ulioboresha unahusisha mafunzo jumuisha na mafunzo ya amali ambapo utekelezaji wake umeshaanza kwa baadhi ya shule za sekondari nchini huku ukitajwa kuwa na tija kubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu.
Mwenyekiti wa wakuu wa shule za sekondari Wilaya ya Chunya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Isangawana mwalimu Sikitu Wakson Shurra akifungua mafunzo ya utekelezaji wa mtaala mpya ulioboreshwa kwa walimu wakuu na maafisa elimu katika ukumbi mdogo wa mikutano wa shule ya sekondari Kiwanja.
Mthibiti ubora wa shule Wilaya ya Chunya mwalimu Arton Joseph Kayombo akitoa mafunzo ya utekelezaji wa mtaala mpya ulioboreshwa kwa walimu wakuu na maafisa elimu katika ukumbi mdogo wa mikutano wa shule ya sekondari Kiwanja.
Walimu wakuu na maafisa elimu wakimpongeza mtoa mada wa mtaala mpya ulioboreshwa, Mthibiti Ubora shule Wilaya ya Chunya Arton Joseph Kayombo katika ukumbi mdogo wa mikutano wa shule ya sekondari Kiwanja, Januari 24, 2025.
Walimu wakuu na maafisa elimu wakifutia kwa makini mada mbalimbali za utekelezaji wa mtaala mpya ulioboreshwa katika ukumbi mdogo wa mikutano wa shule ya sekondari Kiwanja, Januari 24, 2025.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.