Mkurugenzi wa zao la Tumbaku kutoka Bodi ya Tumbaku Tanzania ndugu Nicholaus Mauya amewataka viongozi wa bodi za vyama vya ushirika kuwasimamia wanachama wao ili wazalishe Tumbaku yenye ubora na viwango kuendana na mahitaji ya soko ili tumbaku hiyo iweze kuuzwa kwa bei nzuri na hatimaye kuleta faida kwa wananchi na taifa kwa ujumla
Mauya ametoa ushauri huo jana tarehe 08/03/2024 wakati alipoungana na timu ya Tathimini ya zao la Tumbaku inayoendelea na zoezi la Tathimini ya zao hilo kwenye mkoa wa Kitumbaku Chunya ambapo zoezi hilo jana liliendelea kwenye vyama vya ushirika vya Igangwe na Mtanila ambapo timu zote mbili yaani timu A na Timu B zote zilifanya kazi ya Tathimini ya zao katika Vyama hivyo viwili
“Ni muhimu sana kuhakikisha tunaenda sambamba na mahitaji ya soko hivyo sisi kama viongozi tuendelee kutoa elimu kwa wakulima wetu ili wazingatie ubora na viwango vinavyohitajika vya uzalishaji wa Tumbaku ili masoko yatakapoanza wakulima wetu wauze kwa bei nzuri jambo ambalo litapelekea wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa uzalishaji wa zao la Tumbaku kufaidika”Alisema Mauya
Aidha Mauya amepongeza namna wadau wa zao la Tumbaku walivyojitokeza kwa wingi katika zoezi la Tathimini ya zao kwa mwaka huu huku akiwataka kuendelea kujitokeza kwa wingi namna hiyo ili kufanya zoezi la Tathimini kuwa na uhalisia jambo litakalopelekea upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazosaidia kupanga mipango mbalimbali ya hapo mbeleni na hata katika kipindi cha masoko
“Wajumbe ni watu/ wadau muhimu katika uzalishaji wa tumbaku hasa kipindi hiki cha Tathimini ya zao la Tumbaku hivyo niwapongeze kushiriki kwa wingi na kwa mchanganyiko kutoka taasisi mbalimbali zinazohusika kwenye mnyororo wa uzalishaji wa Tumbaku” Aliongeza Mauya
Awali kabla ya Kumkaribisha mkurugenzi wa zao la Tumbaku, Meneja wa kanda ya Iringa ya Iringa inayojumuisha Mkoa wa Iringa, Ruvuma na Mbeya Ndugu Mohamed Kifunko amepongeza mwitikio wa wadau pamoja na ushirikiano mkubwa aliouona kwa timu ya tathimini mwaka huu 2024 katika kipindi cha siku mbili alizoshiriki zoezi la Tathimini na kusema malengo ya Tathimini yatapatikana kwa ushirikiano na sio vingine
Meneja uendeshaji kutoka Chama kikuu cha Ushirika cha Tumbaku Chunya CHUTCU ndugu Juma Shinshi ameyataka Makampuni ya ununuzi wa Tumbaku kuwafundisha wakulima kugredi Tumbaku kwa vitendo na sio kwa nadharia akisema makampuni wanayo nafasi ya kuwasaidia wakulima wao ili waweze kupata bei stahiki
“Nendeni mkawafundishe wakulima wenu kugrade Tumbaku kwa vitendo na sio kutoa elimu ofisi tu hiyo inakuwa nadharia, wafundisheni kwa vitendo kwamba hii Tumbaku ni daraja la kwanza na hii daraja gani na mnayo nafasi ya kufanya hivyo na kwa kufanya hivyo hatutapata changamoto wakati masoko yatakapofunguliwa” alisema Shinshi
Kiongozi wa msafara wa Tathimini ya zao la Tumbaku mwaka 2024 ambaye pia ni katibu wa wadau wa Tumbaku mkoa wa Kitumbaku Chunya Ndugu Faustine Mtweve amewapongeza wadau walioko kwenye timu ya Tathimini pamoja na wajumbe wanaosaidia kuongoza mashamaba kwenye vyama husika akisema wameonesha ushirikiano mkubwa jambo ambalo bila shaka amesema litaleta matokeo yaliyokusudiwa.
Akihitimisha kikao cha Majumuisho, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Mtanila Ndugu Ayubu Hussein aliwashukuru wadau wote waliofika na kushriki zoezi la Tathimini ya zao la Tumbaku na kuahidi kuwasimamia wakulima wao katika hatua zote ili kuhakikisha hawaathiri uboro unaohitaji sokoni na hatimaye wakulima wapate bei stahiki ambayo itasaidia kukidhi maisha yao ya kila siku.
Zoezi la Tathimini ya zao la Tumbaku mwaka 2024 lilianza rasmi tarehe 04/03/2024 na linataraji kuhitimishwa rasmi tarehe 22/03/2024 kwa kikao maalumu ambapo kupitia kikao hicho takwimu ambazo ni matokeo ya tahimini ya zao inayoendelea sasa zitatolewa na kupitia takwimu hizo ndio msingi wa maandalizi ya msimu mwingine wa kilimo yaani msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025
Mkurugenzi wa zao la Tumbaku ndugu Nicholaus Mauya (Aliyevaa shati jeupe na ameshika notebook mkononi mwake) akishuhudia tathimini ya zao la Tumbaku katika moja ya Shamba la mwananchama wa Chama msingi cha Mtanila
Meneja wa kanda ya Iringa ndugu Mohamed Kifunko akifafanua jambo wakati wa kikao cha tathimini baada ya kuhitimisha zoezi la tathimini ya zao la Tumbaku katika ukumbi wa Chama cha msingi Mtanila
Meneja uendeshaji kutoka Chama kikuu cha Ushirika cha Tumbaku Chunya CHUTCU ndugu Juma Shinshi akizungumza jambo mbele ya wajumbe wa bodi ya Chama cha Ushirika cha Mtanila pamoja na wataalamu waliojumuika katika zoezi la tathimini ya zao mwaka 2024
Katibu wa wadau wa Tumbaku mkoa wa kitumbaku Chunya Ndugu Faustine Mtweve akizungumza mbele ya wajumbe wa kikao cha tathimini ya zao la Tumbaku baada ya kuhitimisha zoezi la kufanya Tathimini katika chama cha msingi cha Mtanila
Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika cha Mtanila Ndugu Ayubu Hussein akitoa salamu za chama kwa niaba ya wanachama wa chama cha msingi cha suhirika cha Mtanila mbele ya wageni waliofika kwaajili ya kufanya tathimini ya zao la Tumbaku kwa mwaka 2024 (Hapo ilikuwa kikao cha Majumuisho)
Mkurugenzi wa zao la Tumbaku kutoka Bodi ya Tumbaku Tanzania ndugu Nicholaus Mauya aking'oa majani kwenye moja ya Mashamba ya wanachama wa chama cha msingi cha Ushirika Mtanila wakati alipopata nafasi ya kushiriki zoezi ya Tathimini ya zao la Tumbaku inayoendelea kwenye mkoa wa kitumbaku Chunya
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.