Timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya imewataka wahandisi wa ujenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya kusimamia kwa weledi miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo ili ilete tija iliyokusudiwa kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.
Akiwa katika ukaguzi wa ujenzi wa uzio wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya leo tarehe 18/12/2024, Kiongozi wa timu hiyo ya wataalamu Ndugu Mohamed Mkindi amesema mafundi wa kujenga uzio huo waongezeke ili kuharakisha ujenzi wa uzio huo kabla ya kipindi cha Masika hakijafika huku akiwataka wahandisi wa Halmashauri kusimamia hilo.
“Nimeambiwa hapa kwenye taarifa kuwa kuna mafundi 16 tu wanaofanya kazi hii ya ujenzi wa uzio wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya nataka mafundi waongezeke wafike 40 ili kuharakisha ujenzi wa uzio kabla ya kipindi cha mvua hakijaanza ambapo itapelekea kuchelewesha kazi na vifaa vya ujenzi vitapanda bei” amesema Mkindi.
Aidha, timu hiyo ya wataalamu toka Mkoani imetembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja katika shule ya mchepuo wa Kiingereza ya Chunya yaani (Chunya Pre and Primary English Medium School)ambapo amemtaka mhandisi wa Halmashauri kumsimamia Mkandarasi kukamilisha ujenzi kabla ya shule kufunguliwa Januari 16, 2025.
“Mhandisi msimamie Mkandarasi ili akamilishe ujenzi na thamani ya fedha ionekane. Fanyeni utaratibu ada ya mafunzo iwe nafuu kulinganisha na shule nyingine ili kupata wanafunzi wengi na tija ya kuanzisha shule ya mchepuo wa kiingereza ionekane” amesema Mkindi.
Katika hatua nyingine Mkindi alikagua ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya inayojengwa jirani na jengo jipya la Halmashauri ambapo nyumba hiyo imefikia asilimia tisini kukamilika huku Mhandisi wa Halmashauri akiahidi kusimamia kwa ukaribu kukamilisha ujenzi uliobaki ikiwemo uzio, mageti,kusawazisha eneo na ununuzi wa samani.
Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ikiongozwa na Mohamed Mtindi ikikagua mradi wa ujenzi wa uzio wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya Iliyopo Chunya mjini.
Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ikiongozwa na Mohamed Mtindi ikikagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Chunya inayojengwa jirani na jengo jipya la Halmashauri.
Muonekano wa uzio wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji ukiwa umefikia asilimia 57 ya kukamilishwa kwake ambapo inatarajiwa kukamilishwa mwishoni wa mwezi Januari, 2025.
3Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ikikagua ujenzi wa Vyumba vitatu na ofisi moja ya shule ya mchepuo wa kiingereza ya Chunya.
Muonekano wa majengo ya vyumba vitatu na ofisi moja ya Shule ya mchepuo wa kiingereza Chunya inayoendelea na ujenzi ambapo inatarajiwa kukamilika mwanzoni wa Mwezi Desemba, 2025.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.