Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Mhe Bosco Said Mwanginde amewataka viongozi wote kushirikiana na wananchi kuhakikisha biashara ya Mkaa wilayani humo inakomeshwa haraka sana na amesema kuendelea kwa biashara hiyo ni ishara kwamba viongozi hao wanahusika na biashara hiyo hivyo hatua zitaanza kuchukuliwa dhidi yao
Ametoa kauli hiyo jana tarehe 5/4/2023 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara Kitongoji cha Kambikatoto kilichopo kijiji cha Shoga kata ya Sangambi baada ya kuhitimisha zoezi la kutembelea na kuona uharibifu mkubwa wa Mazingira unaosababishwa na shughuli za Uchomaji wa Mkaa
“Sitaki mkaa utoke tena hapa kwa namna yoyote ile na kama tukiona mkaa unatoka huku basi sisi serikali tutaamini wajumbe wa serikali mnahusika hivyo tutaanza na ninyi viongozi na baadaye tuwafuate wale wale waharibifu wa mazingira. Haya ni amelekezo kutoka baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya”
Aidha Mhe. Mwanginde alimtaka mwenyekiti wa kijiji cha Shoga kuhakiki wananchi wanaoishi katika eneo hilo kama ni wakulima ili kuendana na mpango wa matumizi ya ardhi wa mwaka 2006 ambao unaonesha eneo hilo ni kwaajili ya kilimo na makazi hivyo shughuli zinazotakiwa eneo hilo ni kilimo sio uchomaji wa mkaa
“Mwenyekiti wa kijiji, anayetakiwa kuwepo hapa ni mkulima hivyo hakikini mashamba ya watu na asiye na shamba hatakiwi kuwepo hapa, anayetaka kukata mkaa afuate taratibu na kinyume na hapo basi tutamshughulikia ipasavyo” alisema Mwanginde
Awali akitoa salamu za kata kwa mwenyekiti wa halmashauri Diwani wa kata ya Sangambi Mhe. Junjulu Ndete amesema uharibifu wa mazingira ni mkubwa sana maeneo haya jambo ambalo halikubaliki kabisa, ameongeza kuwa kama hatutajipanga kulinda mazingira haya basi tutakaribisha ukame ambao utapelekea njaa kwetu sisi na taifa kwa ujumla.
“Miaka miwili iliyopita tulikuwa tunaenda Mnyolima, tulipotea njia tukapita hapa, Hali tuliyoikuta mwaka juzi tofauti kabisa na hali tuliyoiona leo, uharibifu wa mazingira ni Mkubwa mno” alisema Mhe Junjulu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya amehitimisha ziara iliyodumu kwa siku mbili tarehe 4/4/2023 na tarehe 5/4/2023 katika kata ya Sangambi ambapo lengo kubwa ni kukemea uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli za uchomaji mkaa katika kata hiyo na kupitia mikutano hiyo amewataka wananchi wote wilayani Chunya kushiriki zoezi la kutunza na kulinda Mazingira kwani ukame hauna mipaka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Mhe Bosco Mwanginde akizungumza na Wananchi juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kwenye mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Kambikatoto kilichopo kijiji cha shoga kata ya Sangambi
Mwenyekiti wa Halmashauri wa wilaya ya Chunya Mhe Bosco Mwanginde akishuhudia uharibifu wa mazingira unaosababishwa na uchomaji wa Mkaa katika kijiji cha Shoga kata ya Sangambi
Diwani wa Kata ya Sangambi Mhe. Junjulu Ndete akieleza jambo kabla ya kumkaribishwa Mweshimiwa Mweyekiti wa halmashauri kuzungumza na wananchi wa kitongoji cha Kambikatoto
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.