Wenyeviti na wajumbe wa Halmashauri ya vijiji vya Mwiji na Lualaje, tarafa ya Kipembawe wamejengewa uwezo kwenye mafunzo ya siku moja ya utawala bora, uongozi na manajimenti ya rasilimali fedha ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuthibiti matumizi mabaya ya rasilimali fedha.
Afisa Tarafa ya Kipembawe, Kasim Salimu Kilondomara ametoa mafunzo hayo Machi 21, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Lualaje uliopo, tarafa ya kipembawe Wilayani Chunya, ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kuboresha utendaji kazi na utawala bora kwa watumishi wa umma wa tarafa ya Kipembawe.
“Nimefanya tafiti nimegundua kuwa, vijiji vingi havikusanyi mapato mengi ilihali fursa ya kukusanya ipo, miradi mingi iliyopo katika ngazi ya kijiji haisimamiwi ipasavyo na wananchi wamekuwa na kero za muda mrefu ambazo hazipatiwi ufumbuzi ndio maana nimeamua kutoa mafunzo haya ili kuwajengea uwezo wenyeviti wa vijiji na wajumbe ya Halmashauri ya vijiji kujidhatiti kutoa huduma bora kwa wananchi” amesema Kilondomara.
Aidha, Kilondomara amebainisha kuwa, wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa Halmashauri ya vijiji walipatikana baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa kumalizika mwezi Novemba, 2024 hivyo baadhi yao hawana uzoefu kufanya kazi, semina hiyo imelenga kuwafahamisha majukumu yao, muundo wa kijiji, mipaka ya kiutawala, kutatua kero za wananchi, kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi na kuongeza tija ya kukusanya mapato.
“Nimeshatoa mafunzo haya ya elimu ya utawala bora, uongozi na menejimenti ya fedha kwa vijiji 23 vya Tarafa ya Kipembawe bado kijiji kimoja tu, nikihitimisha mafunzo nitafanya tathimini kubaini mabadiliko ya utendaji kazi kwa kila kijiji na kuchukua hatua stahiki kwa kijiji kitakacho kiuka miongozo na taratibu za kisheria kutoa huduma kwa wananchi” amesema Kilondomara.
Kilondomara amewasisitiza wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa Halmashauri ya vijiji kuwahimiza wananchi kushiriki kwenye mikutano ya hadhara na kuchangia fursa mbalimbali kwenye miradi ya maendeleo inayoletwa na serikali kuu vilevile kuibua na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya vijiji vyao.
“Viongozi wa vijiji munapaswa kufanya mikutano ya hadhara na kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya vijiji kuonesha uwazi na matumizi bora ya rasilimali fedha ambazo ni msingi wa maendeleo ya vijiji vyetu” amesema Kilondomara.
Naye, mjumbe wa kamati ya mipango, Uchumi na Fedha wa kijiji cha Mwiji, Joseph Mathias, amesema semina walioipata inawapa nguvu kubwa ya utendaji kwenye masuala mbalimbali ikiwemo manunuzi, upangaji wa bajeti, matumizi bora ya fedha na uwajibikiaji wa kiongozi kwa ngazi ya Halmashauri ya Kijiji.
“Mafunzo tuliyopata hapa tunaenda kuyaishi kwa kufanya kazi hususani kamati ya fedha kwa kuwa tuikuwa tunafanya kazi kwa kutumia busara sasa tumejengewa uwezo na tumepata miongozo wa kufanya kazi kwa weledi” amesema Mathias.
Atupokile Japheti Mwakibata, Mjumbe wa Halmashauri ya kijiji cha Lualaje, Kamati ya Mipango, Fedha na Uchumi, amemshukuru Afisa Tarafa ya Kipembawe kwa semina hiyo ambayo imemuongezea uelewa namna ya kuwatumikia wananchi na kuongeza mapato ya kijiji kwa kuibua vyanzo mbalimbali vya mapato kwa kushirikiana na wajumbe wenzake na wananchi.
Mafunzo ya siku moja ya elimu ya utawala bora, uongozi na menejimenti ya fedha yametolewa na Afisa Tarafa ya Kipembawe, Kasim Salimu Kilondomara na kuhudhuriwa na Watendaji, Wenyeviti na Wajumbe wa Halmashauri ya kijiji cha Mwiji na Lualaje ili kuonengeza ufanisi wa utendaji kazi na kuhakikisha maendeleo ya vijiji yanawanufaisha wananchi.
Wenyeviti wa Kijiji na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji wakifuatilia kwa makini mafunzo ya Utawala bora, Uongozi na Menejimenti ya fedha iliyotolewa katika ukumbi wa shule ya Sekondari Lualaje.
Afisa Tarafa ya Kipembawe, Kasim Salimu Kilondomara akitoa mafunzo ya Utawala bora, Uongozi na Menejimenti ya fedha kwa Wenyeviti wa Kijiji na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji katika ukumbi wa shule ya Sekondari Lualaje.
Wenyeviti wa Kijiji na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa Tarafa ya Kipembawe baada ya kutamatika kwa semina ya siku moja ya Utawala bora, Uongozi na Menejimenti ya fedha iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Lualaje.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.