Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe: Juma Zuberi Homera amesema azma ya serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha Mkoa wa Kimadini Chunya unatoka kwenye uzalishaji wa Dhahabu kilogramu 300 na kufika kilogramu 500 kwa mwezi na amewataka wachimbaji na wananchi kwa ujumla kuendelea kumunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali kwa ujumla ili lengo la kuwainua wananchi kiuchumi litimie
Amezungumza hayo jana (9/2/2023) akiwa katika siku ya pili ya ziara yake maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kimadini Chunya ambapo ametembelea wachimbaji wakubwa na wadogo Kijiji cha Itumbi, msitu wa Mbiwe, Makongolosi na Mwaoga ambapo amewataka kufanya kazi kwa bidii kwani serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa kila mtu kufanya shughuli za uchimbaji
Akiwa katika Kijiji cha Itumbi baada ya kusikiliza kero mbalimbali za wachimbaji na wananchi Mkuu wa Mkoa ameongoza Zoezi la Uchangishaji wa fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Shule ya sekondari ili kutatua kero ya kukosekana kwa sekondari eneo hilo, ambapo zaidi ya Milioni tatu zilipatikana, wananchi wakichangia Milioni moja laki tatu na ishirini na moja (1,321,000/=) na ofisi yake ikichangia milioni mbili (2,000,000/=)
Shule hiyo amependekeza kuitwa MASACHE SEKONDARI kama kumuuenzi Mbunge wa jimbo la Lupa, hata pindi atakapo maliza muhula wake, aidha kwa lengo la Mbunge huyo kuwa mlezi na Msimamizi tangu hatua za ujenzi mpaka kukamilika kwake
Aidha Mhe; Homera amewaonya viongozi wa serikali kuanzia ngazi za vijiji, kata na hata wilaya kutotumia vibaya nafasi zao kwa kuwanyanyasa wananchi jambo ambalo amesema sio lengo la serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Rais Mhe: Dkt Samia Suluhu Hassan.
“Watu wataendelea kuchimba madini na hakuna mtu atakaye wazuia, ninyi fuateni taratibu. Hata ninyi (wachimbaji wadogo) mnaweza kujiunga pamoja mkaenda ofisi za Madini na kwa wakala wa misitu (TFS) mkaomba kibali ili mpate maeneo ya uchimbaji kwenye msitu wa mbiwe na hakuna atakaye waondoa”
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya amewataka wachimbaji hao wanapopata faida katika uchimbaji wa dhahabu kuhakikisha wanawekeza Chunya kwani muda utafika ambapo hawataweza kufanya kazi hiyo tena hivyo unahitaji kuwa na eneo la kuishi na hata kukuingizia kipato
“Mnapopata pesa angalau asilimia hamsini (50%) wekezeni kwa kujenga nyumba za biashara, hoteli na biashara nyingine kwaajili ya kupata pesa na maisha yako ya baadaye”
Muhifadhi misitu wilaya ya Chunya Ndugu. Innocent Lupembe akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa amesema msitu wa Mbiwe ni hifadhi ya serikali kuu na inahifadhiwa kwa lengo la kuhifadhi na kutunza vyanzo vya maji, hivyo tunawakaribisha wananchi na wawekezaji kuja kuomba kibali cha uchimbaji huku utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji unazingatiwa
“Haturuhusu miti kukatwa ndani ya hifadhi, miti yote inayotumika katika shughuli za uchimbaji ndani ya hifadhi hii (Mbiwe) inatoka nje ya hifadhi, tunawakaribisha wadau kuja kuomba vibali vya uchimbaji wa madini katika msitu wa Mbiwe”
Afisa madini Mkazi wa Mkoa wa kimadini Chunya Eng. Nyansiri Sabai amesema wachimbaji katika Mkoa wa Kimadini Chunya wanafuata sheria na taratibu zote za uchimbaji wa madini huku akiwakaribisha wadau wengine kuwekeza kwenye madini kwakufuata taratibu
“Watu hawa wanatekeleza sheria na wengine wanakaribishwa lakini wafuate utaratibu”
Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya imedumu kwa siku mbili katika mkoa wa kimadini chunya ambapo ametembelea maeneo mbalimbaji ya uchimbaji ili kujionea na kusikiliza kero za wachimbaji wakubwa na wadogo na kuzitatua zinazowekekana kwa wakati huo na kutafuta suluhu kwa zile ambazo hazikuwezekana kwa wakati huo
Wananchi wa Kijiji cha Itumbi wakiwa kwenye Mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera wakati wa ziara yake ya Kutembelea sekta ya madini katika Mkoa wa Kimadini Chunya
Muonekano wa kijiji cha Itumbi kata ya Matundasi wilayani Chunya.
Wachimbaji wadogo wadogo wa Dhahabu katika kijiji cha Itumbi wilayani Chunya wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera wakati wa ziara yake ya kutembelea sekta ya madini katika mkoa wa kimadini Chunya
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.