MKUU wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Z. Homera amewaasa wakulima kufuata mbinu bora za kilimo zinazotolewa na maafisa kilimo na kuacha kuchanganya tumbaku ili soko liweze kwenda vizuri.
Homera ameyasema hayo wakati akifungua soko la ununuzi wa zao la Tumbaku katika kijiji cha Bitimanyanga, kata ya Mafyeko wilaya ya Chunya.
“Tumezindua soko letu la tumbaku leo, wataalam wetu wametuonesha jinsi gani ambavyo tumbaku yetu imekuwa na thamani nzuri na imekuwa na ubora,” amesema Homera.
Aidha, aliwataka wakulima kuacha tabia ya kuchanganya tumbaku, kwani kwa kufanya hivyo, athari mbalimbali zinaweza kujitokeza ikiwemo kupoteza soko kibiashara.
"Pia kumekuwa na changamoto ya wakulima kuchanganya tumbaku na kupelekea tumbaku kukataliwa sokoni na kurudishwa kwa mkulima ili aweze kuchambua na kuipanga vizuri."
Halikadhalika, Mhe. Homera amewataka maafisa ugani kuhakikisha wanawasaidia wakulima katika kuichambua tumbaku na kuipanga vizuri ili kuweza kuingia sokoni na kununulika kwa wakati.
“Haya mambo ya kuchanganya tumbaku ndio nasisitiza sasa maafisa ugani kufanya kazi yao vizuri kwa mkulima isiishie kumsaidia kwenye kulima tu hata kwenye kuchambua tumbaku inabidi asaidiwe." Alisisitiza Homera.
Vile vile amewaomba wanunuzi wakuu wa tumbaku kutanguliza busara pindi wanapo nunua tumbaku kwani kwa msimu huu kumekuwa na changamoto kubwa ya hali ya hewa, ikiwemo upungufu wa mvua na kupanda kwa pembejeo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Homera amewataka wanunuzi kuhakikisha wanawapatia wakulima fedha zao kwa wakati ili waziweke kwenye mzunguko na kutatua changamoto zao za kiuchumi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe Mayeka S. Mayeka amesema, Bitimanyanga ni sehemu ambapo zao la tumbaku linalimwa kwa wingi na ndio zao lao kuu la kibiashara na kuwasisitizia wakulima wa tumbaku kuepuka utoroshaji wa zao hilo kwani atakayekamatwa anafanya hivyo sheria kali zitachukuliwa dhidi yake ikiwa pamoja na kutaifishwa kwa tumbaku hiyo.
"Utoroshaji wa tumbaku ni tatizo kubwa, kila mwaka tumekuwa tunakamata, mwaka juzi na mwaka jana tumekamata naamini hata mwaka huu kama watafanya tutakamata tu.
“Mimi niwaombe sana hatuna sababu ya kutaifisha tumbaku ya mtu, hebu fuata utaratibu kamati ya ulinzi na Uslama wilaya ipo makini, nawapongeza wale wanaoendelea kutupa taarifa." Alisema Mayeka.
Naye mnunuzi mkuu wa tumbaku Chunya Ndg Ally Ramadhni amesema kiujulma tumbaku ni nzuri, pia amewaomba wakulima kuhakikisa wanafunga vizuri tumbaku zao ili zikifika sokoni kusiwepo na kukataliwa.
“Tunapenda sana tunapokuja kununua tumbaku kama imeandaliwa mitumba elfu tatu basi tununue yote elfu tatu inaporudi kama Bitimanyanga walikuwa na masoko manne ukirudisha mitumba tayari unatengeneza soko la tano na uendeshaji wa soko ni gharama.” Alisema Ramadhan.
"Niendelee kuwasisitiza na kuwaomba ndugu zetu wajumbe kila mmoja kwa nafasi yake tupambane wote kwa pamoja tuhakikishe wanafunga vizuri na wakileta mitumba yao yote inunulike." Aliongeza Ramadhan.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.