Kamati ya Uendeshaji ya Halmashauri ya Wilaya Ya Chunya (CMT) imewataka idara ya Elimu awali na msingi kuendelea kutafuta maeneo zaidi yatakayotumika kujenga shule nyingine za Mchepuo wa Kiingereza maana wilaya ya Chunya inakua kwa kasi hivyo lazima na mahitaji ya shule za mchepuo wa kiingereza yataongeza
Rai hiyo imetolewa leo 27/11/2023 na CMT ikiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Ndugu Athuman Bamba akikaimu nafasi ya Mkurugenzi mtendaji baada ya kamati hiyo kutembelea shule ya Chunya Pre & Primary English Medium School inayomilikiwa na Halmashauri ya wilaya ya Chunya ilipoenda kukagua eneo ambalo yanajengwa madarasa manne ambapo chanzo cha fedha za ujenzi ikiwa ni mapato ya Ndani
“Maeneo zaidi yatafutwe kwaajili ya ujenzi wa shule nyingine za mchepuo wa Kiingereza maana wilaya ya Chunya inakua kwa kasi hivyo uhitaji wa huduma kama hii utakuwa ni mkubwa kuliko sasa hivyo afisa Elimu awali na msingi jaribu kutafuta maeneo makubwa na mazuri kwaajili ya kujenga shule za namna hii” Amesema Ndugu Bamba
Naye Kaimu Mkuu wa idara ya Mipango na uratibu ndugu Nebart Gavu ameshauri uongozi wa shule kwakushirikiana na ofisi ya Afisa Elimu awali na msingi waandae mpango unaoonesha lengo la shule hiyo ni kuhudumia wanafunzi wangapi na idadi hiyo itumike kukadiria idadi ya majengo yanayokusudiwa na baadaye eneo lote lipangwe mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza hapo baadaye
“Naomba muandae mpango kazi kwamba shule hii inahitaji kuwa na madarasa mangapi na orodha hiyo tukiipata wahandisi waandae mpango wa matumizi ya eneo maana tukichelewa kufanya hivyo inaweza kuleta changamoto hapo baadaye na zile kauli za kwamba tungejua mapema jengo Fulani tungejenga hapa au pale” Alisema Nebert Gavu
Akifafanua baadhi ya mambo yaliyoulizwa na kamati hiyo kaimu Afisa Elimu awali na msingi wilaya ya Chunya Mwalimu Abdallah Mcheru amesema lengo la awali la kujenga shule hiyo ilikuwa ni kila darasa kuwa na mikondo miwili kwa kila darasa lakini amesema jambo la kuleta mapendekezo ya matumizi bora ya eneo la shule hiyo yatafanyiwa kazi kwa wakati na kuyawasilisha kwenye vikao vijavyo
“Usajili wa shule hii kwasasa ni mikondo miwili kwa kila darasa kwa maana ya wanafunzi 90 yaani arobaini na tano kwa kila mkondo lakini sasa ni kweli kuna haja ya kujadili mwendelezo wa shule hii na sisi tutayafanyia kazi mapendekezo hayo” Amesema Mwalimu Mcheru
Ziara hiyo imekuja baada ya kikao cha asubuhi ya leo Mhandisi wa Halmashauri Eng Charles Kway kupitia Afisa Elimu Msingi kuwasilisha mchoro wa ujenzi wa madarasa manne wenye mabadiriko baada ya mchoro wa awali kutokutosha kulingana na eneo hilo na ndipo mwenyekiti alishauri wajumbe kufika eneo la ujenzi na kushauri yote yanayowezekana kushauri
Kupitia mapato ya ndani Halmashauri ya wilaya ya Chunya inajenga madarasa manne kwa gharama ya shilingi milioni mia moja (100) katika shule ya Mchepuo wa Kiingereza Chunya ili kujiandaa kwa mwaka wa masomo 2024 ambapo mpaka sasa fedha hizo zimetolewa na tayari taratibu mbalimbali za ujenzi zinaendelea
Picha za Madarasa yanayojengwa shule ya Mchepua wa Kingereza Chunya, Mchoro huo umetengezwa na wataalamu (Wahandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya
Wajumbe wa kamati ya uendeshaji ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya wakiwa eneo linalojengwa madarasa manne Shule ya awali na msingi mchepuo wa Kiingereza Chunya (Aliyenyoosha mkono mwenye suti nyeusi ni kaimu Mkurugenzi mtendaji Mwana Athuman Bamba na ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao kilichoamua kutembelea eneo hilo, na mwingine aliyenyoosha mkono ni Mhandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Eng Charlse Kway)
Wajumbe kamati ya uendeshaji ya Halmashauri ikiendelea kushauriana mambo mbalimbali kuhusu ujenzi wa madarasa katika shule ya Mchepua wa Kiingereza Chunya (Aliyeshika Karatasi Ni Mhandisi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Eng Charlse Kway, anayefuata kulia kwake na amenyoosha mkoa ni kaimu mkuu wa idara ya Mipango na Uratibu ndugu Nebart Gavu na anayefuata ni Mweka hazina wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Ndugu Rajabu Lingoni
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.