MRADI wa kuendeleza haki na ulinzi wa ardhi kwa wazalishaji wadogo kwa uhakika wa chakula umefanya kikao cha wadau wa masuala ya ardhi Wilaya ya Chunya Machi 8, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Mradi huo unaoendeshwa na shirika la MIICO unatekelezwa katika mikoa mitatu ambayo ni Mbeya, Rukwa na Njombe ambapo kwa upande wa Mkoa wa Mbeya, mradi huo unafanyika Wilayani Chunya katika Kata za Sangambi na Upendo.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa MIICO Bi. Catherine Mulanga amesema lengo la programu hiyo ni kuwawezesha wazalishaji wadogo hasa wakulima na wafugaji katika kuhakikisha wanapata ardhi bora kwa ajili ya uzalishaji.
“Tunalenga katika kuhakikisha wazalishaji wadogo wanaweza kupata ardhi, wamiliki kisheria, ni haki yao lakini kuhakikisha tunakuwa na uhakika wa chakula”. Alisema Bi. Catherine.
“Leo tumekuwa na kikao hiki ili kuwakutanisha wadau wa ardhi, sio wa Kata za Sangambi na Upendo peke yao, ila ni wadau wote wanaohusiana na ardhi katika Wilaya ya Chunya, kwa pamoja tujadili masuala yanayohusu ardhi katika Wilaya yetu.” Aliongeza Bi. Catherine.
Programu hiyo inatekelezwa na shirika la MIICO ambalo linatekeleza mradi wa ushawishi wa upatikanaji wa ardhi bora kwa wazalishai wadogo katika Wilaya ya Chunya kata za Sangambi na Upendo kwenye vijiji 6 ambavyo ni Sangambi,Shoga, Itundu, Nkwangu,Upendo na Lola.
Mradi huo umewajengea uwezo wananchi katika kutambua sheria mbalimbali na matumizi bora ya ardhi ambapo kupitia mradi huu wananchi mbalimbali wameweza kutambua umuhimu wa kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi, ambapo jumla ya wananchi 153 wamejiandikisha kwa ajili ya kupimiwa maeneo yao ili kupata hati za kimila.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa kikao Mh. Bosco Mwanginde ambaye ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Chunya ameliomba Shirika la MIICO kufika katika maeneo mengi zaidi ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi.
“Mimi naomba Shirika lenu liweze kutanuka, badala ya kata mbili liongeze wigo kwenye maeneo mengine kwa namna yoyote ile ili watu wapate elimu ya ardhi ili kuondoa migogoro tunayokutana nayo huko.” Alisema Mwanginde.
Aidha Mwanginde ameutaka uongozi wa ardhi Wilaya kuhakikisha vijiji vyote ambavyo havina ramani na bikoni vipatiwe ili kuweza kuondoa migogoro ya ardhi kwenye maeneo hayo.
Pia amewataka MIICO kwa kushirikiana na Maafisa Ardhi wa Wilaya kuhakikisha wanakwenda kwa wananchi kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi ili jamii iwe na uelewa wa masuala ya ardhi.
“Msiishie tu kwa sisi viongozi hii nafikiri ikienda kwenye mikutano ya hadhara wananchi wakipata elimu itakuwa ni vyema zaidi, kama mtapanga ratiba yenu kwenda kutoa elimu kwenye maeneo mbalimbali kwenye mikutano ya hadhara inaweza kuwa na maana kidogo.” Alisema Mwanginde.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.