Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Mheshimiwa Ramadhani Shumbi amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kwendelea kushikamana na kusimama kwa nguvu moja katika kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Halmashauri inaendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuvuka lengo lililokusudiwa la kukusanya Shilingi Bilioni 38 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani na nje mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Chunya.
Hayo ameyasema Septemba, 22/2024 kwenye kikao cha Baraza la madiwani lililoketi katika ukumbi Halmashauri ya Wilaya ya Chunya jengo jipya la Utawala.
Aidha, Mheshimiwa Shumbi amesema Halmashauri imeidhinisha kukusanya kiasi cha bilioni 38 kutoka vyanzo vya ndani na nje, mpaka kufika mwezi Septemba, 2024 Halmashauri imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 12 sawa na asilimia 33 ya makusanyo yote huku akihimiza kuendeleza kasi ya ukusanyaji mapato .
“Halmashauri ya Wilaya ya Chunya inaendelea kuwa miongoni mwa Halmashauri zinazofanya vyema katika maeneo mbalimbali ikiwemo ukusanyaji wa mapato ambapo hadi kufikia robo ya kwaza tumeweza kukusanya mapato kwa asilimia 30 ikiwa ni zaidi ya asilimia 5 ya lengo la ukusanyaji mapato, kazi ya ukusanyaji mapato ni yetu sote nasisitiza zoezi hili liendelee kwa kasi mpaka utakapomalizika mwaka wa fedha 2024/2025” amesema Mhe. Shumbi.
Ameongeza kwa kusema, Halmashauri itaendelee kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato kwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kufikia malengo ya ukusanyaji mapato na kuwaletea wananchi maendeleo kupitia ilani ya chama cha mapinduzi, amesema Mhe. Shumbi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Alhaji Batenga amemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kufuatilia madeni ya wadau mbalimbali ikiwemo kampuni ya Tumbaku ambayo inadaiwa zaidi ya Shilingi bilioni 3 ili kufikia lengo la kukusanya shilingi bilioni 38 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
“Halmashauri ya Wilaya ya Chunya tumepanda daraja kutoka asilimia 40 mpaka asilimia 60 katika kutekeleza miradi ya maendeleo, lengo la mwaka wa fedha 2024/2025 ni kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 38, Mkurugenzi fuatilia tunaowadai wote ikiwemo kampuni ya Tumbaku tunaowadai shilingi bilioni 3.5” amesema Mhe. Batenga.
Katika hatua nyingine, Mhe. Batenga amewataka madiwani wa Wilaya ya Chunya kuwahimiza wananchi wao kwenda kupiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa itakapofika tarehe 27 Novemba, 2024 huku akieleza idadi ya wananchi waliojiandikisha ni asilimia 80 kati ya wananchi 18,544 ya idadi ya wakazi katika kata zote 20 za Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
“Asilimia 80 ya waliojiandikisha kwenye daftari la mkazi lazima ionekane kwenye zoezi la kupiga kura kila mmoja kwa nafasi yake ahakikishe anawahimiza wananchi kwenda kupiga kura” amesema Batenga.
Mkutano wa Baraza la Madiwani robo ya Kwanza kwa kipindi cha Julai hadi Septemba umehudhuriwa na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, katibu wa chama cha Mapinduzi, Wataalam mbalimbali kutoka Halmashauri , Wananchi pamoja na Waandishi wa Habari.
waheshimiwa Madiwani wakiendelea kupitia taarifa mbalimbali za robo ya kwanza kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba wakati wa kikao cha baraza la robo ya kwanza kilichoketi katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri (Jengo jipya la Utawala).
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.