Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mbarak Alhaji Batenga amewashukuru viongozi wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) jimbo la Lupa kwa moyo wao wa kujitoa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kutoa mifuko mia moja ya Saruji kwa uongozi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Makongolosi ili saruji hiyo itumike kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kujengwa.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi saruji hiyo kwa uongozi wa kata ya Bwawani na kata ya Makongolosi iliyofanyika leo tarehe 12/07/2024 kwenye viwanja vya soko la Makongolosi Mhe Batenga amesena Serikali inapenda aina hiyo ya ushirikiano kwani unalenga kuwahudumia wananchi wale wale ambao upande wa Serikali wanaitwa wananchi na upande wa Madhehebu huitwa waumini
“Kila kata hapa imepokea mifuko hamsini ya saruji, bwawani imepokea mifuko hamsini Makongolosi imepokea mifuko hamsini, Nirudie tena kuushukuru uongozi wa Kanisa la TAG kwa jinsi ambavyo waliguswa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo na kutoa saruji mifuko mia moja yenye thamani ya zaidi ya milioni mbili, wameonesha moyo wa kujitolea sana na sio kwamba wao hawana miradi bali ni kuwahudumia wananchi, na huu ndo ushirikiano tunaoupenda” Amesema Mhe Batenga
Aidha Mhe Batenga amewashukuru viongozi wa dini zote kwa namna ambavyo wanaunga mkono juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania kwa namna tofauti tofauti kwani zipo taasisi mbalimbali zinazo milikiwa na madhehebu mbalimbali zinatoa huduma kwa wananchi maeneo mbalimbali
“Madhehebu ya dini yanachangia sana katika kutoa huduma kwa jamii, kama mnavyofahamu kuna shule, vyuo katika viwango mbalimbali, hospitali vyote vinamilikiwa na madhehebu ya dini lakini huwahudumia wananchi, hivyo sisi Serikali tuna uhusiano mzuri kabisa na madhehebu yote maana sote tunawahudumia wananchi wale wale kwa namna moja au nyingine” Ameongeza Mhe Batenga
Awali akitoa taarifa ya uwepo wa Saruji hiyo mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo Makongolosi Ndugu Linus Mwanitega akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya amesema Saruji hiyo ilikabidhiwa na uongozi wa Kanisa la TAG ikiwa ni hitimisho la maadhimisho ya miaka 85 ya kanisa lao na lengo lao ilikuwa ni kuungana na Serikali kuendelea kujenga miundombinu katika kata mbalimbali za Mamlaka ya mji mdogo wa Makongolosi.
Kwa niaba ya wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo la kukabidhi saruji hiyo, Bwana Efrahim Kanyenye ambaye pia ndiye mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Makongolosi amewashukuru viongozi wa Kanisa la TAG kwa kuwaptia saruji hiyo na ameiomba Serikali kuendelea kupeleka miradi kwenye kata hiyo kwani wataisimamia kwa weledi
Mtendaji wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Makongolosi Bwana Linus Mwanitega akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa wilaya ya Chunya wakati alipokuwa akisikiliza kero za wananchi wakati wa Hafla ya kukabidhi saruji kwa uongozi wa Kata ya Bwawani na Makongolosi mapema leo
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kata ya Makongolosi Ndugu Efrahim Kanyenye akitoa shukrani zake kwa kanisa la TAG baada ya kata yake kupokea mifuko Hamsini ya Saruji kutoka kwa uongozi wa Kanisa hilo iliyokabidhiwa leo na Mkuu wa wilaya ya Chunya
Sehemu ya Saruji iliyokabidhiwa kwa uongozi wa kata ya Bwawani na Makongolosi mapema leo, Saruji hiyo ilitolewa na Uongozi wa Kanisa la TAG Jimbo la Lupa ili kuungana na Serikali katika kutekeleza miradi ya Maendeleo katika wilaya ya Chunya
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.