Mkuu wa wilaya ya Chunya Mrakibu mwandamizi wa Uhamiaji Mhe Mbarak Alhaj Batenga amefanya mazungumzo na Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Mbeya ili kupata ufumbuzi wa haraka kwa changamoto ya Barabara ya kuelekea Sambilimwaya na Barabara ya Matundasi –Itumbi kwani maeneo hayo yana idadi kubwa ya watu lakini yana uzalishaji mkubwa unaochangia pato katika Halmashauri na Taifa kwa ujumla
Mazungumzo hayo yamefanyika leo ofisini kwa Mkuu wa wilaya na baadaye kufanya ziara ya kuzitembelea barabara hizo, Mkuu wa wilaya ya Chunya amemwambia Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mbeya kwamba barabara ya Matundasi-Itumbi itazamwe kwa upya kulingana na shughuli za kiuchumi zilizopo katika eneo hilo kwani zinamchango mkubwa kwa Halmashauri na Taifa lakini Barabara ya Mnazi mmoja kwenda Sambilimwaya ikiwezekana iingizwe haraka kwenye mtandao wa barabara na ianze kutengenezwa ili wananchi wanaoishi kwenye kitongoji hicho waendelee kuifurahia serikali ya awamu ya sita
“Najua TARURA mna mchakato wenu wa namna ya kuingiza barabara kwenye mtandao wenu ili ianze kutambulika lakini naomba mchakato ufanyike kwa haraka ili wananchi wanaoishi kwenye kitongozi hicho wapate barabara, lakini Barabara ya Matundasi-Itumbi itazamwe kwa jicho la pekee sana kwani idadi ya wakazi wa eneo hilo ni kubwa lakini pia shughuli za uzalishaji mali zinazoendelea zinamchango mkubwa kwenye mapato ya Taifa hilo” Amesema Mhe Batenga
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mbeya Mhandisi Albert Kindole amekiri kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa matengenezo ya Barabara hizo baada ya kuzikagua huku akisema pamoja na milioni 92 ambazo tayari Mkandarasi ameanza kazi katika barabara ya Itumbi lakini barabara hiyo imetengewa shilingi milioni 450 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwaajili ya Matengenezo makubwa
“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya nimekubaliana na mazungumzo tuliyofanya pale ofisini, ni kweli barabara hizi ni muhimu, uwepo wa Mabasi 17 hapa Itumbi ni ishara tosha kwamba Barabara hiyo ni muhimu na inahitaji matengenezo ili kuwarahishia wananchi upatikanaji wa usafiri, hivyo pamoja na million 92 ambazo tayari mkandarasi yupo kazini pia kwa mwaka 2024/2025 Barabara hii imetengewa shilingi milioni 450, Pamoja na hayo nafikiri ofisi yangu itaenda kuandika andiko maalumu ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami hapo mbeleni” Amesema Mhandisi Kindole
Diwani wa kata ya Matundasi Mhe Kimo Choga amesema wananchi wa Matundasi wanapenda maendeleo na wako tayari kujitoa kwani kupitia nguvu za wananchi pamoja na michango mbalimbali ya wadau tayari wameendelea na ujenzi wa majengo mbalimbali kwaajili ya sekondari ambayo tayari ilishapewa jina na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati alipofanya ziara yake katika kitongoji cha Itumbi na kubaini changamoto ya umbali wa shule ya Kata hiyo ambayo imejengwa Matundasi umbali wa Kilomita 12
Ernest Mwakibete, Adamu Mwampiki, Godfrey Mataluma, Oden Mwakanyamale, Mussa Mohamed na wengine kwa niaba ya wananchi wengine walimweleza Mkuu wa wilaya kuhusu changamoto mbalimbali zinazohitaji kutatuliwa huku Barabara ikiwa changamoto kubwa na imezungumzwa na watu wote waliopata nafasi na imeshapatiwa majibu
Ziara hiyo iliyohusisha kamati ya Usalama ya wilaya pamoja na meneja wa TARURA Mkoa sambamba na meneja wa TARURA wilaya ya Chunya imekuja ikiwa ni siku chache baada ya kamati ya siasa kupita kukagua utekelezaji wa Ilani na baadaye kamati ya Fedha, uchumi na Mipango ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya kupita kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya huku miradi ya TARURA ikiwa ni kati ya miradi iliyokaguliwa
Meneja wa wakala wa barabara za vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mbeya Mhandisi Albert Kindole (Aliyenyoosha mkono) akizungumza jambo kwa Mkuu wa wilaya ya Chunya mapema leo kabla ya ziara ya kukagua barabara za Sambilimwaya na Itumbi
Mkuu wa wilaya ya Chunya akiongozana na kamati ya usalama ya wilaya sambamba na Meneja wa TARURA Mkoa wa Mbeya wakikagua barabara ya Matundasi-Itumbi mapema leo
Diwani wa kata ya Matundasi Mhe Kimo Choga akipiga magoti mbele y aMeneja wa wakala wa barabara za vijijini na mijini TARURA Mkoa wa Mbeya Mhandisi Albert Kindole akiomba kutengezwa kwa barabara ya Matundasi-Itumbi ili wananchi wake waweze kusafiri pamoja na kufanya shughuli nyingine za kiuchumi kwa urahisi
Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Itumbi wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Batenda alipowatembelea na kuzungumza nao mapema leo (Pamoja na hali ya Mvua wananchi hao waliendelea kumsikiliza Mkuu wa wilaya kwa makini)
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.