WAHESHIMIWA madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya wamewapongeza Wataalamu wa Halmashauri na kuwataka kuhakikisha wanatekeleza miradi yote inayoendelea katika wilaya hiyo kwa ubora na kuikamilisha kwa wakati uliopangwa
Pongezi hizo zilitolewa wakati wa ziara ya Madiwani hao walipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri, Mh Bosco Mwanginde amesema, lengo la ziara hiyo ni kujiridhisha juu ya fedha wanazozituma kwenda kwenye miradi kama zinafanya kazi iliyokusudiwa.
"Tunawapongeza kwa utekelezaji wa miradi kwani tunaona kuwa miradi mingi inayotekelezwa ndani ya Wilaya ya Chunya inaonesha imetekelezwa kwa kiwango kizuri na thamani ya fedha inaonekana, Waheshimiwa Madiwani wameutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kukamilika ili iweze kuwanufaisha wananchi na sio mradi unaanzishwa na kubaki kiporo,“ alisema Mwanginde.
"Ilikuwa inatokea huko nyuma mradi unakaa mpaka miaka mitatu, lengo letu ni kutatua matatizo kama tumeanza lazima tuukamilishe huo mradi” Aliongeza Mwanginde.
Aidha Madiwani wameielekeza menejimenti kufanya marekebisho kwa baadhi ya miradi ambayo waliitolea ushauri ili kuifanya miradi hiyo kuwa na tija kwa jamii na Wilaya kwa ujumla.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chunya Ndg. Tamim Kambona amewahakikishia Madiwani kuwa watayafanyia kazi maelekezo yote na ushauri ambao wameutoa katika miradi yote, ambapo Kambona amesema Halmashauri imejipanga kuhakikisha kwenye vituo vyote vya afya vyenye changamoto ya maji Halmashauri itachimba visima ili kuondoa changamoto hiyo.
“Mwaka huu wa fedha tutaanza na katika vituo tutaanza vile ambavyo vimeanza kutoa huduma” Alisema Kambona.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Bosco Mwanginde sanjari na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Ndg. Tamim Kambona, Waheshimiwa Madiwani walikagua ujenzi wa shule shikizi Manyili iliyopo kijiji cha Sipa kitongoji cha Manyili, ujenzi wa kituo cha Afya Kambikatoto pamoja na kituo cha Afya Mafyeko.
Aidha Waheshimiwa Madiwani walitembelea ujenzi wa hospitali ya Wilaya, soko la madini, kituo cha afya Sangambi, ujenzi wa uzio katika mnada wa mapogoro pamoja na ujenzi wa jengo la utawala.
|
|
Waheshimiwa Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chunya wakikagua Ujenzi wa Jengo la IMD katika hospitali ya wilaya yaChunya
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya Dr. Darison Andrew aliyevaa shati Jeupe akitoa maelezo kwa Waheshimiwa Madiwani wa halmashauri walipotembelea hospitali ya wilaya kukagua miradi inayotekelezwa haspitalini hapo
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.