WAKUU wa Wilaya ya Chunya na Mbeya Vijijini wameumaliza mgogogro wa ujenzi wa miradi ya maji baina ya wakazi wa kijiji cha Ikukwa Wilaya ya Mbeya na kijiji cha Ifumbo kilichopo Wilaya ya Chunya.
Hivi karibuni kulizuka mgogoro kwenye utekelezaji wa miradi ya maji kwenye maeneo hayo hadi kusababisha wananchi wa kijiji cha Ikukwa kuzuia kuendelea kwa mradi huo.
Wilaya za Mbeya na Chunya zinatekeleza ujenzi wa miradi ya maji katika vijiji vya Ikukwa na Ifumbo ambapo chanzo kikuu cha maji kipo katika kijiji cha Ikukwa Wilaya ya Mbeya.
Wakati injinia wa maji Wilaya ya Chunya akitekeleza mradi huo kwa kuanza kupeleka vifaa vya kazi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi ndio, kukaibuka mzozo na kusababisha kuzuia kuendelea kwa mradi huo.
Wananchi wa kijiji cha Ikukwa wanadai kutoshirikishwa katika mchakato wa makubaliano ya kupeleka maji katika kijiji cha Ifumbo, hivyo kusababisha kutoridhia kuendelea kwa mchakato huo.
Kwa upande wa Chunya, mradi huo unatekelezwa kwa fedha za ufadhili wa Water Charity chini ya CRS kwa kushirikiana na Serikali ambapo mradi huo unakadiriwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 600.
Mradi wa maji kijiji cha Ikukwa unatekelezwa kwa fedha za serikali kupitia mfuko wa maji na mradi huu unakadiriwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 474.
Akizungumza wakati wa utatuzi wa mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe. Mayeka S Mayeka amesema wao kama wawakilishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi kubwa ni kusikikiza wananchi wanataka nini na kutatua matatizo yao.
“Sisi wote tupo Mbeya, mimi naweza kuhamishwa na kuletwa Mbeya Vijijini na mwenzangu kupelekwa Chunya, lakini wote tupo kwenye mkoa mmoja, tunawahudumia watanzania wale wale," alisema mayeka.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Rashid Chuachua amewaasa wananchi wa kijiji cha Ikukwa kutokuwa na wasiwasi kwani miradi itatekelezwa kwa pande zote mbili.
“Tumekuja hapa sababu tunataka mradi utekelezwe, kwa hiyo niwasihi na niwaeleze kwamba hapa hakuna udanganyifu kwa pande zote mbili, fedha zipo kwenye akaunti na utekelezaji wa mradi ni miezi sita,” alisema Chuachua.
Tumekuja kwanza kuwathibitishia kwamba mradi utaanza kutekelezwa na tungekuwa hatuna uhakika tusingekuja kwa sababu muda uliopo ni mfupi, tunahitaji fedha zitumike ili mradi uweze kutoa matunda yake," aliongeza Chuachua.
Kwa usanifu uliofanyika maji yanayokwenda kuvunwa kwenye chanzo hicho ni lita 1.5 milioni ambapo kwa kijiji cha Ikukwa, lita zinazohitajika ni lita laki mbili na nusu na kwa upande wa Ifumbo, lita laki mbili yanahitajika kwa shughuli mbalimbali za wakazi wake.
Aidha, Chuachua aliwaasa viongozi wa vijiji kuwashirikisha wananchi kwenye shughuli za kimaendeleo ndani ya vijiji vyao kwani itaondoa migogoro midogomidogo ndani ya jamii.
“Nduu zangu, hapa sisi tunahitaji maendeleo, hakuna mtu asiyetaka maji ya bomba na kilikuwa kilio chenu cha muda mrefu, mimi nadhani kama maoni ya wenzetu waliozungumza kwamba hakuna changamoto, nadhani tusimamie hapo tukatekeleze huu mradi wa maji." Alisema Chuachua
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe. Mayeka S. Mayeka akizungumza na Wakazi wa kijiji cha Ikukwa wakati wa utatuzi wa mgogoro kati ya Ikukwa na Ifumbo
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Vijijini Mhe. Rashid Chuachua akizngumza wa Wananchi wa kata ya Ikukwa wakati wa utatuzi wa mgogoro wa utekelezaji wa miradi ya maji kati ya kijiji cha ikukwa na kijiji cha Ifumbo
Wananchi wa Kata ya Ikukwa wakiwa kwenye Mkutano
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.