MBUNGE wa jimbo la Lupa Mhe Masache Kasaka amesema, kukamilika kwa zahanati ya kijiji cha Itumba iliyopo Kata ya Chalangwa Wilayani Chunya kutawafanya wakazi wa Wilaya hiyo kuimarika afya zao kwa kupata huduma za afya kwa uhakika.
Mheshimiwa Kasaka amefanya uzinduzi huo Mei 9, 2022 ambapo alielezea furaha yake ikiwa mwaka jana alifika kwenye jengo la zahanati hiyo na kuahidi kukamilisha ujenzi wake kwa maslahi mapana ya wana Chunya kwa ujumla.
“Mwaka jana nilivyokuja kuwashukuru nilifika hapa na kuitembelea zahanati hii, tukakuta ipo usawa wa linta, na nikawaahidi kwenda kutafuta fedha ili kukamilisha ujenzi, leo ninayo furaha nilichoahidi jengo limekamilika na huduma zinaanza kutolewa.
“Ndugu zangu wanaitumba kukamilika kwa zahanati yetu hii tunaenda kuhakikisha afya zetu zinaendelea kuwa bora zaidi, ili mambo mengine yaendelee vizuri, cha kwanza tuwe na afya njema na imara.” Alisema Mheshimiwa Kasaka.
Aidha, aliongeza kwa kusema ili kuwa na afya njema na imara lazima kuwe na zahanati na vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma ili wananchi waweze kuhudumiwa kwa ukaribu zaidi.
Kwa upnde wa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Dkt. Darison Andrew alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa kijiji cha Itumbi kwa kujitoa kwenye shughuli za maendeleo hasa katika ujenzi wa zahanati.
Aliongeza kwa kusema kuwa, siku ya Alhamisi ya Mei 12, 2022 kutakuwa na kampeni ya awamu ya pili ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuwapeleka watoto wao kwenda kupata chanjo hiyo.
“Ugonjwa huu hauna tiba ila una kinga, na kinga ina kinga kwa asilimia 100, mtoto akiumwa polio kuna matokeo mawili, na yote ni mabaya aidha apoteze maisha ama apooze na akipooza hawezi kupona, hivyo tunawaomba sana sana mjitokeze kwa wingi, muwalete watoto wenu kupata chanjo ya polio.
Uzinduzi wa zahanati hiyo umeenda sambamba na harambee ya kuchangia ukamilishwaji wa nyumba ya Mganga ambapo jumla ya shilingi milioni 6.5 zilikusanywa.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.