Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria ndugu, Eliakim Maswi amefungua mafunzo ya siku moja kwa wataalamu wa Halmashauri za Mkoa wa Mbeya utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria wa Mama Samia huku akiwataka wataalamu kwenda kutoa msaada wa kisheria bure bila malipo kwa wananchi wasio na uwezo wa kulipa gharama za wakili kutatua changamoto zao za kisheria zinazowakabili
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo leo Februari 23, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, ndugu Eliakim Maswi amesema Wizara imekamilisha kampeni ya msaada wa kisheria katika mikoa 17 nchini ambapo amewataka wataalamu kwenda kutoa msaada huo wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo wa kulipa gharama za wakili ili kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi.
“Nimeona Watumishi wa Chunya hapa, kwasababu wananchi wanaonewa sana kuna mwananchi mmoja kapokonywa ng’ombe zake 57, mbuzi, kuku na punda na dalali wa mahakama huku maamuzi ya mahakama ni kuchukua ngo’mbe 20 yule ni mtanzania na yupo kwenye nchi yake hatuwezi kukubali hali hii iendelee” amesema Eliakim Maswi.
Aidha, Katibu Mkuu Maswi ametoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanaenda kuwasaidia wananchi kwa kiasi kikubwa kwenye msaada wa kisheria kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo migogoro ya ardhi pamoja na mirathi.
Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa kisheria wa Mama Samia, Wakili Athumani Bamba, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, amesema nimepokea maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria kuhusu mgogoro huo wa mkulima wa Chunya na dalali wa mahakama huku akiahidi kufuatilia kwa karibu na kutafuta suluhisho la haraka.
“Awali sikufahamu kuhusu mgogoro huo, ndio nimesikia hapa, sasa baada ya mafunzo haya ninaenda kufuatilia kwa karibu kujua suala hili kwa undani wake, nimpate huyo mkulima, nimpate dalali na nijue mahakama gani imetoa uamuzi ili tumsaidie huyu mkulima apate haki yake na ikiwezekana mifugo yake iweze kurudi” amesema wakili Bamba.
Akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia,Mkurugenzi wa huduma za kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Mwasheria Ester Msambazi amesema lipo ombwe kubwa la wananchi kutokuelewa sheria ndio maana Wizara ikaja na msaada huu wa kisheria ambayo inajulikana kama Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) ambapo malengo ya Kampeni ni kuongeza uelewa wa wananchi kutatua migogoro.
Wataalamu kutoka kwenye Halmashauri za mkoa wa Mbeya wamehudhuria mafunzo ya msaada wa kisheria wa Mama Samia ambapo wataalamu hao watatoa huduma ya msaada wa kisheria kwa muda wa siku kumi bila malipo kwa wananchi wa Halmashauri za Mkoa wa Mbeya.
Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria ndugu, Eliakim Maswi akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chunya wakati wa uzinduzi wa Mafunzo ya kampeni ya msaada wa Kisheria wa Mama Samia uliofanyika leo Februari 23, 2025 katika ukumbi wa Mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Mtoa mada wakiwasilisha kutoka Wizara ya Katiba na Sheria akiwasilisha andiko lake kwa washiriki wa mafunzo ya utekelezaji wa msaada wa kisheria wa Mama Samia kutoka katika Halmashauri za Mkoa wa Mbeya.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.