Kamati ya Fedha, Uongozi na mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Chunya huku usimamizi mzuri wa Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wataalamu wengine ukitajwa kuwa ndio sababu ya miradi hiyo kutekelezwa vizuri.
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Mhe. Bosco Mwanginde akizungumza kwa niaba ya kamati ya hiyo mapema Oktoba 7, 2024 katika viwanja vya Shule ya Msingi Chemichemi iliyopo kata ya Chalangwa amesema kamati hiyo imeridhishwa na kasi ya mradi huo wa ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja katika shule hiyo.
“Kamati ya fedha na mipango imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa shule ya Chemichemi, Halmashauri itasaidia pale mulipokwama kupitia mapato ya ndani kukamilisha ujenzi” amesema Mhe. Mwanginde.
Aidha, Kamati hiyo kupitia mwenyekiti wa kamati iliagiza uongozi wa kamati ya ujenzi wa shule ya msingi Chemichemi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo ambapo wameagizwa kwamba ifikapo mwezi Disemba 2024 mradi uwe umekamilika na kwakufanya hivyo kutaongeza tija kwa wanafunzi kuendelea na masomo lakini kupokea wanafunzi wengine mwaka ujao.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa madarasa hayo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi ChemiChemi Mwalimu Crispin Laurent Lugwira amesema anaipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kwa kutoa fedha Shilingi millioni saba kwenye ujenzi wa majengo mawili na Ofisi moja katika shule hiyo huku akibainisha kazi zilizobaki kuwa ni kupiga lipu, kubeba mchanga kwaajili ya sakafu, kupaka rangi na kununua samani ikiwemo madawati.
“Tunawapongeza Halmashauri kwa kutuletea fedha za ujenzi na kazi inaendelea kazi tulizonazo kwa sasa ni kupiga lipu, kubeba mchanga kwaajili ya sakafu, kupaka rangi pamoja na kununua madawati ” amesema Lugwira.
Akifafanua baadhi ya hoja kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wilaya ya Chunya, Mkuu wa Idara ya elimu Awali na msingi Mwalimu Ferd Mhanze amesema idara ya elimu msingi itachangia mafuta ya gari lita 100 ili kurahisisha uchukuaji wa mchanga kujaza kwenye msingi wa vyumba vya madarasa mawili ambapo juhudi hizo zitasaidia kuharakisha ukamilishwaji wa mradi kwa wakati.
Kamati ya Fedha imefanya ziara yake ya kawaida kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 kukagua miradi ya Maendeleo ambayo inatekelezwa na Halmashauri ya wilaya ya Chunya ili kushauri au kutafuta namna sahihi ya kuhakikisha miradi itekelezwa kwa viwango, kwa wakati na kwa ufanisi kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali.
"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi"
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi ChemiChemi Mwalimu Crispin Laurent Lugwira akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi mbele ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya wakati kamati hiyo ilipotembelea Shuleni hapo kukagua maendeleo ya ujenzi
Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya wakiambatana na wataalam kutoka Halmashauri wakifuatilia kwa karibu maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi katika Shule ya Msingi Chemichemi iliyopo kata ya Chalangwa
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.