HALMASHAURI ya Wilaya ya Chunya imefanikiwa kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 4.1 kutokana na mapato ya ndani kwa kipindi cha robo tatu cha mwaka wa fedha unaoelekea ukingoni 2021/22.
Mapato hayo yaliyoingizwa katika kipindi cha miezi mitatu kutoka Januari hadi Machi mwaka huu, ni sawa na asilimia 86 ya malengo ya ukusanyaji mapato katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kilichofanyika Machi 13, 2022, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bosco Mwanginde amesema, dhumuni la kikao hicho ni kujadili mipango mbalimbali ya kimaendeleo ambayo wamejiwekea kwa utaratibu wa kila baada ya miezi mitatu.
“Naomba kuwaomba viongozi wenzangu kushirikiana na wataalam wetu katika kusimamia shughuli za maendeleo kwa uadilifu, uaminifu na ufuatiliaji wa karibu ili shughuli hizo za kimaendeleo ziweze kufanyika vizuri,” alisema Mwanginde.
Aidha, aliwaasa waheshimiwa madiwani na wataalam kuepuka kuanzisha migogoro isiyo ya lazima katika miradi wanayoisimamia.
Katika muda wa maswali ya papo kwa hapo, Mhe. Benson Msomba Diwani wa Kata ya Kasanga aliulizia mpango wa Halmashauri kuhusu kuhamisha machinjio yaliyozungukwa na makazi ya watu kutokana na kukua kwa mji.
Akijibu swali hilo Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Mwanginde amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imetenga eneo la machinjio ya kisasa katika kijiji cha Kibaoni ambapo halmashauri imepanga kutenga bajeti kwaajili ya kuanza hatua za awali za ujenzi wa machinjio hiyo.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya Mhe. Mwanginde amewataka waheshimiwa madiwani pamoja na wataalam wa Halmashauri kuhakikisha wanakusanya mapato kwa wingi ili kutimiza malengo waliyojiwekea.
“Hatuwezi kwenda na Halmashauri haiwezi kuendelea bila kuwa na mapato ya ndani, rai yangu kwenu waheshimiwa haya mambo yote tunayoyajadili hapa mapato ya ndani makusanyo yanatoka kwenye kata zetu twendeni tukashirikiane na wataalam wetu kukusanya mapato."
“Sisi kama madiwani ni wajibu wetu kuwa karibu na hii miradi, mradi ule ukiwa kwenye kata yako na ukausimamia vizuri unakupa heshima na wewe kwa sababu hautakuwa na ubadhirifu na hautajengwa kwa kiwango cha chini." Alisema Mwanginde.
Mhe. Ramadhan A. Shumbi makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya chunya akiwasilisha taarifa ya Kamati ya fedha, Uongozi na Mipango kwenye kikao cha baraza la madiwani kwa robo ya tatu.
Mh Anaklet Michombero katibu tawala wa wilaya ya chunya ambaye alimwakilisha Mkuu wa wilaya akitoa salamu za Mkuu wa wilaya kwenye kikao cha Baraza la Madiwani
Waheshimiwa madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya Tatu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya chunya Mh Bosco Mwanginde akifafanua jambo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.