Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ndugu Tamim Kambona ametoa rai kwa walimu Wakuu na Walimu wa madarasa ya elimu ya awali kwamba mwaka huu 2025 hataki kusikia kuna mwanafunzi wa darasa la tatu au darasa la nne hajui kusoma, kuandika na kuhesabu katika shule yoyote ile kwani wanafunzi wanapata lishe ya kutosha wanapokuwa shule hali inayoongeza umakini na uwezo mkubwa wa kuwasikiliza walimu wawapo darasani.
Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 18/01/2025 wakati akifungua mafunzo kwa walimu wakuu na walimu wanaofundisha madarasa ya awali juu ya njia na Vifaa vya Mtaala wa Elimu ya awali vilivyoboreshwa kwa walimu kutoka shule 48 za Halmashauri ya Wilaya ya Chunya yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Kibaoni.
“Mwaka huu Sitaki kusikia katika shule yoyote ile kwamba kuna mwanafunzi darasa la tatu na darasa la nne asiyejua kusoma, kuandika na kuhesabu na walimu mpo pale shuleni mnalipwa mshahara, sitarajii kuona kitu kama hicho kwani watoto wanapata lishe ya kutosha na wana ubongo mzuri hivyo wanauwezo huo, Mwanafunzi anatakiwa atoke darasa la awali akiwa anajua kusoma ,kuandika na Kuhesabu ” amesema Kambona.
Aidha Kambona amewataka walimu wakuu na Walimu wa elimu ya awali kusikiliza kwa makini mafunzo yanayotolewa ili wakayafanyie kazi kwenye vituo vyao kwani mafunzo hayo yatakuwa msaada mkubwa kwao kama walimu na kwa wanafunzi wanaokwenda kuwafundisa katika Shule zao kwasababu mafunzo hayo yamelenga njia na Vifaa vya Mtaala wa elimu ya awali ulioboreshwa
Awali akitoa taarifa ya Mafunzo hayo mratibu wa Miradi ya Boost Wilaya ya Chunya Mwalimu Abdallah Mchelu amesema kuwa lengo la mufunzo hayo ni kuwajengea uwezo walimu wakuu na walimu wanaofundisha elimu ya awali juu ya miongozo mbalimbali ya elimu ya awali, ushirikishwaji jamii katika elimu ya awali, upimaji wa elimu ya awali, kutengeneza zana zinazotumika kufundishia na mambo mengine mengi
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kibaoni na Mwalimu Jackson Laizer kutoka Shule ya Msingi Nkwangu kwaniaba ya walimu wengine walioshiriki Mafunzo hayo wamesema mafunzo waliyoyapata yatawasaidia katika kuandaa zana bora na mbinu za ufundishaji lakini pia yatawasaidia katika ufundishaji na wanafunzi katika kujifunza kupitia miongozo mbalimbali iliyotolewa na Serikali .
Mafunzo ya kuhusu njia na Vifaa vya mtaala wa elimu ya awali vilivyoboreshwa nchini chini ya afua ya mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kupitia mradi wa Boost yatatolewa kwa siku saba kuanzia tarehe 15/1/2025 na kuhitimishwa tarehe 21/01/2025 kwa walimu wakuu na na walimu wa elimu ya awali yameanza na Shule za msingi 48 kwa awamu ya kwanza kati ya shule 90 za halmashauri ya Wilaya ya Chunya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Chunya Nndugu Tamim Kambona akitoa rai kwa walimu wakuu na walimu wa elimu ya awali wakati wa kufungua mafunzo juu ya njia na vifaa vya mtaala wa elimu ya awali vilivyoboreshwa yaliyofanyika Shule ya msingi Kibaoni Wilayani Chunya.
Mwalimu Mkuu Shule ya msingi Kibaoni Mwl Gloria Ndelwa akieleza namna ambavyo mafunzo hayo yatawasaidia katika kufundisha na kujifunza kwa wanafunzi wa awali.
Mwezeshaji wa kitaifa ndugu Jerome Mwakifuna akiendelea kufundisha maada mbalimbali kwa walimu wakuu na walimu wa elimu ya awali wakati wa mafunzo juu ya njia na na vifaa vya mtaala wa elimu ya awali vilivyoboreshwa.
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.