MKUU wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon Mayeka amewataka waachama wa Lupa AMCOS kulipa madeni wanaodaiwa na wadhamini kwa wakati ili kuepuka adha zinazoweza kuwakuta ikiwemo kufilisiwa.
Mayeka ameyasema hayo alipofanya kikao na Wanachama wa Lupa AMCOS wanaojishughulisha na ulimaji wa zao la tumbaku katika ofisi za AMCOS hiyo.
“Hatujaja hapa kuzuia watu wasilipe madeni, isije ikawa watu wanajua Mkuu wa Wilaya amekuja kurusha taulo kwamba sasa hawatalipa, tumekuja hapa kuangalia taratibu zilizotumika ni sahihi, wanaodaiwa wanadaiwa kiasi hicho na huyo aliyekuja kama dalali yupo kihalali?” Alisema Mh. Mayeka.
“Kwa taratibu za kiushirika nyinyi wenyewe mnajua namna mnavyoishi na mnavyoshirikiana, kwa hiyo nyie ndio mnaweza kuendeleza Lupa AMCOS ni nyinyi wenyewe akaiuwa AMCOS yenu.” Alisisitiza Mh. Mayeka.
Aidha, Mheshimiwa Mayeka amewaasa wanachama hao kufuata utaratibu, kwani Serikali haipo tayari kukaa kimya na kuacha mambo yakiharibika.
“Sisi kama Serikali hatuwezi kukaa kimya tukaacha mambo yaende ndivyo sivyo, lazima kila kitu kifuate utaratibu, lakini sUala la kulipa hilo linaeleweka, kwa hiyo mtu asije akakaa akafikiri Mkuu wa Wilaya amekuja kuzuia watu wasilipe.” Alitahadharisha Mh. Mayeka.
Mayeka ameutaka uongozi wa AMCOS hiyo kuhakiki madeni yote upya na kuhakikisha wadaiwa wote wanashirikishwa kwenye uhakiki wa madeni hayo na kisha zoezi la kulipa liendelee.
“Mwende mkahakiki madeni yote, na yanapohakikiwa watu wa ushirika wawepo, mtu mmoja mmoja aende kuhakiki deni lake na Afisa Ushirika ayathibitishe hayo madeni.
Pia Mkuu wa Wilaya alitumia nafasi hiyo kusitisha zoezi la kufilisiwa na kukamatwa kwa wanachama wanaodaiwa ili kila uongozi na wanachama kuhakiki upya madeni yao.
“Mimi nadhani hili zoezi lililokuwa liendelee la kuja kufilisiwa na kukamatwa lisitishwe kwanza, mhakiki madeni yenu kila mtu aridhike kwamba hili ni deni langu halafu sasa tukae mnalilipaje”. Alisema Mayeka
Naye Mrajisi Msaidizi Mkoa wa Mbeya Bw. Richard Zengo alisema, vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa mujibu wa masharti na masharti hayo yanawekwa na wanaushirika wenyewe.
Aidha Zengo aliongeza kwa kusema kuwa, kuna kila sababu ya uongozi kuhakikisha unafanya marejeo mapya ya madeni ilikuwepo na uhalisia wa madeni na wadhamini wathibitishe kuwepo na madeni hayo.
Kwa upande wa Afisa Tarafa wa Tarafa ya Kipembawe Ndg. Kassim Kirondomara alieleza sababu mbalimbali zinazopelekea wanachama kuwa na madeni ndani ya AMCOS hiyo, akiitaja moja ya sababu kubwa ni wanachama kutorosha tumbaku na kwenda kuuza sehemu nyingine, na wengine kuuza pembejeo wanazopewa kwa ajili ya kilimo cha tumbaku.
“Kimsingi Mkuu wa Wilaya wapo watu ambao wametorosha tumbaku na wapo ambao wameuza pembejeo na kupelekea kulaza madeni kwa makusudi.” Alisema Ndg. Kirondomara
Wanachama wa LUPA AMCOS wakiwa kwenye kikao na Mkuu wa Wilaya ya Chunya kilichofanyika katika Ukumbi wa Lupa AMCOS
Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mh Mayeka Simon Mayeka wa katikati akiwa na Das wa wilaya ya Chunya Mh Anaklet Michombero pamoja na mwenyekiti wa Lupa AMCOS kwenye kikao kilicho wakutanisha Wanachama na Viongozi mbalimbali wa Wilaya
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.