Mkuu wa wilaya ya Chunya Mrakibu mwandamizi wa Uhamiaji Mhe Mbarak Alhaji Batenga amewataka vyama vya Ushirika, Makampuni yanayonunua Tumbaku na watu wote wanaohusika kwenye mchakato wa ununuzi wa Tumbaku kuhakikisha wanatenda haki kwa wakulima kwakuhakikisha mizani zinazotumika kupima Tumbaku kuthibitishwa na mamlaka husika ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Ametoa maelekezo hayo Jana tarehe 29/4/2024 wakati akizungumza na wakulima waliojitokeza kuuza Tumbaku kwenye Chama Cha Msingi Mtanila ikiwa ni Chama cha kwanza katika Mkoa wa Kitumbaku Chunya kuanza kuuza Tumbaku huku Kampuni ya Premium Active wakisema malipo kwa wakulima ambao Tumbaku yao imenunuliwa siku hiyo yatalipwa ndani ya siku 14 kwa mujibu wa Sheria.
“Niombe mizani inayotumika kupima mizigo ya Tumbaku ya wakulima iwe imethibitishwa na mamlaka husika ili mkulima aweze kupata haki yake kadiri ya kujituma kwake ili tusije tukaingia kwenye migogoro na wakulima kwani imeshatokea maeneo mengine mkulima anaamini ana kilo kadhaa na mizani inatoa jibu tofauti” Alisema Mhe Batenga
Aidha Mhe Batenga ameonya wakulima kujiingiza kwenye utoroshaji wa Tumbaku jambo ambalo linaweza kupelekea kukamatwa na kufunguliwa Mashitaka kwa Mujibu wa Sheria na Miongozo ya kilimo cha zao la Tumbaku hivyo wahakikishe kila mmoja anauza Tumbaku yake kwenye maeneo waliyokubaliana kuuza Tumbaku.
“Niwaombe wakulima, utoroshaji wa Tumbaku utahatarisha kupotea kwa haki yako maana tutakukamata na kukuweka ndani kwa mujibu wa Sheria, taratibu na miongozo ya zao la Tumbaku, Naomba msitoroshwe Tumbaku iwe kutoka Chama kimoja kwenda chama Kingine lakini pia kutorosha kwenda nje ya wilaya, hivyo kila mtu ahakikishe anatenda haki katika nafasi yake” Aliongeza Mhe Batenga
Fredy Essau Meneja wa kampuni ya ununuzi wa Tumbaku ya Premium Mkoa wa kitumbaku Chunya amesema wao kama Kampuni wanajivunia kuwa Kampuni ya kwanza kuanza ununuzi wa Tumbaku kwani lengo lao kama Kampuni ni kuwapa fursa wakulima lakini pia kwa kuanza mapema kununua Tumbaku itapelekea wakulima wanaofanya kazi na Kampuni ya Premium watapata fedha Mapema kuliko wengine
“Kimsingi najivunia sana kuwa Kampuni nunuzi kwa Chama Cha Msingi Mtanila na kama ulivyoona wakulima wamehamasika na niwapongeze wakulima wa Mtanila na kwa dalili hii maana yake wakulima watapata pesa kwa wakati na wataanza mapema maandalizi ya kilimo kwa Msimu ujao” Alisema Fredy
Kwa niaba ya wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika Mtanila Nuru Martini Kambaulaya amesema hali ya soko ni nzuri na Mitumba yao wataendelea kupeleka kwenye chama chao cha Msingi maana Bei ni nzuri tofauti na ilivyokuwa hapo awali hivyo wakulima wote tupeleke Tumbaku zetu kwenye vyama vya Msingi
Mkuu wa wilaya ya Chunya alifika kwenye Chama Cha Msingi Mtanila kuona zoezi la ununuzi wa Tumbaku linavyoenda na baadaye aliendelea na ziara yake ya kukagua miundombinu ya Barabara zitakazotumiwa na wakulima kusafirisha Tumbaku kutoka eneo moja kwenda kwenye Maghala ya Tumbaku tayari kwa kuuza Tumbaku hiyo kwa Makampuni waliyoingia nayo Mkataba.
Mkuu wa wilaya ya Chunya akikagua mwenendo wa soko la Tumbaku Chama cha Msingi cha Ushirika cha Mtanila Jana alipotembelea zoezi la ununuzi lililoanza Jana (Aliye vaa shati la Blue bahari ni Bw Faustine Mtweve Katibu wa wadau wa Tumbaku Mkoa wa Kitumbaku Chunya, Kushoto kwa Mkuu wa wilaya ni Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Chunya
Meneja wa kampuni ya ununuzi wa Tumbaku ya Premium Mkoa wa kitumbaku Chunya Bw Fredy Essau akizungumza Mbele ya Mkuu wa wilaya na wanachama wa Chama Cha Ushirika cha Mtanila Jana wakati Mkuu wa wilaya alipotembelea kuona mwenendo wa soko
Wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Mtanila wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Chunya alipotembelea kuona mwenendo wa soko la Tumbaku jana
Itigi Road
sanduku la posta: P.O box 73 Chunya
simu ya mezani: 025 2520121
simu ya mkononi: 025 2520121
Barua pepe: ded@chunyadc.go.tz
Copyright ©2017 Chunya District Council . All rights reserved.